2013-02-14 10:59:09

Ratiba ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuelekea kwenye uchaguzi wa Papa Mpya


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika katekesi yake, Jumatano tarehe 13 Februari 2013 amebainisha mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutamka wazi wazi kwamba, ameamua kung'atuka kutoka madarakani kwa utashi na uhuru kamili kwa ajili ya mafao ya Kanisa.

Anatambua kwamba, Kanisa ni mali ya Kristo, ataliongoza na kulisimamia kwa kuliwezesha kupata tena mchungaji mkuu. Huu ni uamuzi ambao unafumbata tafakari ya kina na imani thabiti, kwamba, Kristo anaendelea kuliongoza Kanisa lake kwa njia ya neema na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Ni mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya Kanisa na kwa Papa anayekuja.

Ni ufafanuzi wa Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican, wakati huu dunia inapoendelea kujiuliza na kutafakari uamuzi wa hekima na busara uliochukuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa kuamua kung'atuka kutoka madarakani. Anatambua kwamba, wakati wote huu, ameendelea kusindikizwa kwa sala za Kanisa na waamini kutoka pande mbali mbali za dunia. Anakazia toba na wongofu wa ndani kuwa ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha ya Mkristo.

Toba anasema Baba Mtakatifu si hali ya mtu kujitafuta mwenyewe, bali ni ushuhuda unaojionesha katika ukweli, imani na mapendo thabiti katika uhalisia wa maisha ya mwamini; mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee kabisa kwa kuyamwilisha. Baba Mtakatifu anayasema haya yote kwa kuwa wakati wote wa uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amejitahidi kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumamosi, jioni anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Seneti Mario Monti, aliyekuwa Waziri mkuu wa Italia. Rais Giorgio Napolitano wa Italia anatarajiwa kukutana na hatimaye kuagana na Baba Mtakatifu tarehe 23 Februari 2013 baada ya Baba Mtakatifu kutoka katika Mafungo yake ya kiroho na Rais Napolitano kurejea kutoka Marekani.

Baba Mtakatifu atakuwa pia na mazungumzo ya faragha na baadhi ya Makardinali Jumatatu, tarehe 25 Februari 2013. Kwa wakati huu, hija za kitume zilizokuwa zimepangwa kwa Maaskofu mbali mbali zimefutwa. Tarehe 27 Februari 2013, Baba Mtakatifu atahitimisha Katekesi zake kwa siku ya Jumatano, tukio ambalo linatarajiwa kuhudhuriwa na umati mkubwa wa waamini kutoka sehemu mbali mbali kama kielelezo cha shukrani na ukarimu kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Tarehe 28 Februari 2013, Makardinali watapata fursa ya kuweza kuagana rasmi na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. Hii itakuwa ni nafasi kwa Kardinali mmoja mmoja kuzungumza na Papa kwa faragha, ikiwa kama anataka. Saa 11:00 jioni kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, atapanda Elikopta kuelekea Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo. Saa 2:00 Usiku. Kiti cha Khalifa wa Mtakatifu Petro, kitakuwa wazi na hapo mchakato wa kuanza kumpata Papa mwingine utaanza kushika kasi.

Katika kipindi hiki chote, Kardinali Caerlengo Tarcisio Bertone atasimamia na kuratibu shughuli za Vatican. Wakati wote huu, Makardinali wataendelea kufanya vikao mbali mbali kama njia ya kufahamiana, kubadilishana mawazo, kupembua na kubainisha vipaumbele na changamoto zinazolikabili Kanisa kwa sasa na kwa siku za usoni sanjari na mwelekeo wa mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya. Tarehe rasmi ya uchaguzi wa Papa itapangwa na Makardinali wenyewe, ambayo inapaswa kuwa ni kati ya tarehe 15 hadi tarehe 19 Machi 2013.

Baada ya kuchaguliwa kwa Papa Mpya, Makardinali wataendelea na utaratibu uliowekwa na kwamba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, hatahusika kwa jambo lolote kwa wakati huu, kwani kufanya hivyo ni sawa na kuingilia mchakato wa uchaguzi wa Papa. Anaweza kuandika ujumbe wa kitaalimungu kwa ajili ya watu wa Mungu, akipenda. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, itaendelea kukujuvya habari mbali mbali, kadiri zinavyotolewa na Vatican. Unaweza pia kuwashirikisha wenzako kuhusu mtandao huu ili kuweza kujipatia ufahamu mkubwa zaidi kuhusu maisha na utume wa Kanisa.







All the contents on this site are copyrighted ©.