2013-02-15 12:15:53

Iweni vyombo vya haki na amani, kwa kutetea na kulinda haki msingi za binadamu, kama njia ya kumuenzi Marehemu Askofu Msarikie


Marehemu Askofu mstaafu Amedeus Msarikie wa Jimbo Katoliki Moshi, alizikwa kwenye Kanisa kuu la Kristo Mfalme, Jimboni Moshi, Alhamisi tarehe 14 Februari 2013, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Tarcisio Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na kuhudhuriwa na Maaskofu wengine 21.

Sala za rambi rambi kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Tarcisio Bertone, katibu mkuu wa Vatican, zilisomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Francisco Montecillo Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania. Katika salam zake za rambi rambi, Baba Mtakatifu anamshukuru sana Marehemu Askofu Msarikie kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Aliandaa watu katika medani mbali mbali za maisha, akafanikiwa kuwatumia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na Jamii kwa ujumla. Ni kiongozi aliyefanikiwa kujenga urafiki na watu wengi zaidi, akafanikiwa kupima malengo yake kwa njia ya moyo na akili; akaonesha busara na hekima ya hali ya juu hadi mauti ilipomfika.

Umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka ndani na Nje ya Jimbo la Moshi ulikuwepo ili kumsindikiza Marehemu Askofu Msarikie aliyekuwa kweli ni mwalimu wa Imani, akatekeleza utume wake kwa kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, Jimbo Katoliki Moshi.

Ni Askofu aliyejali sana malezi mfungamano, yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho, kimwili na kiakili. Hayo yamesemwa na Askofu Ngalalekumtwa wakati wa mahubiri yake kwenye wa Ibada ya Misa ya Mazishi ya Askofu Msarikie ambaye aliwaongoza Watu wa Mungu, kwa unyofu na uaminifu mkubwa. Alijitambua na kumtambua kila mwamini kuwa ni kiungo muhimu cha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Alionesha upendo mkubwa kwa watu wake bila ubaguzi, akahimiza umoja na mshikamano wa dhati, changamoto endelevu kwa Familia ya Mungu Jimboni Moshi na Tanzania kwa ujumla.

Alijitoa kimaso maso kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania tangu mwaka 1987 hadi alipong'atuka madarakani kunako mwaka 2007. Alikuwa na mang'amuzi ya kina kuhusu mikakati na mipango ya shughuli za kichungaji na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mwenge ni matunda ya juhudi hizi, kwa ajili ya maboresho ya sekta ya elimu nchini Tanzania.

Ibada ya mazishi ya Askofu Msarikie ilihudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais mstaafu Benjamini Mkapa pamoja na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi pamoja na viongozi waandamizi kutoka Serikali ya Tanzania. Rais Kikwete katika salam zake za rambi rambi amesema kwamba, Marehemu Askofu Msarikie ni mtu aliyependa na kusimamia maendeleo kwa ajili ya watanzania wengi; akasimama kidete kufanya maboresho katika sekta ya elimu. Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mwenge, kinachotoa walimu wa masomo ya sayansi ni kielelezo cha hali ya juu cha mikakati yake katika sekta ya elimu.

Rais Kikwete amewataka watanzania kuendelea kumuenzi Marehemu Askofu Msarikie kwa kuwatumikia watu wao kwa uaminifu, uadilifu, wema, upole na amani. Watanzania wajenge utamaduni wa kuheshimiana na kuthaminiana pamoja na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuvunja amani na utulivu miongoni mwa Jamii.

Naye Askofu Isaac Amani wa Jimbo la Moshi, amewashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema waliofika kumsindikiza Marehemu Askofu Msarikie katika usingizi wa amani aliyefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Saratani. Licha ya maumivu na mateso aliyokabiliana nayo, alikuwa na amani na utulivu wa ndani. Askofu Amani anasema, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi, kuna saratani nyingi zinazowanyima watu amani na utulivu wa ndani. Haya ni mambo kama vile: udini, ukabila, ubaguzi, uchu na uroho wa mali na madaraka; ubaguzi na chuki.

Askofu Amani anawaalika wote kuwa ni wajenzi wa msingi wa haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa; daima wakisimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wawe ni chachu ya maendeleo endelevu kama alivyojitahidi kutekeleza katika maisha yake, Marehemu Askofu Amedeus Msarikie.







All the contents on this site are copyrighted ©.