Kanisa limempoteza kiongozi makini katika maisha, kazi na wito wake!
AskofuTarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anatarajiwa
kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Askofu mstaafu Amedeus Msarikie
wa Jimbo Katoliki Moshi, aliyefariki dunia hivi karibuni.
Mahubiri kadiri
ya taarifa kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania yatatolewa na Askofu mkuu Josephat
Lebulu wa Jimbo Kuu la Arusha na Askofu Isaac Amani wa jimbo Katoliki Moshi, ataongoza
Ibada ya Maziko ya Askofu Amedeus Msarikie. Habari zaidi zinabainisha kwamba, Kardinali
John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, ameongoza Ibada ya Misa takatifu
kwa ajili ya kumwombea Marehemu Askofu Msarikie kabla ya kusafirishwa hadi Jimboni
Moshi.
Rais mstaafu Benjamini William Mkapa ni kati ya viongozi wakuu wa Serikali
wanaohudhuria mazishi ya Askofu Msarikie kwa kutoa heshima zao na baadaye kushiriki
katika Ibada ya Masifu ya Jioni. Kwa upande wa Kanisa, Kardinali Polycarp Pengo na
Balozi wa Vatican nchini Tanzania wanatarajiwa kuhudhuria kadiri ya taarifa kutoka
Jimbo Katoliki Moshi.
Akizungumza na Radio Vatican, Askofu Telesphor Mkude
wa Jimbo Katoliki Morogoro anasema, Kanisa la Tanzania limempoteza kiongozi makini
katika maisha, kazi na wito wake; mtu aliyependa kusimamia dhana ya ukweli na uwazi;
pamoja na utekelezaji wake. Alikuwa ni mtu mwenye kutoa na kupokea ushauri kutoka
kwa wengine.
Askofu Mkude anasema kwamba, alianza kumfahamu wakati ambapo Baba
Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alipotembelea Tanzania, hapa alionesha uwezo mkubwa
katika kupanga, kusimamia, kuratibu na kutekeleza yale yaliyokuwa yameamriwa. Waamini
na watu wenye mapenzi mema wanapoomboleza kifo cha Askofu Msarikie wanapaswa kutambua
kwamba, ni kiongozi aliyejenga maisha na utume wake kwa katika Mwamba thabiti ambao
ni Yesu Kristo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu.
Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani yaliyotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita, iwe ni fursa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuenzi yale mambo
msingi ambayo Marehemu Askofu Msarikie aliyasimamia na kuyatekeleza kwa ajili ya ustawi
na maendeleo ya Watanzania kiroho na kimwili. Kama Askofu aliwafundisha, akawaongoza
na kuwatakatifuza watu wake, mwaliko na changamoto ya kurithisha zawadi ya Imani kwa
watoto na vijana wa kizazi kipya, ili Bwana atakapokuja aweze kuikuta imani ikiwa
bado ipo!