2013-02-09 08:18:55

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa Siku ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2013


Enenda zako nawe ukafanye vivyo hivyo, ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Siku ya 21 ya Wagonjwa Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Februari, sanjari na Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes. Kwa mwaka huu, maadhimisho haya kimataifa yanafanyikia kwenye madhabahu ya BikiraMaria wa Altotting, Ujerumani. RealAudioMP3
Ni siku maalum iliyotengwa na Mama Kanisa kwa ajili ya kuonesha mshikamano wa dhati na wagonjwa, wahudumu wa sekta ya afya pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kwa njia ya sala, kushirikishana pamoja na kutolea mateso kwa ajili ya mafao ya Kanisa, pamoja na kutambua ile sura ya Kristo mteseka ambaye kwa njia mateso, kifo na ufufuko wake ameweza kuwakomboa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wagonjwa na wote wanaoteseka kiroho na kimwili, kwa kuwakumbusha kwamba, hawako peke yao, bali wao ni kielelezo cha sura ile ya Kristo. Anawasindikiza kwa sala katika hija ya maisha ya kiroho kutoka Lourdes, alama ya matumaini na neema hadi kwenye Madhabau ya Bikira Maria ya Altotting, wakitafakari kwa pamoja ile sura ya Msamaria mwema, inayowasaidia watu kutambua na kuonja upendo wa Mungu katika hija ya maisha yao yak ila siku, lakini zaidi kwa wagonjwa na wote wanaoteseka, wakihamasishwa kutenda kama alivyotenda yule Msamaria mwema.
Ili waamini waweze kuwaonjesha jirani zao upendo wa Mungu ambao hauna kifani, hawana budi kujishikamanisha na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala, ili kujitoa bila ya kujibakiza katika kuwahudumia wagonjwa wale wanaowafahamu na wale wasiowafahamu. Hili ni jukumu la kila mtu na wala si tu kwa wahudumu katika sekta ya afya na kwamba, waamini wanaweza kupata mang’amuzi haya kutoka katika imani, kwa kukumbatia mateso na mahangaiko, ili kupata maana na ukomavu unaowaunganisha wagonjwa na Kristo aliyeteseka kutokana na upendo usiokuwa na kifani kwa ajili ya binadamu.
Mababa wa Kanisa wanamwona Yesu mwenyewe kuwa ni kielelezo makini cha Msamaria mwema; ndiye Adam mpya na Mwana Mpendwa wa Mungu anayemwonjesha mwanadamu ule upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Yesu hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni jambo la kung’ang’ania sana, akajinyenyekesha hata kuutwaa mwili wa binadamu katika mateso na mahangaiko yake, ili aweze kuwa karibu naye, akashuka hadi kuzimu, ili kumpatia mwanadamu tumaini na mwanga, akimfariji kwa mvinyo safi wa matumaini.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani anasema kwamba, huu ni muda muafaka wa kuimarisha huduma ya upendo inayotolewa na Jumuiya mbali mbali za Kikristo, ili kumwezesha kila mwamini kuwa kweli ni kielelezo cha Msamaria mwema kwa ndugu na jirani zake. Kuna watakatifu kama Theresa wa Mtoto Yesu anayejulikana kama mtaalam wa sayansi ya upendo, aliyezama katika mateso ya Kristo, kiasi cha kuugua na hatimaye kufariki. Mtumishi wa Mungu Luigi Novarese anafahamika sana kwa ajili ya majitoleo yake ya sala kwa ajili na pamoja na wagonjwa hasa kwenye Madhabau ya Bikira Maria wa Lourdes.
Raoul Follereau alisukumwa na upendo wa jirani, akayatoa maisha yake kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wa Ukoma, kiasi hata Jumuiya ya Kimataifa ikatambua mchango wake na kuanzisha Siku ya Wagonjwa wa Ukoma Duniani. Kanisa linamkumbuka Mama Teresa wa Calcuta aliyekuwa anaanza utume wake kwa kufanya tafakari ya kina mbele ya Ekaristi Takatifu na baada ya hapo angeweza kutoka nje, akiwa na Rozari yake mkononi kumhudumia Kristo anayejionesha miongoni mwa wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Alikuwa na upendo wa pekee kwa wasiotakiwa, wasiopendwa wala kuhudumiwa.
Mtakatifu Anna Schaffer aliyaunganisha mateso na mahangaiko yake pamoja na yale ya Kristo, kitanda chake cha ugonjwa kikawa ni chumba chake cha tafakari na mateso yake kama kielelezo cha huduma ya kimissionari, akajiunga na Kristo kwa njia sala na upendo wa Mungu ulioendelea kumfariji.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika ujumbe wake kwa Siku ya 21 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2013 anamwangalia Bikira Maria, aliyefanya hija ya Njia ya Msalaba akimsindikiza Mwanaye Mpendwa, hata akadiriki kusimama pale chini ya Msalaba. Ni Mama ambaye hakupoteza tumaini kutokana na ushindi wa Mungu dhidi ya dhambi, mateso na kifo; akaonesha jinsi anavyokumbatia imani na upendo kutoka kwa Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo, aliyezaliwa Bethlehem na kufa pale juu Msalabani na siku ya tatu akafufuka, kielelezo cha matumaini mapya na ukaribu wa Kristo unaoendelea kufariji.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anachukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wote wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa pamoja na kushiriki katika utume wa Mama Kanisa katika huduma kwa wagonjwa na wanyonge. Anawatakia kheri na baraka tele na kwa njia ya maombezi ya Bikira Maria waweze kupata faraja na tumaini thabiti. Awasaidie wahudumu wa matendo ya huruma waweze kuwa kweli ni Wasamaria wema kwa ndugu na jirani zao wanaoteseka kutokana na ugonjwa na mahangaiko.







All the contents on this site are copyrighted ©.