Vijana wa Taizè wanamkumbuka Baba Mtakatifu Benedikto XVI
Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè inachukua fursa hii kumshukuru Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita, kwa kuweza kuwapokea na kushiriki na umati mkubwa wa vijana waliokuwa
wanashiriki kwenye mkutano wa Sala wa vijana wa Taizè Ulaya, uliofanyika mwishoni
mwa mwaka 2012, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Kwa
vijana wa Taizè hili lilikuwa ni tukio la neema lililowaonjesha vijana mchakato wa
kujenga na kujiimaarisha katika umoja na Kristo, ili wote wawe wamoja.
Vijana
walipata bahati ya kulitafakari Fumbo la Msalaba linalowachangamotisha waamini kujenga
uhusiano wa dhati na Mwenyezi Mungu. Katika kipindi chote cha uongozi wake anasema
Fra Alois, Mkuu wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè, kwamba, amewaimarisha waamini katika
imani, matumaini na mapendo, kwa njia ya nyaraka zake za kichungaji, katekesi, changamoto
ya kusonga mbele kwa imani na matumaini ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali
mbali zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo.
Kwa upande wake, Mheshimiwa
Padre Adolfo Nicolas, Mkuu wa Shirika la Wayesuit, kwa niaba ya Wayesuit wenzake,
wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa hekima, busara
na unyenyekevu pamoja na upendo mkubwa aliouonesha kwa Kristo na Kanisa lake. Wanakumbuka
changamoto aliyowapatia Wayesuit walipokuwa wanaadhimisha Mkutano wao mkuu wa thelathini
na tano, alipowaambia kwamba, wanapaswa kuthubutu kwenda mahali ambapo wengine wanshindwa
kwenda: iwe ni kiroho au kijiografia.
Wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwaamini
wanapoendelea kutekeleza ile nadhiri ya nne ya Utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro,
katika utekelezaji wa dhamana na utume wake ndani ya Kanisa. Wanaendelea kumkumbuka
kwa sala na kujiamisha tena kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika utekelezaji wa utume
wake. Ni matumaini yao kwamba, Kristo Mfufuka ataendelea kuwa mwaminifu kwa ahadi
yake ya kuwa pamoja na Kanisa hadi utimilifu wa dahari.