Waziri mkuu Pinda: Changamoto zinazowakabili Watanzania kwa sasa
Ifuatayo ni hotuba ya Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda wakati wa kuahirisha mkutano
wa 10 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyoitoa tarehe 8 Februari 2013
mjini Dodoma. Ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa ni kati ya changamoto kubwa
zinazoikabili Tanzania; hali ya chakula na lishe; mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria,
Mchakato wa kuelekea Katiba Mpya; tathmini ya utawala bora Barani Afrika na mapambano
dhidi ya fedha haramu zilizofichwa na watanzania ni kati ya mambo yaliyozungumziwa
na Waziri mkuu Pinda.
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, tumekuwepo hapa
Bungeni, Dodoma kwa takriban siku 11 ambapo leo tunahitimisha shughuli zilizopangwa
katika Mkutano wa Kumi wa Bunge lako Tukufu. Nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi
Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nitumie nafasi hii kutoa pole kwa
Ndugu, Jamaa na Marafiki waliopoteza Wapendwa wao katika ajali mbalimbali zilizotokea
hapa Nchini, ikiwemo ajali ya Jahazi la Sunrise iliyotokea Wangwi katika Bahari ya
Hindi na Ajali ya Lori kule Mbarali ambapo Watu wamepoteza maisha na kupata majeraha.
Aidha, tunawapa pole Majeruhi wote na Abiria waliopoteza mali katika ajali hizo. Kwa
kipekee kabisa napenda kutoa pole kwa Ndugu, Jamaa na Marafiki wa Askofu Thomas Laiser
wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati - Arusha ambaye amefariki jana Mchana na Askofu
Mstaafu Amedeus Msarikie wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Moshi ambaye amefariki Usiku
wa kuamkia leo huko Nairobi alikokuwa anapata matibabu. Wote tunawapa pole sana!
SHUGHULI
ZA BUNGE
Maswali
Mheshimiwa Spika,
katika Mkutano huu jumla ya Maswali 116 ya Msingi na 286 ya nyongeza yalipatiwa majibu.
Vilevile, Maswali 6 yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo
kwa Waziri Mkuu.
b) Miswada Mheshimiwa Spika, katika
Mkutano huu, Miswada ifuatayo ilisomwa kwa mara ya Kwanza:
Muswada wa Sheria ya Vyama vya Ushirika wa Mwaka 2013 [The Cooperative Societies
Bill, 2013]; na
Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali
wa Mwaka 2013 [The Written Laws Miscellaneous Amendments, Bill 2013].
Mheshimiwa Spika, Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2012
[The Written Laws Miscellaneous Ammendments (No. 3) Act, 2012] ulisomwa kwa mara ya
Pili na kupitia ngazi zake zote;
c) Hoja Binafsi za Wabunge Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, pia Waheshimiwa Wabunge walipata
fursa ya kuwasilisha Hoja Binafsi kama ifuatavyo:
Hoja
Binafsi ya Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba, Mbunge wa Iramba Magharibi ya kuitaka
Serikali iwasilishe Bungeni Muswada wa Sheria ya Uanzishwaji wa Mfuko wa Elimu ya
Juu (The Higher Education Fund Act);
Hoja
Binafsi ya Mheshimiwa James Francis Mbatia, Mbunge wa Kuteuliwa kuhusu udhaifu ulioko
katika Sekta ya Elimu Nchini;
Hoja Binafsi
ya Mheshimiwa Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla, Mbunge wa Nzega ya kuitaka Serikali
ianzishe Mpango Maalum wa Kukuza Ajira kwa Vijana na kuanzisha Mfuko wa Mikopo ya
Vyama Wanaowekeza kwenye Kilimo na Viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja na Kilimo;
na
Hoja Binafsi ya Mheshimiwa John Mnyika,
Mbunge wa Ubungo juu ya Kuboresha Upatikanaji wa Maji Safi na ushughulikiaji wa Maji
Taka katika Jiji la Dar es Salaam.
d) Maazimio Mheshimiwa
Spika, vilevile, katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge waliweza kujadili na kupitisha
Maazimio Mawili yafuatayo:
Azimio la Bunge la Kujiunga
na Mkataba wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu Dhidi ya Watu wenye Kinga ya Kimataifa pamoja
na Wakala wa Ki-Diplomasia (Convention on The Prevention and Punishment of Crimes
Against Internationally Protected Persons Including Diplomatic Agents 1973); na
Azimio la Bunge la Kujiunga na Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Vitendo
vya Ugaidi wa Kutumia Nyuklia (International Convention for Suppression of Act
of Neuclear Terrorism, 2009).
Ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa
kukamilisha Mijadala hiyo.
UJENZI WA UMOJA WA KITAIFA
Mheshimiwa
Spika, kwa namna ya pekee Taifa letu limejaliwa na Mwenyezi Mungu kutimiza miaka zaidi
ya 51 sasa ya Uhuru likiwa bado linaendelea kudumisha Umoja wa Kitaifa. Umoja
huu wa Kitaifa umejengwa kwenye nguzo na misingi imara ya Amani, Utulivu na Mshikamano.
Mimi naamini sote tunapaswa kujivunia Umoja huu wa Kitaifa ambao ni Tunu kubwa na
nguzo muhimu ya maendeleo yetu. Msingi mkubwa wa Umoja wa Kitaifa tunaoshuhudia leo
uliwekwa na malezi mazuri ya Waasisi wa Taifa hili wakiongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume. Aidha, Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inasisitiza, pamoja na mambo mengine, kujenga Jamii inayozingatia
misingi ya Uhuru, Haki, Udugu na Amani. Ni jukumu la kila Mwananchi kulinda Umoja
huu ambao hauna mbadala.
Mheshimiwa Spika, Nchi yetu
ina Makabila zaidi ya 120 ambayo kwa Mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi
ya Mwaka 2012 yamefikisha Idadi ya Watu Milioni 44.929. Aidha, hivi sasa tuna Madhehebu
ya Dini yaliyoandikishwa takriban 885 na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali zaidi ya 6,675
na tumejenga Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa ambapo hadi sasa tuna Vyama vya Siasa
19 ambavyo vimepata Usajili wa Kudumu. Licha ya kuwepo kwa Idadi kubwa ya Watu wa
Makabila tofauti yenye desturi mbalimbali na makundi mbalimbali ya Madhehebu ya Dini,
Itikadi za Kisiasa na Watu wenye Rangi mbalimbali, bado tunajivunia kwamba tunaheshimiana
na hatubaguani kwa namna yoyote ile. Hali hii ya amani imeipatia Nchi yetu sifa Kitaifa
na Kimataifa na mfano wa kuigwa.
