2013-02-09 09:13:59

Marehemu Askofu Msarikie kuzikwa hapo tarehe 14 Februari 2013 kwenye Kanisa kuu la Kristo Mfalme, Moshi


Askofu mstaafu Amedeus Msarikie wa Jimbo Katoliki Moshi, aliyefariki dunia wakati akipata matibabu Jijini Nairobi, anatarajiwa kuzikwa kwenye Kanisa kuu la Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki Moshi, hapo tarehe 14 Februari 2013.

Taarifa kutoka Jimbo Katoliki Moshi zinabainisha kwamba, Mwili wa Marehemu Askofu Msarikie unatarajiwa kuwasili kwenye Kiwanja cha Kimataifa cha Kilimanjaro KIA, Jumatano asubuhi tarehe 13 Februari 2013 na baadaye msafara kuelekea kwenye Kanisa kuu, ambako waamini na watu wenye mapenzi mema watapata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho.

Askofu Amedeus Msarikie amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 82, baada ya kuliongoza Jimbo Katoliki Moshi kwa kipindi cha miaka 23. Marehemu Askofu Msarikie anakumbukwa na wengi kwa kupenda kuwekeza zaidi katika elimu. Wachunguzi wa mambo wanasema, pengine Jimbo Katoliki Moshi ni kati ya Majimbo ya Kanisa Katoliki Tanzania yaliyowekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu, kuanzia: elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo. Alikuwa ni muasisi wa Chuo Kikuu kishiriki cha elimu, Mwenge.

Anakumbukwa kwa namna ya pekee na Mapadre na wote waliopitia mikononi mwake alipokuwa Baba mlezi wa maisha ya kiroho, St. James Seminary. Kwa miaka mingi amekuwa ni Mwenyekiti wa Tume ya Walei Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na matunda ya kazi zake kwa kushirikiana na Maaskofu wengine yanaonekana. RIP. Amina.







All the contents on this site are copyrighted ©.