2013-02-12 09:05:15

Siku ya Wagonjwa 2016 kuadhimishwa Mjini Nazareti


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita mara baada ya Maadhimisho ya Siku ya 21 ya Wagonjwa Duniani iliyofanyika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Altotting sanjari na Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes ameamua kwamba, Siku ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2016 itaadhimishwa mjini Nazareti "kwa kujidhaminisha mikononi mwa Bikira Maria: lolote atakalowaambia, fanyeni" Yoh. 2:5.

Uamuzi huu umetangazwa kwa niaba ya Baba Mtakatifu na Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la wahudumu katika sekta ya afya, mara baada ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya 21 ya wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2013.

Lengo la maadhimisho ya Siku ya 24 ya Wagonjwa Duniani Mwaka 2016 kufanyika mjini Nazareti ni kutaka kukoleza moyo wa Sala na Tafakari ya kina kwa kumuiga Bikira Maria, aliyejiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ili kutekeleza mapenzi yake, akaonja utii wa Mwanaye wa pekee hadi pale alipoyamimina maisha yake Msalabani.

Mada nyingine zilizopendekezwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa Maadhimisho ya Siku ya 22 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2014 ni: Imani na Upendo "Katika hili tumelifahamu pendo: kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu." 1 Yoh. 3:16.

Mada itakayoongoza Maadhimisho ya Siku ya 23 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2015: Hekima na Upendo: "Nalikuwa macho kwa kipofu, nalikuwa miguu kwa aliyechechemea." Ayubu 29: 15.

Askofu mkuu Zygmunt Zimowski anasema maandalizi na hatimaye Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa ni Kielelezo makini cha hija ya imani, matumaini na mapendo, yanaofumbatwa wakati mwingine katika mateso na mahangaiko ya ndani; kama alivyokuwa Msamaria mwema, kila mwamini anachangamnotishwa kutoa huduma kwa jirani yake anayeteseka: kiroho na kimwili; uzee, ulemavu pamoja na upweke ambao unaweza kumkatisha mtu tamaa ya maisha.

Anamshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita ambaye ameonesha uwepo wake wa karibu kama Baba mwema na Mchungaji mkuu wa Kanisa Katoliki kwa wote wanaoteseka: kiroho na kimwili. Tafakari ya Neno la Mungu na Sala imwilishwe katika matendo ya huruma kwa wagonjwa na wahitaji.







All the contents on this site are copyrighted ©.