Kutokana na Demokrasi
pana iliyopo, Wananchi wetu wana Uhuru mkubwa wa kutoa maoni, kuanzisha na kujiunga
na Vyama vya Siasa pamoja na kushiriki katika kuchagua Viongozi wa Chama chochote
wanachokipenda kwa kuzingatia Misingi ya Katiba na Sheria za Nchi. Vilevile, Serikali
imetoa uhuru mkubwa wa kupata na kutoa habari kwa uwazi bila vikwazo vyovyote kwa
kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni mbalimbali na Maadili ya Vyombo vya Habari. Kutokana
na Uhuru huo, Idadi ya Vyombo vya Habari imeongezeka sana ambapo hadi sasa Idadi ya
Vituo 86 vya Redio vilivyopewa Leseni na vinafanyakazi, Vituo vya Televisheni 26 na
Magazeti 768 yaliyoandikishwa na yanayotolewa na Taasisi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo yanayodhihirika wazi, hivi karibuni
kumekuwepo na dalili za kupoteza sifa yetu nzuri ya Umoja wa Kitaifa na Amani ambayo
imedumu kwa miaka mingi. Tumeshuhudia Wananchi mmoja mmoja wakishindwa kuvumiliana,
japo kwa tatizo dogo tu miongoni mwao. Aidha, tumeshuhudia Vyama vya Siasa vikionesha
dalili ya kuhamasisha Wanachama wao kuingia kwenye malumbano ya Siasa baina yao
wenyewe kwa wenyewe au baina ya Chama kimoja cha Siasa na Chama kingine. Baadhi
ya Wanachama wameshikana mashati na kujeruhiana.
Mheshimiwa
Spika, napenda kutumia fursa hii kuwaasa Viongozi wa Vyama vya Siasa kuepuka kutumia
majukwaa ya Siasa kuvuruga Amani yetu na Utulivu uliopo. Waepuke matamko ya vitisho
na kuhamasisha Wanachama wao kuendeleza vitendo vya uvunjifu wa amani na kujenga chuki
na uhasama miongoni mwa Jamii na kwa Serikali halali iliyopo madarakani. Pamoja na
kutofautiana kwa mawazo na Sera za Vyama vya Siasa, ni muhimu tujenge mazingira ya
kuvumiliana kwa hali ya juu katika kujenga Demokrasia ya kweli hapa Nchini. Viongozi
wa Vyama wanatakiwa kueleza Sera zao badala ya kutukanana, kubezana, kushutumiana
na kuzomeana. Tujenge Nchi yetu kwa Amani na Utulivu ndipo tutapata maendeleo endelevu.
Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia pia kuibuka kwa choko choko za Kidini. Baadhi
ya Waumini wa Dini wamekuwa wakikashifu Dini nyingine kwa kejeli na vitendo vingine
visivyostahili. Aidha, baadhi ya Viongozi wa Madhehebu ya Dini wamekuwa wakiwaingiza
Waumini wao katika Migogoro isiyoisha, ikiwa ni pamoja na kufungiana milango na kuzuia
Waumini Wasiabudu siku za Ibada. Napenda kusisitiza kuwa Madhehebu ya Dini yana nafasi
kubwa ya kujenga Umoja wa Kitaifa, Amani na mshikamano. Nawaomba Viongozi wa Madhehebu
ya Dini kutatua kwa amani migogoro iliyopo na kuelimisha Waumini wao kuthamini, kujenga
na kuenzi Amani na Utulivu uliopo Nchini. Serikali imetoa uhuru wa Wananchi wake Kuabudu,
kila mtu kwa Dini anayoitaka. Hivyo, hakuna sababu ya Dini moja kukashifu Dini nyingine.
Aidha, tupinge kwa nguvu zetu zote choko choko za Kidini ambazo zimeanza kujitokeza
katika sehemu mbalimbali Nchini.
Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali baadhi yao yamekuwa yakihusishwa kuwa
mstari wa mbele katika kuwarubuni Wananchi kufanya vurugu zinazolenga kuleta uvunjifu
wa Amani. Napenda kusisitiza kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yana jukumu kubwa
la kuelimisha Wananchi kuhusu umuhimu wa kujenga Umoja wa Kitaifa. Viongozi wa Mashirika
haya waepuke kutumiwa na baadhi ya Viongozi kujenga mbegu mbaya kwa Wananchi kuvuruga
Amani.
Mheshimiwa Spika, nigusie pia Vyombo vya Habari,
ambapo kumekuwa na kutiliana mashaka kwa baadhi ya Vyombo hivyo kuandika habari za
Uchochezi, hivyo kuashiria Uvunjifu wa Amani na Mshikamano wa Kitaifa tuliojijengea.
Vyombo vya Habari vina wajibu mkubwa wa kuelimisha Umma na kuhabarisha kuhusu masuala
mbalimbali ya maendeleo, kama wafanyavyo wenzetu jirani, husan Vyombo vya Habari vya
Nchi ya Rwanda. Aidha, Vyombo hivi vina fursa nzuri ya kutumia uhuru uliopo kudumisha
Amani na Utulivu Nchini.
Tufanye Nini
Mheshimiwa
Spika, kutokana na changamoto zilizopo za baadhi ya Watu waotaka kubomoa Umoja wa
Taifa letu na kuhatarisha Amani na Utulivu Nchini, sisi kama Taifa hatuna budi kufanya
yafuatayo:
Serikali, Wananchi na Wadau wote ikiwemo Vyama
vya Siasa, Madhehebu ya Dini, Vyombo vya Habari, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, n.k.
tunapaswa tukae chini tuzungumze na kutafakari kuhusu hali hii;
Tunapaswa kwa namna zote tuvumiliane na kuheshimiana kwa kuzingatia
Utamaduni wa Kitanzania na Misingi ya Amani na Utulivu tuliojijengea kwa muda mrefu;
na
Wananchi wote tuzingatie na kuheshimu Utawala
Bora wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.
