2013-02-11 09:18:38

Imani na matumaini ni nguzo muhimu katika kuitikia wito wa Kristo!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili iliyopita alitafakari kuhusu Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya tano ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, kwa kuangalia wito wa mitume wa kwanza wa Kristo, baada ya kuwafundisha watu waliokuwa wamemiminika kumsikiliza anamwambia Petro kushusha nyavu zake tena baada ya kuvua usiku kucha bila mafanikio. Simoni anatii na kushusha nyavu zake na hivyo kufanikiwa kupata wingi wa samaki.

Mwinjili Luka anaonesha imani na matumaini ya Mitume wa kwanza wa Yesu, kwa kuacha yote na kumfuasa, kwa kumtambua kuwa ni Bwana na Mwalimu. Baba Mtakatifu anasema, wito wa Mungu kwa waja wake hauangalii sana ubora wa mtu bali imani yake, kama anavyodhihirisha Simoni kwa kusema, "Bwana kwa neno lako nitazishusha nyavu zangu".

Baba Mtakatifu anasema, Wainjili wanaelezea matukio makuu mawili ambayo yanawahusisha mitume katika shughuli yao ya uvuvi: kabla ya mateso ya Kristo na baada ya ufufuko wake, kielelezo makini cha utume wa Kanisa kwa sasa na baada ya ufufuko wa wafu. Kwa sasa linakusanya wema na wabaya, lakini baada ya ufufuko Kanisa litakuwa ni kwa ajili ya watu wema tu! Ndivyo anabyobainisha Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalim wa Kanisa.

Mtakatifu Petro ni kielelezo cha wafuasi wa Kristo ambao kamwe hawapaswi kukata tamaa kumtangaza Kristo kwa watu wote hadi miisho ya dunia. Liturujia ya Neno la Mungu kwa Jumapili hii ni mwaliko wa kutafakari wito wa kipadre na kitawa, kazi ya Mungu! Binadamu si chanzo cha wito wake mwenyewe, bali anajibu changamoto hii kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kamwe mapungufu ya binadamu yasiwe ni kikwazo pale Mwenyezi Mungu anapomwita mtu. Jambo la msingi ni kuwa na imani na nguvu kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma anayebadili na kufanya mtu kuwa mpya zaidi.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujiaminisha katika Neno la Mungu ili kama watu binafsi na Jumuiya za Kikristo wawe na ujasiri na imani ya kutangaza na kushuhudia Injili hadi miisho ya dunia. Vikwazo na magumu kamwe yasiwakatishe tamaa, bali wasonge mbele kwa imani na matumaini kwa kutekeleza wajibu wao na Kristo atakamilisha yale yanayosalia. Anawataka waamini kujiaminisha kwa Bikira Maria, Malkia wa mitume, aliyefahamu unyonge wake, lakini akatoa jibu la uhakika linaloonesha kujitoa kwake bila ya kujibakiza. Bikira Maria awasaidie waamini kuendelea kujitoa kikamilifu ili kumfuasa Kristo Bwana na Mwalim.







All the contents on this site are copyrighted ©.