2013-02-14 08:17:38

Imani ya Jumuiya za Kikristo Barani Afrika


Imani ni sehemu ya vinasaba vya watu wa Afrika inayojionesha kwa namna ya pekee katika uhalisia wa maisha ya kila siku, kiasi kwamba, wakati mwingine kweli za Kiinjili zinajikuta ziko mashakani kutokana na ukweli kwamba, kuna baadhi ya mila na tamaduni za kiafrika zinazosigana na Injili. Hapa kuna kuja ya kuendeleza mchakato wa utamadunisho, ili Injili iweze kuingia katika tamaduni na kusafisha pale ambapo bado kuna misigano na Injili.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Angola, tarehe 21 Machi 2011 wakati wa mahubiri yake kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo aligusia wasi wasi na changamoto zinazoendelea kutolewa na tamaduni pamoja na mila zinazowafanya waamini wengi licha ya kuukumbatia Ukristo, lakini wanaelemewa na woga wa uwepo wa mashetani, kiasi kwamba, kuna sehemu ambazo baadhi ya watu wanawatoa watoto kafara ili kutuliza mizuka.

Ni imani za kishirikina zinazopelekea hata mauaji ya vikongwe na walemavu wa ngozi katika baadhi ya nchi za Kiafrika. Katika wasi wasi na mashaka ya maisha, baadhi ya Jumuiya za Waamini Barani Afrika zimejikuta zikikabiliana na maamuzi machungu au kukumbatia mila na desturi zilizopitwa na wakati au kuenzi kweli za Kiinjili. Baadhi ya Jamii hazijishughulishi sana katika kudhibiti hali kama hii, kwani kwa upande wao ni njia ya kuishi katika amani, kuvumiliana na usawa wa Kijamii.

Moises Malumbu katika tahariri yake kwenye mtandao wa Radio Vatican anabainisha kwamba, kuchanganya mila na desturi hizi pamoja na imani na kweli za Kiinjili ni jambo la hatari, kwani wakati mwingine utu na zawadi ya maisha viko hatarini. Ni jambo lisiokubaliwa kwa watoto wachanga, walemavu wa ngozi na wazee kutolewa sadaka kutokana na imani za kishirikina ambazo wakati mwingine zinafumbata ndani mwake uchu wa mali na uroho wa madaraka. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika mahubiri yake Luanda alisema, kuna baadhi ya watu wanasema kila mtu aachwe jinsi alivyo ili aendelee kuamini katika imani yake, lakini si hivyo!

Kama Wakristo, kuna mang’amuzi ya hali ya juu kwamba, kwa njia ya Kristo, maisha ya mwanadamu yanafikia utimilifu wake na kwamba, ni haki kwa Kanisa kumtangaza Kristo kama njia ambayo kwayo mwanadamu anaweza kutambua ukweli wa maisha yake. Ni mwaliko kama huu ambao Baba Mtakatifu aliutoa Barani Afrika kuondokana na mila na desturi ambazo zinakumbatia utamaduni wa kifo kwa mauaji ya watoto wachanga, walemavu wa ngozi na vikongwe kwa imani za kishirikina.

Baraza la Maaskofu Katoliki Angola katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, lina waalika waamini kujikita katika amani inayobubujika kutoka kwa Yesu Kristo, kwa kuachana na mila na desturi zinazokwenda kinyume na kweli za Kiinjili. Waamini wayasimike maisha yao katika fadhila ya imani na mapendo, daima wakijitahidi kuziishi ahadi zao za Ubatizo; Nadhiri na Utume na maisha yao kama Watawa na Mapadre. Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayepaswa kuabudiwa, kumbe kupiga ramli pamoja na kukumbatia imani za kishirikina ni kwenda kinyume kabisa cha Amri ya kwanza ya Mungu. Waamini wajitahidi kufahamu kweli za Kiinjili na Imani yao, ili kuondokana na maisha ya ndumilakuwili: Imani ya Kikristo na wakati huo huo wakiwa na Hirizi shingoni…!

Imetayarishwa na Moises Malumbu, Idhaa ya Kireno ya Radio Vatican na kutafsiriwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.