Mheshimiwa
Spika, napenda kutumia fursa hii kuwaomba sana Wananchi na Watanzania wenzangu kuendeleza
umoja na mshikamano wa Kitaifa ili kudumisha Amani na Utulivu uliopo Nchini. Ni
vyema kutambua kuwa Amani na Utulivu uliopo Nchini ni mazingira wezeshi ya kusaidia
kila mmoja wetu kufanya shughuli zake za kijamii na kiuchumi na kujiletea maendeleo.
Bila Amani na Utulivu hakuna maendeleo ya Watu. Kwa upande wa Serikali itahakikisha
kwamba, Umoja tuliojijengea unadumishwa. Taasisi mbalimbali za Serikali, zikiwemo
Vyombo vya Dola ni lazima zihakikishe kwamba, Wananchi wanaishi kwa Amani na Utulivu.
Vilevile, kuhakikisha kuwa, Umoja wa Kitaifa tulioujenga kwa miaka mingi haupotei.
Naziomba Taasisi zote zinazohusika na kusimamia Amani na Usalama kuhakikisha kuwa,
pamoja na Changamoto zilizopo, Umoja wa Kitaifa unadumishwa.
HALI YA CHAKULA
NCHINI
Hali ya Mazao na Mvua
Mheshimiwa Spika, tathmini iliyofanyika hivi karibuni juu ya upatikanaji wa chakula
Nchini na athari za mvua zinazoendelea kunyesha, inaonesha kuwa maeneo mengi hasa,
yale yanayopata mvua za msimu kama vile Mbeya, Ruvuma, Rukwa, Iringa, Tabora, na Mtwara
mazao mengi yapo katika hatua mbalimbali za ukuaji. Inatarajiwa kwamba, endapo mvua
hizi zitaendelea vema, upatikanaji wa chakula katika maeneo hayo utakuwa mzuri.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hali hiyo ya hewa, tathmini ya kina ya hali
ya chakula na lishe iliyofanyika mwezi Januari 2013 inaonesha upungufu wa chakula
katika Wilaya 47 zilizoko katika Mikoa 15 ambazo zitahitaji msaada wa chakula katika
vipindi tofauti. Inakadiriwa kuwa jumla ya Watu 1,615,445 watahitaji jumla ya Tani
32,870 za chakula.
ii) Hatua Zinazochukuliwa na Serikali Mheshimiwa
Spika, kutokana na matarajio hayo ya uhaba wa Chakula, Serikali itahakikisha kuwa
Kitengo cha Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kinaendelea kusambaza mahindi katika
maeneo yenye uhaba wa chakula. Hadi sasa jumla ya Tani 20,000 zilishatolewa kwa Mikoa
ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Singida, Morogoro, Lindi, Tanga, Mtwara,
Pwani, Dar es Salaam, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara na Tabora. Aidha, Kitengo hicho
(NFRA) kitaendelea kununua nafaka mapema baada ya mavuno ili kuhakikisha kuwa Serikali
ina hifadhi ya kutosha ya chakula kwa ajili ya kusambaza katika maeneo yatakayokuwa
na uhaba wa chakula. Hadi tarehe 6 Februari 2013 Ghala la Taifa la Chakula lilikuwa
na jumla ya Tani 68,712.9 za mahindi pamoja na Tani 3,335.989 za Mtama.
Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya upatikanaji
wa chakula Nchini na kuhakikisha kuwa hakuna Mwananchi atakayepoteza maisha kutokana
na njaa. Nitoe wito kwa Wananchi kuendelea kuweka utaratibu wa kuhifadhi sehemu ya
mavuno yao baada ya kuvuna kwa ajili ya akiba ya baadaye badala ya kuuza mavuno yao
yote.
MAPAMBANO DHIDI YA UGONJWA WA MALARIA NCHINI
Hali
Halisi ya Ugonjwa wa Malaria Nchini
Mheshimiwa Spika,
Nchi yetu inayo changamoto kubwa ya kukabiliana na Magonjwa makubwa Duniani, yakiwemo
Malaria, Kifua Kikuu, UKIMWI, Saratani, n.k. Niruhusu leo katika Hotuba yangu nizungumzie
kidogo kuhusu Ugonjwa wa Malaria. Ugonjwa wa Malaria bado unaongoza kuwa sababu kubwa
za Wagonjwa wengi wanaohudhuria katika Vituo vya huduma za Afya Nchini. Aidha, ugonjwa
huu unaongoza kwa kusababisha vifo, hasa kwa Watoto walio chini ya umri wa miaka Mitano.
Takwimu kutoka Vituo vya kutolea huduma ya Afya Nchini zinaonesha kuwa, takriban Wagonjwa
Milioni 11 hadi 12 huhudhuria katika Vituo vya huduma za Afya kwa sababu ya ugonjwa
wa Malaria. Vilevile, tafiti zilizofanyika katika Jamii [Tanzania HIV/Malaria Indicator
Survey (THMIS) 2011/2012] zinaonesha kuwa Asilimia 10 ya Watoto katika Kaya wana maambukizi
ya vimelea vya ugonjwa wa Malaria.
ii) Jitihada za Serikali katika
kumaliza tatizo la Malaria Nchini Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana
na tatizo hili katika kuhakikisha Wananchi wanaendelea kujikinga na maambukizi dhidi
ya ugonjwa wa Malaria, Serikali imefanya mambo muhimu yafuatayo:
Moja: Kutekeleza
Mpango Mkakati wa Taifa wa Mapambano Dhidi ya Ugonjwa wa Malaria wa Miaka Mitano (2008-2013)
ambao una lengo la kupunguza vifo kwa Asilimia 80 ifikapo mwaka 2013 mwishoni. Utekelezaji
wa Mpango huu unafanyika kwa kushirikiana na Mikoa, Wilaya na Wadau mbalimbali hadi
katika ngazi ya Jamii;
Pili: Kusambaza na kuongeza matumizi ya vyandarua vyenye
viuatilifu vya muda mrefu katika Kaya. Hadi sasa zaidi ya vyandarua Milioni 26 vimesambazwa
kupitia Kampeni iliyolenga Watoto wenye umri chini ya miaka Mitano;
Tatu: Kutekeleza
Mpango wa Hati Punguzo unaolenga kuhakikisha Akina Mama Wajawazito na Watoto wanaozaliwa
wanaendelea kupata vyandarua hivyo na kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Malaria;
Nne: Kuendeleza
Mpango wa kunyunyizia dawa ya ukoko majumbani ili kutokomeza mazalia ya Mbu. Mpango
huo unaendelea kutekelezwa katika Mikoa ya Kagera, Mwanza na Mara ambapo zaidi ya
Kaya 1,440,000 sawa na Asilimia 90 katika Wilaya za Mikoa hiyo zitanyunyiziwa viuatilifu.
