2013-02-11 10:28:10

UNESCO: Mchango wa Papa Yohane Paulo II: kuhusu: Utu, Elimu na Utamaduni


Shirika la Elimu na Sayansi la Umoja wa Mataifa, UNESCO kwa kushirikiana na Mwakilishi wa Vatican kwenye UNESCO na Mfuko wa Yohane Paulo wa Pili, kwa pamoja wameaandaa Kongamano la kimataifa litakalofanyika mjini Paris, Ufaransa, Jumatano tarehe 13 Februari 2013 ili kujadili mchango wa mawazo ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili mintarafu: utu, elimu na utamaduni.

UNESCO inasema, Papa Yohane Paulo wa pili alitoa mchango mkubwa katika masuala ya elimu, sayansi na utamaduni, mambo ambayo yanamwezesha mwanadamu kuweza kufanya rejea katika maisha na utu wake kama binadamu.

Ni kwa njia ya utamaduni binadamu anafikia utimilifu wa utu na uwezo wake wa kufikiri na kutenda. Ndivyo alivyowaambia wajumbe wa UNESCO wakati wa hotuba yake aliyoitoa kunako tarehe 2 Juni 1980. Anasema, binadamu anaishi vyema kwa kufanya kazi sanjari na kutumia vyema akili yake, kwa maneno mengine, hiki ni kielelezo cha mtu anayeishi kadiri ya utamaduni wake. Kutokana na mantiki hii kuna uhusiano wa dhati pale Jamii inaposimama kidete kulinda na kutetea utamaduni wake ni sawa na kutetea utu, heshima, uhuru pamoja na akili zake.

Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili anabainisha kwamba, mwanadamu hakuumbwa ili akaye kama kisiwa bali anapata utimilifu wake kwa kuishi katika Jamii ya watu, wenye lugha na tamaduni zao. Haya ni mawazo yanayokubalika na wanasayansi ya binadamu kama vile Levi Strauss na wenzake. Papa Yohane Paulo wa pili alipenda pia kuunganisha sayansi na utamaduni, kwani yote haya ni mambo yanayomgusa mwanadamu.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kwa njia ya ufahamu, sanaa na matendo mwanadamu anafikia utimilifu wake kadiri ya mawazo ya Mtakatifu Toma wa Akwino, ambaye alikuwa ni kielelezo rejea kwa Mafundisho mengi ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili.

Kati ya wataalam elekezi walioalikwa kwenye Kongamano hili ni pamoja na Bi Irina Bokova, Mkurugenzi mkuu wa UNESCO, Kardinali Stanislaw Rylko, Rais wa Baraza la Kipapa la Walei na Rais wa Mfuko wa Yohane Paulo wa pili pamoja na Askofu mkuu Francesco Follo, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican makao makuu ya UNESCO. Ni fursa makini kwa wadau mbali mbali kuweza kushirikisha mawazo kuhusu: tunu na kweli za kiinjili katika mchakato wa utamadunisho, uchumi na maendeleo endelevu ya binadamu; vijana wa kizazi kipya katika utamaduni mamboleo; umuhimu wa elimu; utu na heshima ya mwanamke pamoja na elimu mintarafu Mafundisho ya Yohane Paulo wa pili.








All the contents on this site are copyrighted ©.