TANZIA: Askofu Thomas Laizer wa Jimbo la Kaskazini Kati Arusha, Kanisa la Kiluteri
la Kiinjili Tanzania amefariki dunia
Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, Februari 7, 2013, ametuma salamu za rambirambi
kwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Mkuu Dkt. Alex
Malasusa kuombeleza kifo cha Askofu Thomas O. Laizer wa Jimbo la Kaskazini Kati Arusha
la KKKT aliyeaga dunia tarehe 7 Februari 2013.
Katika salamu zake, Rais Kikwete
amemwambia Askofu Mkuu Malasusa: “Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa
za kifo cha Askofu Thomas Laizer ambaye nimejulishwa kuwa ameaga dunia muda mfupi
uliopita, jioni ya leo, katika Hospitali ya Rufaa ya Selian, Arusha.”
“Askofu
Thomas Laizer ametutoka lakini tutaendelea kumkumbuka kama kiongozi aliyetoa mchango
mkubwa katika uongozi wa kiroho wa Watanzania na ambaye wakati huo alitafuta namna
bora zaidi ya kuwatumikia waumini wake. Daima atakumbukwa kama kiongozi ambaye alitumia
vipaji vyake vyote kuwatumikia waumini wake na wote waliokuwa chini yake.”
Ameongeza
Rais kikwete: “Kufuatia msiba huu mkubwa, nakutumia wewe Baba Askofu Mkuu Alex Malasusa
salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kukupa pole ya msiba huu na kupitia kwako
kuwapa pole nyingi maaskofu na viongozi wenzako katika KKKT pamoja na waumini wote
wa Kanisa kwa kuondokewa na kiongozi mwenzao na muumini mwenzao.”
Aidha, Rais
Kikwete ameongeza, “Pia kupitia kwako Baba Askofu Mkuu, natuma salamu nyingi za moyoni
mwangu kwa familia na wana-ndugu wa Marehemu Thomas Laizer. Naungana nao katika kuomboleza.
Naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na Baba, Babu na mhimili
wa familia. Nawaombea subira ili waweze kuvuka kipindi hiki kwa sababu yote ni Mapenzi
ya Mungu. Aidha, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke
pema peponi roho ya Marehemu Thomas Laizer. Amen.”