2013-02-11 08:05:13

Kampeni ya mshikamano wa upendo "Hakuna haki pasi na usawa"!


Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania kuanzia Jumapili tarehe 10 Februari 2013 litaendesha Kampeni ya 54 ya mshikamano kimataifa, kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Hispania. Kauli mbiu inayoongoza kampeni hii kwa mwaka 2013 inasema kwamba, “hakuna haki pasipo na usawa”. RealAudioMP3
Katika barua ya kichungaji iliyoandikwa na Kardinali Antonio Maria Rouco Varela wa jimbo kuu la Madrid anawakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, kuna uhusiano wa karibu kati ya usawa na haki, jambo linalobainisha umuhimu wa wanawake na wanaume kushirikiana kwa dhati, kwa kutambua usawa unaofumbatwa katika utu na heshima ya binadamu, ambayo kamwe haiwezi kupimwa kwa vigezo vya sera zinazotawala katika ulimwengu wa utandawazi, ambao unataka kufuta hata zile tofauti za kimsingi zilizopo kati ya mwanaume na mwanamke na dhamana ambayo kila jinsia imedhaminishwa na Mwenyezi Mungu. Ni sera ambazo zinawakanganya watu, kiasi cha baadhi ya watu kudhani kwamba, hakuna umuhimu wa tofauti kati ya mwanaume na mwanamke.
Kardinali Varela anasema, kuna haja kwa Jamii kuheshimu na kuthamini tofauti hizi za kimaumbile, zinazoonesha pia utajiri na changamoto kwa wanaume na wanawake kushirikiana kwa dhati ili kukamilishana, kujenga na kuimarisha umoja, kila upande ukitekeleza wajibu na wito wake kadiri ya Mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Jamii itambue kwamba, Mwenyezi Mungu alimuumba mwanamke akiwa na makusudi maalum na wala si kichokoo cha kukidhi tamaa za watu katika Jamii.
Katika mwelekeo wa watu kutaka kukengeuka na kupotosha maadili na utu wema, Kardinali Antonio Maria Rouco Varela, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda na kutetea misingi bora ya maisha ya familia kwa kutambua kwamba, Familia ni kiini cha maisha ya Jamii; ni shule ambamo Jamii inajifunza kuheshimiana na kuthaminiana kutokana na tofauti zilizopo na hivyo kushiriki katika mchakato wa kujenga na kuimarisha haki, usawa na mshikamano wa dhati.
Kampeni ya mshikamano inayoendeshwa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki “Manos Unidas”, kwa baadhi ya nchi imeanza rasmi hapo tarehe 5 Februari 2013. Lengo ni kusaidia juhudi za mapambano dhidi ya umaskini, njaa na maradhi. Kuna watu wanaendelea kuteseka kutokana na kutumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu; vyote hivi ni vitendo vinavyodhalilisha ut una heshima ya binadamu. Haki na Usawa ni tunu muhimu katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili.








All the contents on this site are copyrighted ©.