Maadhimisho ya Mwaka wa Imani nchini Uingereza: Katekesi ya kina na ushuhuda makini
wa tunu msingi za Kiinjili
Baraza la Maaskofu katoliki Uingereza, hivi karibuni liliwakusanya wadau wa Uinjilishaji
kutoka Majimbo mbali mbali nchini humo, ili kuweza kufahamiana, kusali na kulitafakari
Neno la Mungu pamoja; kupeana ari na moyo wa kuweza kusonga mbele kwa imani na matumaini
katika dhamana ya Uinjilishaji mpya, ajenda inayovaliwa njuga na Mama Kanisa, katika
maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Kongamano
la kwanza liliwahusisha waamini walei kutoka katika vyama mbali mbali vya kitume na
kongamano la pili liliwajumuisha Makleri kutoka Uingereza. Ilikuwa ni fursa makini
ya kuweza kusikiliza shuhuda kutoka kwa viongozi wa Kanisa na waamini walei walioshiriki
katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji Mpya, iliyofanyika hivi
karibuni mjini Vatican. Makongamano yote haya mawili yalikuwa na uwakilishi mkubwa,
uliopewa dhamana ya kufikisha yale yaliyojadiliwa, kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka
wa Imani.
Wajumbe katika makongamano yote mawili wanasema kwamba, changamoto
kubwa iliyoko mbele yao kwa sasa kabla ya kujimwaga uwanjani kumtangaza Kristo, wanapaswa
kwanza kabisa kujiinjilisha wao wenyewe kwa kujichotea utajiri mkubwa unaofumbatwa
katika Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, Mafundisho Jamii ya Kanisa, Biblia na Nyaraka
za Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ambazo kwa hakika zina utajiri mkubwa katika mchakato
wa kuyatakatifuza malimwengu; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu na binadamu
aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Katekisimu ni nyenzo muhimu sana katika
kuifahamu na kuiungama Imani inayopaswa kujionesha katika matendo adili. Katika mahubiri
yake, Askofu Seamus Cunnigham wa Jimbo Katoliki la Hexham na Newcastle, Uingereza
alizungumzia kuhusu umuhimu wa Sakramenti ya Ubatizo kama mlango unaomwezesha mwamini
kushiriki: ukuhani, ufalme na unabii wa Kristo. Kutokana na dhamana hii, kila mwamini
anao wajibu wa kurithisha imani na kutangaza Habari Njema ya Wokovu; kwa maneno machache,
kila mwamini anaalikwa na Mama Kanisa kujitosa kimaso maso katika azma ya Uinjilishaji
wa mtu mzima.
Askofu Cunnigham anaonya kwamba, kabla mwamini hajaweza kujimwaga
barabara kwenye Jukwaa la Uinjilishaji, anapaswa kwanza kabisa yeye mwenyewe kujiinjilisha,
kwa kujenga uhusiano wa karibu zaidi na Yesu Kristo, aliyeteswa, akafa na kufufuka
kutoka katika wafu kama yanavyonena Maandiko Matakatifu. Waamini wajibidishe kumfahamu,
kumpenda na kumtumikia, ili waweze kuonja upendo na huruma yake isiyokuwa na kifani.
Kwa kujichotea nguvu kutoka kwa Kristo, waamini nao wataweza kuwashirikisha jirani
zao, ule ushuhuda unaobubujika kutoka katika Imani tendaji.
Mwamini anaweza
kujenga uhusiano wa dhati na Yesu Kristo kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu,
Maisha ya Kisakramenti yanayomwezesha kupata neema na baraka anazohitaji katika hija
ya maisha yake ya kiroho. Nguvu na neema hii inapatikana kwa namna ya pekee kabisa
katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, mahali ambapo, mwamini anajifunza kujitoa
na kujimega kwa ajili ya jirani zake, kama Kristo mwenyewe alivyofanya pale Mlimani
Kalvari.
Hakuna haja ya kuogopa kujitosa katika Uinjilishaji, kwani Kristo
amewaahidia wafuasi wake kwamba, atakuwa nao bega kwa bega na kwa njia ya uwepo wa
Roho Mtakatifu. Kuna haja ya kujenga utamaduni wa kudumu katika sala, tafakari na
ukimya ili kumsikiliza Kristo anayeongea kutoka katika undani wa maisha ya mwamini.
Askofu
Cunnigham anasema inasikitisha kuona kwamba, kuna misululu mirefu ya waamini wanaokwenda
kupokea Ekaristi Takatifu, lakini ni waamini wachache sana wanaopokea Sakramenti ya
Upatanisho, inayomwonjesha mwamini upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani.
Kutoshiriki katika sakramenti hii ni dalili za mwamini kufilisika katika maisha ya
kiroho na matokeo yake, atapotelea kwenye ombwe kwani mwamini kama huyo atakuwa na
dhamiri mfu isiyoweza kupembua mema ya kufuata na mabaya ya kuachana nayo, kama njia
ya kujishikamanisha na Kristo.
Wajumbe wa Makongamano haya wanasema, ulikuwa
ni wakati uliokubalika kwa kusali kwa dhati, kutafakari kwa kina, kuabudu Ekaristi
takatifu katika hali ya Ibada na uchaji mkuu. Waamini walipata pia fursa ya kushirikishana
mang’amuzi ya imani, vikwazo na vipaumbele vinavyotolewa na Mama Kanisa wakati huu
wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, ili kila mwamini aweze walau kufaidika na maadhimisho
haya.
Tukio hili limewakumbusha wengi, changamoto iliyotolewa na Mwenyeheri
Yohane Paulo wa Pili alipowataka waamini kujifunga kibwebwe katika azma ya Uinjilishaji
Mpya katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.