Jifunzeni kwa imani na matumaini Fumbo la Msalaba wa Kristo: kielelezo cha huruma,
upendo na msamaha wa kweli!
Askofu mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania, katika mahojiano na
Radio Vatican anasema, maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani yanayofikia kilele
chake kila mwaka tarehe 11 Februari ni mwaliko wa kuonesha mshikamano wa upendo na
wagonjwa pamoja na wahudumu wa sekta ya afya, ili waweze kusimama kidete kulinda na
kutetea maisha, utu na heshima ya kila mgonjwa wanayemhudumia.
Katika taabu
na mahangaiko ya afya ya roho na mwili, kuna haja kwa waamini kulikumbuka Fumbo la
Msalaba, kielelezo makini cha: upendo, huruma na msamaha kwa binadamu. Ni mwaliko
kwa waamini kushiriki katika mateso ya Kristo kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato
wa kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo mwenyewe. Wawe tayari kupokea Misalaba
ya maisha yao kwa imani, matumaini na mapendo makuu.
Anamshukuru Mungu kwa
wema na ukarimu wake. Kama Padre na Askofu ameonja pia mateso, magumu na mahangaiko
ya ndani katika maisha na utume wake. Jambo la msingi ni kumkabidhi mateso na mahangaiko
yote haya Kristo ili kupata nguvu na ari mpya zaidi. Waamini wajifunze maana ya mateso
yanayookoa na kuyapokea yote kwa moyo wa uvumilivu na subira; changamoto kubwa zaidi
ni kuungana kabisa na Yesu Kristo kwa kuyamimina yote mbele yake!