FAO inamshukuru Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa kusimama kidete kupambana na baa
la njaa na umaskini duniani
Bwana Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja
wa Mataifa, FAO katika mahojiano na Radio Vatican anasema kwamba, amepokea kwa mshangao
mkubwa taarifa za kung'atuka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kutoka
madarakani kutokana na uzee.
Anamshukuru na kumpongeza kwa uamuzi unaoonesha
hekima na busara inayoleta changamoto kubwa kwa kutambua udhaifu wa mwili na hatimaye,
kung'atuka ili kiongozi mwingine aweze kuendeleza Jahazi la Mtakatifu Petro, yaani
kuliongoza Kanisa.
FAO inasema kwamba, Kanisa limekuwa mdau mkubwa katika mapambano
dhidi ya baa la njaa na umaskini duniani. Kwa kufuata mfano na Mafundisho Jamii ya
Kanisa, FAO imeweza kujiwekea sera na mikakati ya kutokomeza baa la njaa nchini Brazil
na Serikali ikafanikiwa. Kwa sasa Jumuiya ya Kimataifa inaelekeza nguvu zake Barani
Afrika. Ni matumaini ya FAO kwamba, Papa atakayechaguliwa ataendeleza sera na mikakati
ya kupambana na baa la njaa pamoja na umaskini duniani.