Maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima mjini Vatican
Kwaresima ya Mwaka 2013 inaongozwa na kauli mbiu “Nasi tumelifahamu pendo alilonalo
Mungu, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu na Mungu hukaa ndani yake” Kwa
maneno machache Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika waamini kumwilisha
Imani yao katika Mapendo. Mama Kanisa anakianza
Kipindi cha Kwaresima, kwa Jumatano ya Majivu, ambamo waamini wanaalikwa kwa namna
ya pekee kufunga kama sehemu ya kufanya toba ili kujiandaa kikamilifu katika hija
ya ukombozi inayowapatia fursa ya kulitafakari Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa
Kristo. Ni kipindi cha Siku arobaini kinachowakumbusha waamini: ile miaka 40 ya
shida na taabu; pale Waisraeli walipokiona cha mtema kuni kutokana na ukaidi wao kabla
ya kuruhusiwa kuingia kwenye nchi ya ahadi iliyojaa maziwa na asali. Musa alitumia
siku 40 kufunga kabla hajapewa jukumu la kuandika Torati ambazo ni Amri za Mungu,
dira, mwongozo na utambulisho wa Waisraeli kama Taifa teule la Mungu. Itakumbukwa
kwamba, Yesu kabla ya kuanza maisha na utume wake hadharani alifunga kwa muda wa siku
40, akapambana na Ibilisi, na kutoka Jangwani akiwa mshindi. Wafuasi wa Yesu walijifungia
ndani kwa siku 40 baada ya ufufuko wa Kristo, wakiogopa kipigo na mkong’oto kutoka
kwa Wayahudi, hadi siku ile waliposhukiwa na Roho Mtakatifu, wakatoka kifua mbele
kutangaza kwa ari na nguvu mpya kwamba: Kristo aliteswa, akafa na kufufuka, changamoto
endelevu hata katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Ni kipindi cha muafaka kabisa
kwa ajili ya kuwaandaa Wakatekumeni kuingia katika Mlango wa Imani, mwaliko kwa waamini
kujikumbusha tena ahadi zao za Ubatizo; nafasi na dhamana yao katika maisha na utume
wa Kanisa kwa kutangaza Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao ya kila
siku. Kwaresima ni Kipindi cha kufunga, ili kumwezesha mwamini kujenga na kuimarisha
uhusiano wake na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala, Tafakari ya kina ya Neno la Mungu;
Maisha ya Kisakramenti, lakini zaidi kwa kupokea Sakramenti ya Upatanisho inayomwonjesha
mwamini huruma na upendo wa Mungu. Inamkumbusha kwamba, ni mdhambi anahitaji kutubu
na kumwongokea Mungu kama sehemu ya hija ya maisha yake hapa duniani. Sakramenti ya
Ekaristi Takatifu inawachangamotisha waamini kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili
ya Mungu na jirani zao kwa njia ya matendo ya huruma. Mwaka wa Imani, uwe ni kielelezo
cha Imani tendaji; kwani Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika ujumbe wake
wa Kwaresima kwa Mwaka 2013 anabainisha kwamba, imani na upendo ni chanda na pete,
kamwe haviwezi kutenganishwa. Kufunga kuna faida kubwa hata katika maisha adili kwani
kunamsaidia mwamini kuratibu vilema vyake, kujikubali na kuanza kujisahihisha ili
kuweza kuwa ni mtu mwema zaidi kwa kuondokana pia na dhambi za mazoea. Mfungo uwawezeshe
waamini kujenga dhamiri safi, daima wakijitahidi kuchagua jema la kufuata na baya
la kuachana nalo! Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita pamoja na wasaidizi
wake wandamizi watakuwa na Mafungo ya Kiroho kama sehemu ya Maandalizi ya Maadhimisho
ya Siku kuu ya Pasaka. Mafungo haya yanaongozwa na Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais
wa Baraza la Kipapa la Utamaduni. Wazo kuu litakaloongoza mafungo haya ya kiroho “Uso
wa Mungu, uso wa mwanadamu katika Zaburi” Kauli mbiu hii kwa lugha ya Kilatini inasomeka
“Ars Orandi, Ars Credenti” Atapembua kwa kina na mapana maana ya maneno: kupumua,
kufikiri, kupambana na kupenda mintarafu Sala ya Mzaburi. Ni tafakari inayolenga kuwashirikisha
walengwa lile Fumbo na Mwanga wa Mungu unaoangazia uso wa mwanadamu. Baba Mtakatifu
amemkabidhi Patriaki Bechara Boutros Rai kuandaa Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka
Magofu ya Coloseo, kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya hija ya kichungaji, iliyofanywa
na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita nchini Lebanoni, ili kuwasilisha Matunda
ya Sinodi ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki Mashariki ya Kati. Tafakari hii itakuwa na
vituo kumi na vinne kama yalivyo Mapokeo ya Kanisa Katoliki. Idhaa ya Kiswahili ya
Radio Vatican, itaendelea kukushirikisha yale yatakayojiri katika Kipindi cha Kwaresima,
kutoka pande mbali mbali za dunia.