Kutokana na Mpango huo, zaidi ya Watu 6,500,000 wameendelea kukingwa dhidi ya maambukizi
ya ugonjwa wa Malaria;
Tano: Kuendeleza Mpango wa kuangamiza viluwiluwi vya
Mbu kwa kutumia njia za Kibaiolojia. Mpango huu ambao unafanywa na Serikali kwa ushirikiano
na Serikali ya Nchi ya Cuba unatekelezwa katika Jiji la Dar es Salaam kuanzia mwaka
2011;
Sita: Kutumia Mwongozo wa kutibu ugonjwa wa Malaria isiyo kali kwa kutumia
Dawa ya Mseto ya Artemether/Lumefantrine (ALu). Mwongozo huu unaendelea kutumika katika
Vituo vyote vya Umma vya kutolea huduma za Afya; na
Saba: Kusambaza kipimo
cha haraka cha kutambua na kuthibitisha uwepo wa vimelea vya Malaria kwenye damu katika
Vituo vyote vya Umma vya kutoa huduma za afya Nchini.
iii) Changamoto Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo makubwa yaliyopatikana, bado
kuna changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi. Changamoto hizo ni pamoja na:
Moja: Kujitokeza
kwa usugu wa mbu dhidi ya viuatilifu vya aina ya “pyrethroids” vinavyotumika katika
vyandarua na unyuziaji dawa ya ukoko majumbani;
Pili: Kupata vyanzo zaidi vya
fedha za ndani za kuendeleza mkakati wa unyunyiziaji dawa ya ukoko majumbani;
Tatu: Uwezo
mdogo wa uzalishaji wa dawa za kuangamiza viluwiluwi vya Mbu na kuanza kuangamiza
Viluwiluwi hivyo katika Jiji la Dar es Salaam; na
Nne: Kuendeleza uhamasishaji
Wananchi kutumia nyenzo na kushiriki katika mikakati iliyopo, hasa inayohitaji ushiriki
wao wa moja kwa moja, kama kuharibu mazalia ya Mbu.
iv) Matarajio ya Mkutano
wa United Against Malaria – Afrika Kusini Mheshimiwa Spika, katika
juhudi za kupambana na Malaria Duniani, Shirika la Roll Back Malaria Partnership wakishirikiana
na Wizara ya Afya ya Afrika Kusini wanatarajia kufanya Mkutano mkubwa unaohusu mapambano
dhidi ya Malaria kwa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuanzia
tarehe 9 - 11 Februari, 2013. Mkutano huo unatarajia kukutanisha Viongozi wa ngazi
ya juu kutoka Nchi za SADC ikiwa ni pamoja na baadhi ya Marais, Mawaziri Wakuu,
Mawaziri wa Afya na Mawaziri wa Michezo katika Nchi hizo. Mkutano huo pia utajumuisha
Viongozi wa juu wa Makampuni mbalimbali ya Sekta Binafsi.
Mheshimiwa
Spika, lengo la Mkutano huo ni kukutanisha Viongozi mbalimbali kwa lengo la kuendesha
mjadala kuhusu janga la Malaria katika Nchi za Afrika; ikizingatiwa kuwa ufadhili
wa utekelezaji wa mikakati mbalimbali unazidi kupungua. Mkutano huo unategemewa kuwa
chachu kwa Viongozi kuongeza Bajeti za udhibiti wa Malaria Nchini mwao na kuongeza
ushirikiano na Sekta Binafsi pamoja na Sekta ya Michezo, hususan katika Mpira wa Miguu
katika dhana nzima ya Mpango wa “Safe Companies”. Aidha, Mkutano huo unatarajiwa kuongeza
kasi ya Kupambana dhidi ya ugonjwa wa Malaria katika Nchi hizo.
Ni matumaini yangu kuwa, Mkutano huo utakuwa wa mafanikio makubwa kwa Nchi
za Kusini mwa Afrika katika vita dhidi ya ugonjwa wa Malaria. Vilevile, utatupatia
uzoefu kwa Nchi yetu katika kupambana na Ugonjwa huu wa Malaria.
v) Jitihada
za Chama cha Wabunge cha Kupambana na Malaria Mheshimiwa Spika,
katika jitihada za kupambana na Malaria Nchini, Muungano wa Wabunge wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano ya Tanzania walianzisha Asasi inayojulikana kama Tanzania Parliamentary
Against Malaria (TAPAMA). Lengo la kuanzishwa kwa Asasi hii ni kuongeza utashi wa
Kisiasa katika kushiriki na kutekeleza Mpango na Sera ya Taifa ya kutokomeza Ugonjwa
wa Malaria Nchini. Asasi hii ilisajiliwa mwaka 2008 na hadi sasa imetekeleza masuala
mbalimbali katika jitihada zake za kupambana na Malaria Nchini kama ifuatavyo:
Moja: Ugawaji
wa Vyandarua kwa Watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa Mikoa ya
Ruvuma, Kilimanjaro na Mwanza ambapo zaidi ya Watoto 2,500 walifaidika na huduma hii;
Pili: Kufanya
mazungumzo na Wawakilishi wa Bunge la Jumuiya ya Ulaya mwaka 2009 waliotembelea Tanzania
na kuona uwezekano wa Jumuiya ya Ulaya kusaidia zaidi Mapambano dhidi ya Malaria Tanzania.
