Marehemu Askofu Amedeus Msarikie alisoma alama za nyakati katika kuleta maboresho
katika sekta ya elimu Tanzania, leo Mwenge kinafunika!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika waraka wake "Dhamana ya Afrika" anabainisha
kwamba, shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki ni raslimali yenye thamani
kubwa katika kujifunza na kujenga mshikamano, umoja na utulivu katika Jamii, kwani
wanafunzi wanafundishwa tunu hizi tangu wakiwa wadogo, wakirithishwa pia tunu bora
za maisha ya Kiafrika sanjari na tunu za Kiinjili.
Ni mahali
ambapo Jamii inajifunza na kujenga utamaduni wa majadiliano ya kidini na kiekumene,
sanjari na kunoa akili na mioyo ya vijana wa kizazi kipya katika mwanga wa Injili
pamoja na kuwa tayari kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika
maisha ya watu Barani Afrika, ili Bara la Afrika liwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.
Maneno haya yanasikika kwa mara nyingine tena, wakati huu Kanisa Katoliki
Tanzania linapompumzisha katika usingizi wa amani, Marehemu Askofu mstaafu Amedeus
Msarikie wa Jimbo Katoliki Moshi, aliyefariki dunia hivi karibuni wakati akipata matibabu
Jijini Nairobi. Kabla ya mwili wake kurudishwa Jimboni Moshi, siku ya tarehe 13 Februari
2013 kwa ajili ya maziko, Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Kenya, aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Marehemu Askofu
mstaafu Msarikie.
Mwili wake ulipofikishwa mjini Moshi, ulipelekwa kwenye nyumba
ya Mapadre wazee Longuo, mahali ambapo, Marehemu Askofu Msarikie aliishi tangu alipong'atuka
kutoka madarakani. Ilikuwa ni fursa ya kuweza kuagana na Mapadre wazee na wagonjwa
ambao kutokana na hali yao hawataweza kuhudhuria Ibada ya Misa na Mazishi ya Askofu
mstaafu Msarikie yanayofanyika kwenye Kanisa kuu la Kristo Mfalme.
Askofu mkuu
Yuda Thadeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu
na kuwakumbusha waamini waliohudhuria katika Ibada hii kwamba, Fumbo la Kifo linamshirikisha
mwamini uhai wa Kristo mwenyewe. Marehemu Askofu Msarikie atakumbukwa kutokana na
matumizi bora ya vipaji alivyokirimiwa na Mwenyezi Mungu, yaani: imani, matumaini,
ukarimu na majitoleo kwa watanzania wengi. Anawaalika waamini na wote wenye mapenzi
mema kuendelea kumsindikiza kwa njia ya imani.
Katika mahojiano maalum na Radio
Vatican, Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro anasema kwamba, kwa taaluma
Marehemu Askofu Msarikie alikuwa ni mwalimu aliyebobea, mwenye uwezo, uzoefu na mang'amuzi
mapana. Alitumia vipaji hivi kukabiliana na changamoto ya kushuka kwa kiwango na ubora
wa elimu Tanzania.
Akapania kuanzisha Chuo cha Ualimu, kitakachowaandaa walimu
watakaowafundisha vyema watoto wa watanzania kwa juhudi, maarifa na weledi. Huo ukawa
ni mwanzo wa Chuo cha Ualimu cha Mtakatifu Yosefu, ambacho kimepanuka na sasa ni Chuo
Kikuu Kishiriki cha Elimu Mwenge, kinachopania kuwa kweli ni mwanga wa dunia "Lux
Mundi". Askofu Mkude anasema, mwanzoni baadhi ya Maaskofu walionesha wasi wasi kutokana
na ugumu na changamoto za kuwa na Chuo cha Ualimu.
Askofu Msarikie hakukata
tamaa, bali alisonga mbele, akakabiliana na changamoto hizi kwa imani na matumaini,
leo matunda yake yanaonekana, amefariki dunia, lakini watakaochota elimu na maarifa
kutoka Chuo Kikuu cha Mwenge, bila shaka watakuwa ni mwanga wa mataifa katika Jamii.
Hii ndiyo changamoto ambayo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limejifunza
na leo hii Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augostino cha Tanzania SAUT kimekuwa ni kinara
kwa vyuo vikuu nchini Tanzania. Marehemu Askofu Msarikie alisoma alama za nyakati
katika maboresho ya elimu Tanzania, kwa hakika ataendelea kukumbukwa kutokana na mchango
wake kwa maisha ya kiroho na kiutu miongoni mwa watanzania.