2013-02-11 10:14:52

Mwaka wa Imani ujioneshe kwa namna ya pekee kwa njia ya Imani tendaji!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu katika ziara yake ya kikazi nchini India, Jumapili tarehe 10 Februari 2013 alitembelea Madhabahu ya Bikira Maria, Mama Yetu wa Afya Njema, yaliyoko Vailankanni, India na kusema kwamba, kwa hakika Bikira Maria ni chombo cha upendo wa Mungu, hasa wakati huu Madhabahu haya yanapoadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu yalipojengwa sanjari na Mwaka wa Imani.

Amewapatia salam na baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. Makanisa yote yaliyowekwa chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria ni kielelezo cha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu kama alivyotangazwa na Mtaguso wa Efeso kunako mwaka 431. Yesu mwenyewe aliwaonesha mitume wake Mama yao ambaye wangepaswa kumtunza, changamoto ya kuendeleza dhamana ya Uinjilishaji Mpya sehemu mbali mbali za dunia. Miaka 50 tangu Madhabahu haya yalipoanzishwa, yamekuwa ni kielelezo cha imani na upendo kwa Bikira Maria.

Bikira Maria ni Mama wa Mungu na wa Kanisa, Mfariji wa wote wanaomkimbilia kwa imani na matumaini, hasa kwa wale wanaomtumikia na kumpenda Mwanaye wa Pekee. Huu ni mwaliko wa kumsikiliza Kristo kwa makini pamoja na kuendelea kumjifunza Kristo kutoka katika shule ya Bikira Maria; daima wakijitahidi kutekeleza kile anacho waamuru kutenda; huku wakijitahidi kuchuchumilia wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.

Bikira Maria ni kielelezo cha mtu wa sala anayewaombea watu mahitaji yao ya msingi pamoja na neema. Muujiza wa arusi ya Kana ulipania kuwaimarisha wafuasi wake katika imani, ili kubadili maisha yao mintarafu mpango wa Mungu. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, iwe ni fursa ya kujibidisha kuifahamu vyema imani kwa Kristo na Kanisa lake.

Hii ndiyo ile hija ya imani na matumaini aliyofanya Bikira Maria tangu alipopashwa habari kwamba, atakuwa Mama wa Mungu, alipomtembelea binamu yake Elizabeth na walipolazimika kukimbilia Misri ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu, hadi pale aliposimama chini ya Msalaba na baadaye kupokea Zawadi ya Roho Mtakatifu. Mwaka wa Imani ujioneshe kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji.

Kardinali Fernando Filoni anawaalika waamini nchini India katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, wajibidishe zaidi na zaidi katika azma ya Uinjilishaji Mpya kwa ari na kasi kubwa zaidi. Kardinali Filoni pia alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu katoliki India.







All the contents on this site are copyrighted ©.