Aidha, walifanya mazungumzo na Viongozi na Wawakilishi wa Asasi ya Malaria No More
ya Marekani, ambao waliongozwa na Balozi Mark Green na kuwezesha kuanza kwa Mradi
wa Zinduka, Malaria Haikubaliki;
Tatu: Kushiriki Kikao cha Nchi za Jumuiya
ya Ulaya Nchini Ufaransa mwaka 2009 ili kujadili juhudi za Viongozi wa Kisiasa katika
Kupamabana na Malaria Nchini;
Nne: Kushiriki kutayarisha Mwongozo (Advocacy
Guideline) utakaotumiwa na Wabunge, Madiwani na Viongozi wengine wa Kisiasa na Kijamii
katika Utekelezaji na ushawishi wao katika kutokomeza Malaria Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuwapongeza Wajumbe wote wa TAPAMA
chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Riziki Said Lulida, Mbunge wa Viti Maalum kwa juhudi
zao za kuhakikisha kuwa wanaungana na Wadau wengine Nchini na Duniani katika kutokomeza
ugonjwa wa Malaria. Nazipongeza pia Taasisi Zisizo za Kiserikali kwa ujumla wao ambazo
zimejitokeza katika Mapambano dhidi ya Magonjwa mbalimbali, yakiwemo UKIMWI, Kifua
Kikuu, Saratani, n.k. Tunawaomba Waheshimiwa Wabunge zaidi wazidi kujiunga na Asasi
hizi na hasa za Magonwa ili kuweka hamasa kwa Wananchi katika Kupambana na Maradhi
hayo. Aidha, natoa wito kwa Wananchi wote kwa ujumla kuunganisha nguvu za Kupambana
na Ugonjwa huu wa Malaria ili kunusuru nguvukazi ya Watanzania. Suala kubwa ni kuzingatia
masharti ya Wataalam kuanzia katika kutunza mazingira yetu na kutumia Vyandarua kama
kinga iliyo ya uhakika.
LISHE
Mheshimiwa
Spika, wakati nikitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa Tisa wa Bunge, mwezi Novemba,
2012 nilieleza kwa kifupi utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Lishe wa Mwaka 2011/2012
– 2015/2016. Pamoja na mambo mengine nilionesha hatua ambazo Serikali inachukua kuondokana
na tatizo la Lishe Nchini. Jambo kubwa na la msingi katika kupambana na tatizo
la Lishe ni kutoa elimu kwa Jamii ili kula vyakula vyenye Virutubisho muhimu hasa
kwa Mama Wajawazito na Watoto Wachanga. Jitihada za Serikali za kuwashirikisha Wadau
mbalimbali katika kutoa Elimu ya Lishe Nchini zimeleta mwamko mzuri ambapo Wadau mbalimbali
wakiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Wadau wa
Maendeleo sasa wanashiriki kikamilifu katika utoaji elimu na kukuza kilimo cha mazao
yenye virutubisho muhimu ili kuongeza vyakula vyenye virutubisho.
Mheshimiwa Spika, katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kupambana
na tatizo la Lishe Nchini, hivi karibuni Waheshimiwa Wabunge chini ya Uenyekiti wa
Mheshimiwa Lediana Mafuru Mng’ong’o Mbunge wa Viti Maalum wameunda Kikundi cha kuongeza
hamasa na kuzidisha chachu ya kutoa elimu kuhusu Lishe Bora hapa Nchini. Nimearifiwa
kwamba, Kikundi hicho cha Wabunge kimekutana tarehe 10 hadi 12 Januari, 2013 na kukubaliana
kuhusu kazi ambazo watafanya ili kuongeza sauti yao kwenye jamii juu ya umuhimu wa
Lishe Bora. Kikundi pia kimeandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitatu (2013-2015) wenye
malengo ya kukuza uelewa wa Umma juu ya Lishe, Chakula na Haki za Watoto. Aidha, kikundi
hicho kiliazimia kushawishi uwekaji wa vipaumbele vya Lishe katika Mipango ya Maendeleo
na Bajeti za Wizara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuingiza masuala ya
Lishe, Chakula na Haki za Watoto katika Sera na Mikakati mbalimbali ya Serikali. Azimio
lingine ni kuimarisha usimamizi wa kazi za Bunge kuhusu Lishe, Chakula na Haki za
Watoto.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa
hii kukishukuru kwa dhati kikundi hiki ambacho kimeona umuhimu wa kuunga mkono juhudi
za Serikali za kupambana na tatizo la Lishe, ikiwemo Utapiamlo. Nitumie fursa hii
kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kuanzisha kikundi hiki. Niwashukuru kwa kuona
umuhimu wa kusimamia tatizo hilo ili kupata suluhu ya kudumu. Ninatambua pia umuhimu
wa Waheshimiwa Wabunge kuhamasisha masuala ya Lishe kwa Wananchi wa Majimbo yao. Niwaombe
Waheshimiwa Wabunge wengine wote kushiriki kutoa msukumo wa pekee kwa Wananchi wa
Majimbo yenu katika Mapambano dhidi ya Utapiamlo ili kwa pamoja tujenge Taifa lenye
Watu walio na Lishe Bora. Lengo ni kuwawezesha kuchangia zaidi katika uzalishaji mali
na ukuaji wa uchumi wa Nchi kwa ujumla.
MCHAKATO KUELEKEA KATIBA MPYA
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa, Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imetangaza kumaliza kazi ya kukusanya maoni binafsi ya Wananchi
mmoja mmoja kama mchango wao kwa ajili ya kuandika Katiba Mpya. Aidha, imekamilisha
kazi ya kukutana na Makundi Maalum, Viongozi wa Kitaifa Wastaafu na Viongozi wa Kitaifa
waliopo Madarakani. Kwa maana hiyo, Tume sasa imekamilisha kazi ya ukusanyaji maoni
kama ilivyopangwa. Hivi sasa Tume inaendelea na kazi za uchambuzi wa maoni yaliyotolewa
na Wananchi na yale yaliyotolewa na Makundi Maalum ili baadaye kutayarisha Rasimu
ya Katiba ambayo itawasilishwa katika Mabaraza ya Katiba yatakayoitishwa na Tume Nchini
kote.
Kulingana na Ratiba, Mikutano ya Mabaraza ya
Katiba itafanyika kuanzia mwezi Juni, 2013 na itajumuisha Wajumbe watakaochaguliwa
na Wananchi wenyewe kuanzia ngazi ya Kijiji. Wajumbe hao ndio watapaswa kuwasilisha
maoni ya Wananchi katika Mikutano ya Mabaraza.
Mheshimiwa
Spika, nimearifiwa kuwa Tume imeandaa Rasimu ya Mwongozo wa namna bora na ya Kidemokrasia
ya kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ambao unaendelea kusambazwa Nchi nzima.
