2013-02-08 07:22:30

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Tano ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa


Tunakuleteeni kipindi Tafakari Neno la Mungu, tayari tukiwa Dominika ya tano ya mwaka C. Mama Kanisa ametuwekea Neno akitukumbusha wito wetu na wajibu wetu wa kutanganza Neno la wokovu kwa mataifa, ili wapate kuokolewa. RealAudioMP3

Hata hivyo twadaiwa sisi wenyewe kutakaswa na kukiri ukuu wa Bwana kwa ajili ya wajibu huo. Nabii Isaya katika somo la kwanza yuko katika ndoto na anamwona Bwana ambaye ameketi katika kiti cha enzi kilicho juu sana.

Bwana huyu aliye katika kiti cha enzi amezungukwa na Maserafi ambao wanamwimbia wimbo maarufu wakisema “mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu”. Katika hili Nabii Isaya anaona utukufu wa Mungu ukingaa mbele yake na kwa unyenyekevu anakiri udhaifu na dhambi zake mbele ya Mungu. Kwa hakika ndivyo inavyopaswa kuwa mbele ya fumbo kuu. Mwaliko kwako mpendwa unayenisikiliza ni kuingia katika maono ya nabii Isaya na kuaanza kutafakari ukuu wa Mungu, kuguswa na hatimaye kuanza safari ya kutumwa kwa ajili ya mataifa, umisionari wetu.

Nabii Isaya anapoona utakatifu wa Bwana anaogopa, hata hivyo haogopi na kukimbia bali anabaki ili aweze kuonja uzuri wa ukuu huo. Namna ya kuonja ukuu wa Bwana ni kukiri kwa unyenyekevu mkubwa kutositahili kwake kuona mambo makuu hayo, anasema “ole wangu mimi mwenye midomo michafu na ambaye hukaa katika watu wachafu” Anakiri pia udhaifu kwa ajili ya wengine.

Kama Mwana wa Mungu alivyojinyenyekeza mno na Baba yake akamkirimia jina lipitalo kila jina, vivyohivyo katika mastahili ya Mwana wa Mungu Nabii Isaya katika upole wake anakirimiwa zawadi ya ondoleo la dhambi. Zawadi hii inatolewa pale mmoja wa maserafi anapomgusa kinywa chake kwa kaa la moto na kumwambia umeondolewa dhambi zako. Kisha zawadi ya ondoleo la dhambi anatumwa kwa ajili ya kutangaza Neno la Mungu kwa jumuiya yake.

Mpendwa hivi leo kaa la moto hutujia kwa njia ya sakramenti ya ubatizo, Ekaristi Takatifu, Kipaimara, kitubio nk. na mara mwaliko wa kutumwa hufuata, maana tukishapokea neema za Bwana tuna nguvu kwa ajili ya kuhubiri Habari njema. Wapendwa kwa ubatizo tumetakaswa kwa ajili ya wajibu wa kuokoka sisi wenyewe lakini pia kwa ajili ya wengine, basi ni kazi kwako kuyaweka mausia ya Bwana yakujiayo kwa njia ya Neno lake kila siku katika mwendo wa kimisionari.

Katika somo la II Mtakatifu Paulo akiwaandikia Wakorintho anataka kuwahakikishia ile imani waliyonayo ina msingi katika Ufufuko wa Bwana ambayo imewafikia kwa njia ya Mitume. Anasema Bwana alikufa kwa ajili ya dhambi na akafufuka na kuwatokea Mitume, kwanza Mtakatifu Petro na kisha wengine. Mwishoni alinitokea mimi ambaye sikustahili kutokewa na Bwana kwa sababu naliliudhi Kanisa, lakini kwa Neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo”. Mtume Paulo anasema kwa neema ya Mungu niliyoipokea nimefanya kazi nzito hata kuwapita wengine, lakini sijivuni bali ni neema ya Mungu pamoja nami. Wakorintho wanaitwa sasa kuishika imani, kwa maana katika kuishika ndiko kuna wokovu wa milele.

