2013-02-12 09:48:37

Mchakato wa kumtafuta Papa Mpya kuanzia tarehe Mosi, Machi 2013


Padre Federico Lombardi akielezea kuhusu tamko la Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita la kung'atuka kutoka madarakani mintarafu sheria za Kanisa anasema kwamba, ili Kiti cha Khalifa wa Mtakatifu Petro kiweze kuwa wazi, lazima idhihirishe wazi kwamba, kujiuzuru huku kuwe ni huru na wala si lazima kukubaliwe na wote.

Hivi ndivyo alivyofanya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatatu tarehe 11 Februari 2013 wakati wa Mkutano na Dekania ya Makardinali. Baba Mtakatifu atang'atuka rasmi madarakani hapo tarehe 28 Februari 2013, saa 2:00 Usiku. Tangu wakati huo Kiti cha Khalifa wa Mtakatifu Petro kitakuwa wazi kadiri ya Sheria za Kanisa.

Padre Lombardi anasema, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita alipohojiwa na Bwana Peter Seewald, mwandishi wa kitabu alionesha kwamba, kuna uwezekano mkubwa kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kujiuzuru wadhifa wake katika hali ya amani, anapojisikia kwamba, hana tena nguvu ya kuweza kulihudumia Kanisa kwa tija na ufanisi mkubwa kutokana na matatizo ya afya, akili na kiroho. Kwa mazingira kama haya Papa anapaswa na kulazimika kujiuzuru wadhifa wake.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatarajiwa kuhamia Ikulu ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma, ili kukamilisha baadhi ya majukumu yake katika uongozi. Wakati huo huo, ukarabati wa nyumba atakamoishi Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, mjini Vatican utakuwa unakamilika. Mchakato wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro, utaanza rasmi hapo tarehe Mosi Machi 2013. Padre Lombardi anasema kwamba, bado tarehe rasmi haijapangwa, lakini hakutakuwa na haja ya kusubiri siku nane kama zinavyotajwa wakati wa maombolezo ya kifo cha Papa.

Katika kipindi cha majuma mawili katika mwezi Machi, Kanisa litakuwa na Papa Mpya. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa unyenyekevu mkubwa hatahusika kwenye Mkutano wa kumchagua Papa mwingine wala kujihusisha na shughuli za uongozi wa Kanisa kadiri ya sheria za Kanisa. Wakati huu Kanisa litakuwa chini ya Dekano wa Makardinali ambaye kwa sasa ni Kardinali angelo Sodano na Kardinali Tarcisio Bertone.

Padre Federico Lombardi anahitimisha kwamba kusema kwamba, binafsi amepokea tamko la Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita la kung'atuka kutoka madarakani kwa mshangao na hamasa kubwa kutokana na uhuru wake wa ndani pamoja na kujali wajibu na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa ajili ya mafao ya Kanisa. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ameonesha ushuhuda mkubwa wa uhuru wa maisha ya kiroho, busara na hekima katika kuliongoza Kanisa kwenye Karne ya 21 yenye changamoto nyingi.







All the contents on this site are copyrighted ©.