Mwogozo huo tayari umetangazwa katika Vyombo vya Habari ili Wananchi waufahamu na
kutoa maoni kuhusu namna ya kuuboresha.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa Rasimu hiyo ya Mwongozo, katika Mikoa ya Tanzania Bara ukiondoa
Mkoa wa Dar es Salaam, kila Kata itawakilishwa na Wajumbe wanne (4) watakaochaguliwa
kutoka miongoni mwa Wakazi wa Vijiji vilivyopo kwenye Kata ambao wataungana na Madiwani
wa Kata na Madiwani wa Viti Maalum kuunda Baraza la Katiba la Wilaya. Kwa Mkoa wa
Dar es Salaam, Tume imeandaa utaratibu tofauti wa kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya
Katiba ya Wilaya ambapo kila Kata watatoka Wajumbe wanane (8) ambao wataungana na
Madiwani wa Kata na Madiwani wa Viti Maalum. Kwa msingi huo, kutakuwa na jumla ya
Wajumbe 18,169 watakaohudhuria Mabaraza ya Katiba ya Wilaya Kwa Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Zanzibar, kutakuwa na Mabaraza
ya Katiba ya Wilaya Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa 13. Kila Shehia itawakilishwa
na Wajumbe watatu (3), ambao wataungana na Madiwani wa Wadi, Madiwani wa Viti Maalum
na Madiwani wa kuteuliwa waliopo kazini kwa sasa. Kwa msingi huo, Wajumbe wote wa
Mabaraza ya Katiba kwa Zanzibar watakuwa 1,198.
Wananchi
wanaopenda kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya watatakiwa kuwasilisha majina
yao kwa Maafisa Watendaji wa Vijiji na Mitaa kwa Tanzania Bara na kwa upande wa Tanzania
Zanzibar watawasilisha kwa Sheha kwa tarehe itakayoelekezwa na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba hapo baadaye.
Mheshimiwa Spika, napenda
kutoa wito kwa Viongozi wote katika ngazi za Wilaya na Serikali za Mitaa kusimamia
kikamilifu utaratibu ambao umewekwa na Tume. Kwa kufanya hivyo, Wajumbe ambao watashiriki
katika Mabaraza ya Katiba watapatikana kwa njia za Kidemokrasia na hivyo, kufanikisha
Vikao vya Mabaraza ya Katiba. Ni matumaini yangu kuwa Wananchi watausoma Mwongozo
huo, na baadaye kuwasilisha mapendekezo na maoni yao kwa Tume kabla ya kazi ya uchaguzi
wa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuanza rasmi.
Nitumie
fursa hii kuwaomba Wananchi wote kushiriki kikamilifu kutoa maoni kuhusu Mwongozo
huo na pia katika kuwapata Wajumbe watakaoshiriki katika Mabaraza ya Katiba kwa mujibu
wa Sheria, na vilevile Wajumbe hao washiriki kikamilifu katika Vikao vya Mabaraza
ya Katiba na kutoa maoni kwenye Rasimu ya Katiba.
RIPOTI YA TATHMINI
YA UTAWALA BORA AFRIKA (APRM)
Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza
dhamira ya uwazi na ujenzi wa pamoja wa utawala bora nchini kwa kuwashirikisha Wananchi,
Nchi yetu imekuwa miongoni mwa Nchi 33 za Umoja wa Afrika zilizoamua kwa hiari yake
kujiunga na Mpango wa Bara la Afrika wa Kujitathmini Kiutawala Bora (The African Peer
Review Mechanism - APRM). Tanzania ilijiunga na mchakato huo mwaka 2004, na Bunge
liliuridhia mwaka 2005.
Mheshimiwa Spika, Mpango
huu wa kujithamini Kiutawala Bora ni muhimu kwetu na unaakisi Sera zetu na za Waasisi
wa Taifa hili juu ya Kujikosoa na Kujisahihisha. Aidha, unahusisha Viongozi wa Afrika
na unatoa fursa kwa Wananchi kutathmini hali ya Utawala Bora katika Nchi zao na kuainisha
kwa pamoja mambo mazuri yanayopaswa kuendelezwa na yale yenye changamoto za kufanyiwa
kazi. Miongoni mwa sababu za Nchi yetu kujiunga na Mpango huu ni kutokana na ukweli
kwamba Watanzania tuna mengi ya kuifundisha Afrika na Watu wake kuhusu Utawala Bora
na sisi pia kujifunza kutoka kwa wenzetu.
Mheshimiwa
Spika, ninayo furaha kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa baada ya zoezi la muda mrefu
la kukusanya maoni Nchi nzima kuhusu Mpango huu ambapo Waheshimiwa Wabunge nao walishiriki
kutoa maoni yao kuhusu Utawala Bora, sasa hivi Nchi yetu, imefikia hatua muhimu katika
Mchakato huo wa kujitathmini kiutawala bora.
Tarehe
26 Januari 2013, Ripoti ya Hali ya Utawala Bora hapa nchini iliwasilishwa mbele ya
Wakuu wa Nchi za APRM Addis Ababa, Ethiopia ambapo Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wetu alipata fursa ya kuzungumzia mwelekeo wa Nchi yetu katika kujenga Taifa
imara zaidi katika kipindi cha miaka 50 ijayo.
Mheshimiwa
Spika, katika Ripoti hiyo ambayo itatumika kama rejea, zimeainishwa juhudi zetu kubwa
za kulinda amani Nchini. Pamoja na kuimarisha Utawala Bora wa Sheria na Haki za Binadamu.
Aidha, kupitia Ripoti hiyo, wenzetu katika masuala ya kuendesha Utawala Bora, Barani
Afrika na Duniani kwa ujumla wametambua jitihada zetu pamoja na mambo mengine katika
kuulinda Muungano, kuimarishwa kwa mapambano dhidi ya Rushwa na zaidi ya yote wamejua
sura ya Tanzania katika ukombozi na utetezi wa amani Afrika ambao Nchi yetu imepongezwa
sana kwa juhudi zake.