Katika Injili, Luka tunapata kusikia juu ya wito wa Mitume. Bwana yuko kando ya ziwa Genezareti, pale kuna vyombo viwili na Bwana anaingia chombo kimojawapo na kumtaka Mt. Petro akipeleke mbali kidogo na pwani. Jambo la kwanza hapa tunaloliona ni uteuzi wa Mt Petro kuwa kiongozi mkuu. Bwana akiwa katika chombo kile anawafundisha watu na akishakumaliza mafundisho yake anamwambia Petro tweka mpaka kilindini! Mt. Petro anasita kwa sababu hawakupata samaki usiku kucha, lakini anaamini na kukiri akisema kwa neno lako nitazishusha nyavu. Matokeo ya kuaamini kwake wanapata samaki wengi. Wafanye nini sasa kwa wingi huu? Wakawaita washirika wao. Hapa twajifunza kuwa jambo jema ambalo ni wokovu ni kwa ajili ya wote.

Mpendwa msikilizaji, mambo yote haya, kwa Mt Petro ni mambo ya ajabu na hivi anaanguka kifudifudi mbele ya Bwana, alama ya ungamo la dhambi kama alivyofanya Nabii Isaya katika somo la I na kisha anakubali na kusadiki ukuu wa Yesu Kristu ya kuwa ni Mwana wa Mungu. Kinachofuata daima kama Nabii Isaya alivyofanyiwa ni kutumwa, sasa utavua watu badala ya samaki! Mara moja pasipo kuchelewa wanaacha nyavu zao na kumfuata Bwana.

Katika injili hii ya leo twaweza kujifunza kama nilivyokwisha sema, yafuatayo yaani wajibu wa kuwasaidia watu wote ili waokoke uko katika ubatizo wetu na sakramenti nyingine zinazotupatia baraka kwa ajili ya utume. Bwana hafundishi akiwa pwani bali yuko ziwani na hivi mwinjili ataka kutuambia kuwa sasa baada ya kusikia Neno la Mungu Jumapili lazima kwenda kwenye maisha ya kawaida na kutangaza ujumbe huo, ndiyo kusema katika Jumuiya Ndogondogo za Kikristo.

Katika chombo kuna watu wa aina zote wadhambi na wema kumbe wokovu si kwa wema tu bali wadhambi, cha msingi ni kuungama kama Mt. Petro alivyofanya mbela ya Bwana. Mt. Petro ndiye anayepeleka chombo ziwani, hapa polepole Bwana anatangaza ukuu wa Mt. Petro katika Kanisa akikabidhiwa kuongoza na kuchunga taifa la Mungu, akiwa mfano hai wa kukiri imani mbele ya Bwana. Tena Mtakatifu Petro hapeleki chombo kadri anavyotaka bali atakavyo Bwana, kumbe Kanisa analoliongoza Baba Mtakatifu ni Kanisa la Bwana, na hivi atafanya anachotaka Bwana, yaani kusikiliza na kufuata mapenzi ya Mungu.

Kumbe wito kwako unayenisikiliza ni kuitikia wito wa Mungu kwa imani na kukubali kuongozwa na Bwana siku zote na si vionjo vyako wala vya mwingine! Jumuiya Ndogondogo ni chombo cha Bwana na si chaguo ambalo ni kwa ajili ya mtu fulani, kumbe tutekeleze wito huo ulio wa tija kwa wokovu wetu.

Ni vema, ndugu yangu mpendwa ukumbuke tunapovua samaki baada ya muda samaki hawa hufa, kumbe ndiyo maana leo Bwana anatualika kuvua watu ambao wakishondolewa katika giza la dhambi huishi milele. Kazi kubwa ni kuondokana na visasi kati yetu sisi wenyewe na kuwasaidia wengine waondokane na vita, wivu, uongo, uvunjifu wa amani kwa sababu ya imani na sadiki tofauti, uhalibifu wa maisha adilifu katika familia na waweze kuishi kwa amani.

Nikutakie furaha na amani katika kipindi hiki na hasa tunapojiandaa hapo tarehe 13Februari kuanza kipindi cha Kwaresima. Iwe ni fursa ya kusali, kutafakari Neno la Mungu, kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa pamoja na kumwilisha Imani katika matendo ya huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.









All the contents on this site are copyrighted ©.