Kanisa ni la Kristo na kamwe hataliacha pweke, bali atalipatia Kiongozi pamoja na
kuendelea kulihudumia!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kabla ya katekesi yake, Jumatano tarehe 13
Februari 2013 kwa waamini na mahujaji waliokuwa wamemiminika kwa wingi mjini Vatican
kwa ajili ya kusikiliza Katekesi yake, aligusia juu ya uamuzi alioufanya wa kung'atuka
kutoka madarakani, dhamana aliyokuwa amekabidhiwa kunako tarehe 19 Aprili 2005.
Baba Mtakatifu
anasema kwamba, amefanya uamuzi huu kwa utashi na uhuru kamili kwa ajili ya mafao
ya Kanisa, baada ya kusali kwa muda mrefu pamoja na kuchunguza dhamiri yake mbele
ya Mwenyezi Mungu, huku akitambua uzito wa maamuzi yake. Anatambua kwamba, kutokana
na uzee hawezi tena kutekeleza wajibu wake kikamilifu kama Khalifa wa Mtakatifu Petro;
nguvu ambazo kimsingi zinahitajika. Anasema anauhakika kwamba, Kanisa ni la Kristo
na kamwe hataweza kuliacha pweke bila ya kulipatia Kiongozi pamoja na kulihudumia.
Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amechukua fursa hii kuwashukuru waamini na watu
wote wenye mapenzi mema kwa upendo na sala ambazo wamemsindikiza nazo katika kipindi
chote cha uongozi wake. Anawaomba kuendelea kusali kwa ajili ya Papa mpya na Kanisa
ana uhakika kwamba, Bwana ataliongoza Kanisa lake.