Ripoti hiyo pia imeainisha
changamoto ambazo wenzetu wa Afrika wanadhani tunapaswa kuzifanyia kazi zaidi. Changamoto
hizo ni pamoja na suala la kushughulikia Kero za Muungano, kuimarisha zaidi juhudi
za kuondoa umaskini na kuilinda amani ya Nchi yetu hasa kutokana na chokochoko za
Kidini zilizoanza kujitokeza. Tumeaswa kuutumia vyema mchakato wa sasa wa Mabadiliko
ya Katiba kuijenga Tanzania bora zaidi katika miaka 50 ijayo.
Mheshimiwa Spika, kuwasilishwa kwa Ripoti hiyo ya APRM kwa Wakuu wa Nchi
wa Mpango huu ndio mwanzo sasa wa Serikali yetu ya kuimarisha maeneo yaliyoonekana
kuwa tunafanya vyema. Pia hatua hiyo inatoa fursa ya kuanza kutekeleza Mpangokazi
wa Miaka Mitano ambao umeainisha namna gani ya kuyafanyia kazi maeneo ambayo wananchi
waliyaona kuwa yanapaswa kufanyiwa kazi zaidi. Suala hili liliwekewa msisitizo na
Mheshimiwa Rais katika Hotuba yake ya Mwisho wa Mwezi Januari 2013 aliyoitoa kwa Taifa.
Mheshimiwa Spika, kutokana na manufaa ya APRM kama daraja kati
ya Serikali na Wananchi wa kutatua matatizo yetu kwa pamoja, Serikali itaendelea kuiimarisha
Taasisi ya APRM hapa Nchini ili iweze kuwa kitovu chetu cha fikra (think tank) katika
kushauri kuhusu masuala ya Utawala Bora Nchini. Vilevile, kuiwezesha Taasisi hii kuendelea
kuwa kiungo kati ya Serikali yetu na Wananchi wake katika kutathmini na kutupatia
mrejesho juu ya mipango na Sera zetu za maendeleo.
Aidha,
Serikali itaendelea kufadhili shughuli za APRM, kuiimarisha Taasisi kwa raslimali
watu na fedha kwa ajili ya kazi pana zaidi za kutoa ushauri, kuunganisha Wadau mbalimbali
na kuendelea kuratibu tathmini nyingine katika siku zijazo kwa lengo la kujipa nafasi
ya kujikosoa ili kujisahihisha. Napenda kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya
Nje, Ulinzi na Usalama wakishirikiana na Sekretariati ya APRM Tanzania kwa kazi nzuri
waliyoifanya ambayo imetuwezesha kufikia mafanikio hayo.
UANZISHAJI WA
MAENEO MAPYA YA UTAWALA
Uanzishaji wa Mikoa na Wilaya
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa, mwezi Machi 2012,
Mheshimiwa Rais aliridhia kuanzisha Mikoa Mipya Minne (4) na Wilaya 19. Napenda kulijulisha
Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali sasa imekamilisha mchakato wa kuanzisha maeneo
hayo Mapya ya Utawala, kwa kuanzisha Mikoa Minne ya Geita, Simiyu, Njombe na Katavi.
Aidha, imekamilisha uanzishwaji wa Wilaya 19 za Buhigwe, Busega, Butiama, Chemba,
Gairo, Ikungi, Itilima, Kakonko, Kalambo, Kaliua, Kyerwa, Mbogwe, Mkalama, Mlele,
Momba, Nyang’wale, Nyasa, Uvinza na Wanging’ombe. Mikoa na Wilaya hizo tayari zimeshaanza
kufanya kazi na kutoa huduma mbalimbali kwa Wananchi. Vilevile, Mheshimiwa Rais alishafanya
Uteuzi wa Viongozi Wakuu wa Mikoa na Wilaya Mpya. Serikali imeendelea kupeleka Watumishi
na kuanza kujenga miundombinu muhimu katika maeneo husika. Hata hivyo, pamoja na dhamira
njema ya Serikali ya kuanzisha maeneo hayo, bado zipo changamoto nyingi, ikiwemo kupata
Watumishi wa kutosha ambazo Serikali inaendelea kuzitatua.
Uanzishaji wa Halmashauri
Mheshimiwa Spika,
ili kupeleka huduma karibu zaidi kwa Wananchi, Serikali pia iliazimia kuanzisha Halmashauri
Mpya 37. Uanzishaji wa Halmashauri hizo unaendelea na upo katika hatua mbalimbali
kwa kuzingatia makundi yafuatayo:
Kundi la Kwanza, linahusu Halmashauri
Mpya 8 za Manispaa, Miji na Jiji pamoja na Halmashauri Moja (1) ya Wilaya ambazo mchakato
wa uanzishaji wake tayari umekamilika Kisheria na zimeanza kufanya kazi. Kundi hili
linajumuisha Halmashauri za Jiji la Arusha, Manispaa ya Ilemela, Manispaa ya Lindi,
Halmashauri ya Mji wa Kahama, Halmashauri ya Mji wa Masasi, Halmashauri ya Mji wa
Makambako, Halmashauri ya Mji wa Geita, Halmashauri ya Mji wa Bariadi na Halmashauri
ya Wilaya ya Busokelo. Halmashauri hizo tayari zimepata Hati na kupangiwa Wakurugenzi.
Kundi
la Pili, linajumuisha Halmashauri Kumi (10) ambazo mchakato wa kuzianzisha umekamilika
na tayari zimetangazwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 23 Novemba 2012. Halmashauri
hizo ni Kalambo, Nsimbo, Mlele, Bumbuli, Ushetu, Msalala, Mbogwe, Busega, Momba na
Kyerwa. Halmashauri hizo kwa sasa zinaandaliwa Hati ili zianze.
Kundi la Tatu,
ni Halmashauri za Wilaya Kumi (10) ambazo mchakato wa uhakiki wake umekamilika na
Amri za Uanzishaji zimeshasainiwa na wakati wowote zitatangazwa katika Gazeti la Serikali.
Kundi hili linajumuisha Halmashauri za Wilaya za Buhigwe, Kaliua, Nyang’hwale, Wanging’ombe,
Chemba, Mkalama, Gairo, Nyasa, Itilima na Kakonko. Aidha, zipo Halmashauri nyingine
Nne (4) katika kundi hili ambazo Amri zake zinakamilishwa na hatimaye zitasainiwa
hivi karibuni. Halmashauri hizo ni Butiama, Tarime, Uvinza na Ikungi.
