Familia ya Mungu yaungana na Benedikto XVI kuanza kipindi cha toba na wongofu wa ndani!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatano ya Majivu, jioni, tarehe 13 Februari
2013, ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, kama
mwanzo wa kipindi cha Kwaresima. Waamini walikusanyika kuzunguka Kaburi la Mtakatifu
Petro ili kuomba maombezi yake kwa ajili ya hija ambayo Kanisa linafanya kwa sasa,
kwa kuuisha imani kwa Kristo mchungaji mkuu.
Kwake, imekuwa ni fursa ya pekee
kwa ajili ya kuwashukuru waamini wa Jimbo kuu la Roma anapokaribia kuhitimisha utume
wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, anawaomba kuendelea kumkumbuka katika sala zao.
Mama
Kanisa katika kipindi hiki cha Kwaresima anawaalika waamini kwa namna ya pekee, kutubu
na kuongoka; kwa kufunga na kusali, kwa kujiachia huru kabisa ili kutoa nafasi ya
uwepo wa Mungu katika hija ya maisha yao, daima wakijitahidi kuikimbilia huruma yake,
kwani Mungu ni mwingi wa huruma na wala si mwepesi wa hasira. Kumrudia Mungu ni jambo
linalowezekana kwani hiki ni kitendo cha neema, ikiwa kama mwamini mwenyewe anakubali
kushirikiana na neema ya Mungu.
Ni mwaliko wa kusimama kidete kupambana kufa
na kupona na makwazo pamoja navitendo vyote vinavyomnyima mwanadamu haki zake msingi.
Mabadiliko haya yanapaswa kufanyika katika undani wa moyo wa mwamini mwenyewe, jambo
ambalo si rahisi linahitaji ujasiri mkuu, kwa kuchunguza dhamiri na nia, ili kumwachia
Mungu nafasi ya kuweza kuleta mabadiliko pamoja na kumkirimia mwamini wongofu wa ndani,
jambo ambalo linahusisha Jumuiya nzima ya waamini; alama makini ya imani na kama kielelezo
cha maisha ya Kikristo.
Kristo amekuja duniani ili kuwaunganisha watu kwa
njia ya imani, mwaliko kwa kila mwamini kutekeleza dhamana hii, hasa wakati huu wa
kipindi cha Kwaresima. Mchakato wa toba ya kweli, unafanywa na Jumuiya ya Waamini
ndani ya Kanisa.
Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, anaendelea kukazia umuhimu
wa ushuhuda wa imani katika maisha ya waamini, kama njia ya kuonesha ile sura ya Kristo,
ambayo wakati mwingine inachafuliwa na waamini wenyewe; kwa kukosa umoja na mshikamano;
utengano na misigano katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kwaresima ni mwaliko
wa kudumisha umoja wa Kikanisa, kwa kuondokana na ubinafsi, chuki na uhasama, kama
kielelezo cha unyenyekevu kwa wale ambao wako mbali na imani au wamekengeuka.
Kwaresima
ndio wakati uliokubalika, unapaswa kutumiwa kikamilifu, kama alivyofanya Kristo mwenyewe
kwa kujinyenyekesha, kiasi cha kuteswa, kufa na kufufuka kutoka katika wafu, ili kuweza
kumpatanisha mwanadamu na Muumba wake kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Katika mateso
na mahangaiko ya mwanadamu, Mwenyezi Mungu anasema Baba Mtakatifu anaonesha ile hali
ya kuhesabiwa haki.
Kwaresima kiwe ni kipindi cha kumrudia Mungu kwa moyo
wote, kwa kufuata ile Njia ya Msalaba kwa kujitoa bila ya kujibakiza. Ni mwaliko wa
kila mwamini kujitambua kwamba ni zawadi safi mbele ya Mwenyezi Mungu, mwaliko wa
kujitoa katika ubinafsi ili kumpatia Mungu nafasi ya kuishi na kutenda. Kwaresima
kiwe ni kipindi cha kusikiliza kwa makini Neno la Mungu linaloangaza mapito ya miguu
ya waamini.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anabainisha kwamba, Mama
Kanisa anawahamasisha watoto wake wakati wa Mfungo wa Kwaresima: kujinyima, kusali
na kufunga kama sehemu ya mchakato wa mwamini kumrudia Muumba wake. Yote haya yafanyike
katika hali ya unyenyekevu bila ya majivuno wala mtu kupenda kujikweza, kama ambavyo
Yesu mwenyewe anavyokemea.
Ushuhuda wa matendo ya huruma utapata thawabu yake
mbele ya Mwenyezi Mungu; mwaliko kwa sasa ni kuendelea kuambatana naye katika imani,
ili baada ya maisha ya hapa duniani; katika mwanga wa amani waweze kuonana naye uso
kwa uso.
Katika kipindi cha Kwaresima anasema Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita, changamoto kubwa iliyoko mbele ya waamini ni kutubu na kumwongokea Mungu;
kwa kupokea neema yake, waamini wanaweza kuwa wapya na hatimaye, kushiriki katika
maisha angavu ya Kristo. Majivu yawakumbushe waamini changamoto ya kutubu na kuongoka!