Kundi
la Nne, linajumuisha Halmashauri Nne ambazo Mchakato wa uanzishaji wake umekamilika
isipokuwa taratibu za Kisheria haziwezi kuanza kwa sababu baadhi ya Kata katika Halmashauri
hizo ni mpya, hivyo hakuna Madiwani. Halmashauri hizo Nne (4) ni za Miji ya Kasulu,
Handeni, Tunduma na Nzega. Mathalani, katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu kuna Kata
14, na kati ya hizo, Kata 6 ni mpya na hazina Madiwani. Kwa upande wa Halmashauri
ya Mji wa Handeni ina jumla ya Kata 12, kati ya hizo 9 ni mpya na hazina Madiwani.
Aidha, Halmashauri ya Mji wa Tunduma ina Kata 5 mpya na zote hazina Madiwani na Halmashauri
ya Mji wa Nzega ina Kata 10, na kati ya hizo Kata 3 ni mpya na hazina Madiwani.
Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha maeneo hayo mapya ni kuwawezesha Wananchi
kupata huduma karibu zaidi kwa Wananchi. Nitoe wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wilaya na
Watendaji wote kuwaongoza Wananchi kutumia fursa hiyo ya kuanzishwa kwa maeneo hayo
katika kujiletea maendeleo. Serikali itaendelea kupeleka huduma zaidi karibu na Wananchi
ili kuongeza kasi ya maendeleo katika maeneo hayo. Aidha, Serikali itaweka utaratibu
wa kuzipatia Halmashauri zinazoanzishwa Watumishi hatua kwa hatua.
HATUA
ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI DHIDI YA WATANZANIA WALIOFICHA FEDHA HARAMU NJE YA NCHI
Mheshimiwa Spika, tarehe 9 Novemba, 2012, Bunge lilipitisha Azimio Na.
9/2012 kuhusu kuitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha
haramu nje ya Nchi kufuatia Hoja Binafsi iliyowasilishwa na Mheshimiwa Zitto Kabwe
(Mb). Azimio hilo linahitaji, pamoja na mambo mengine, Serikali iwasiliane na Benki
ya Dunia kupitia Kitengo cha Asset Recovery Unit ili mabilioni yanayomilikiwa na Watanzania
katika Mabenki nje ya Nchi ambapo hufichwa kwa kukwepa kulipa kodi yarudishwe na kwamba
Watanzania wote wenye akaunti za fedha nje ya Nchi waeleze wamezipataje ili TAKUKURU
wachukue hatua za Kisheria dhidi ya watu wote wenye kumiliki fedha na mali kinyume
na mapato yao halali. Aidha, iliazimiwa na Bunge na Serikali ikakubali kwamba, katika
Mkutano wa Bunge wa 11 italeta Taarifa ya hatua iliyochukuliwa ili kuziba mianya ya
utoroshaji wa fedha nje ya Nchi.
Mheshimiwa Spika,
tarehe 31 Desemba, 2012, Mheshimiwa Rais aliridhia kuundwa kwa Kamati Maalum ya Kitaifa
kushughulia hoja hiyo ya kuitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania walioficha
fedha haramu nje ya Nchi. Kamati hiyo inaundwa na Wajumbe wanane wanaotoka katika
Taasisi za Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu; Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa;
Jeshi la Polisi; Benki Kuu ya Tanzania; Usalama wa Taifa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali. Kazi za Kamati hiyo ni:
Kuchunguza na kubaini
majina ya Watanzania wanaodaiwa kuficha fedha nje ya Nchi kinyume na Sheria na Kanuni
za Nchi;
Kuchunguza iwapo fedha hizo ni haramu
au la;
Kutambua Mabenki na Nchi zilizofichwa
fedha hizo;
Kuandaa mashtaka dhidi ya Watanzania
watakaobainika kuficha fedha haramu nje ya Nchi; na
Kuishauri
Serikali jinsi ya kuzuia uhalifu wa makosa ya fedha.
Mheshimiwa
Spika, Kamati hii imeanza kazi zake rasmi tarehe 9 Januari 2013 kwa kupanga namna
ya kutekeleza kazi zake ikiwemo kukusanya taarifa kuhusu Watanzania wanaodaiwa kutorosha
fedha haramu nje ya Nchi na kuangalia namna ya kupata taarifa muhimu nje ya Nchi.
Kamati hiyo inaratibiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Ili
kuiwezesha Kamati hii kufanya kazi yake kwa ufanisi ni wazi kwamba itahitaji kupata
ushirikiano mkubwa kutoka kwa Wananchi kwa kutoa taarifa mbalimbali kuhusu suala hili.
Hivyo, natoa wito kwa Wananchi wote wenye taarifa sahihi na za ukweli zinazoweza kuisadia
Kamati kutekeleza kazi hii wanahimizwa wajitokeze kutoa maoni yao kupitia Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kushirikiana kwa karibu na Kamati iliyoundwa na Serikali.
Aidha, nawaomba Waheshimiwa Wabunge nao kutoa ushirikiano wa kufanikisha kazi za Kamati
hii.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia
napenda niwashukuru wote waliofanikisha Mkutano huu wa Kumi wa Bunge. Kipekee nikushukuru
wewe binafsi Mheshimiwa Spika kwa kutuongoza vizuri ndani ya Bunge lako Tukufu. Nimshukuru
vilevile, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha Vikao vya Bunge kwa ufanisi.
Aidha, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu. Nimshukuru Katibu wa Bunge
na Wasaidizi wake kwa huduma nzuri walizozitoa wakati wote tukiwa hapa. Niwashukuru
Watendaji wa Serikali na Taasisi mbalimbali kwa kutekeleza majukumu yao vizuri ili
kufanikisha shughuli za Bunge zilizopangwa. Niwashukuru Waandishi wa Vyombo vya Habari
kwa kutufikishia habari kwa Wananchi yale yaliyojiri hapa Bungeni na kwa wakati. Vilevile,
navishukuru Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kazi yao nzuri na Madereva wote kwa huduma
zao kwa Washiriki wa Bunge hili.
Mheshimiwa Spika,
baada ya kusema hayo, naomba niwatakie Safari Njema na sasa natoa hoja kwamba Bunge
lako Tukufu liahirishwe hadi Siku ya Jumanne tarehe 9 Aprili, 2013 Saa 3:00 Asubuhi
kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.