2013-02-08 08:43:58

"Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo"!


Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la Wahudumu Katika Sekta ya Afya anasema, Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2013 yanaongozwa na kauli mbiu “Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo”. Kilele cha maadhimisho haya ni hapo tarehe 11 Februari 2013 kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes.
Hii ni siku iliyoanzishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili kunako tarehe 13 Mei 1992, kama sehemu ya utambuzi wa dhamana na wajibu wa Mama Kanisa katika kuendeleza mchakato wa huduma kwa wagonjwa, utume ambao ulianzishwa na Kristo mwenyewe, kama harakati za kumkomboa mtu mzima: kiroho na kimwili.
Siku hii inalenga pamoja na mambo mengine, kuonesha mshikamano wa dhati na wagonjwa pamoja na wale wote wanaoteseka kiroho na kimwili, ili wanasiasa, watunga sera na wadau mbali mbali waweze kuchangia kwa hali na mali katika maboresho ya huduma ya afya, kwa kukumbatia Injili ya Uhai. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuitambua ile sura ya Yesu Kristo aliyeteseka, akafa na kufufuka kutoka katika wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti miongoni mwa wagonjwa wanaokutana nao katika familia, hospitali na nyumba maalum za wagonjwa na wazee.
Maadhimisho ya Siku ya 21 ya Wagonjwa Duniani kwa mwaka 2013 yanafanyika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Altotting, Ujerumani. Ni fursa kwa wataalam mbali mbali kujadili umuhimu wa kuwahudumia wagonjwa kiroho na kimwili pamoja na kutembelea wagonjwa waliolazwa katika Hospitali mbali mbali nchini Ujerumani. Haya ni matendo ambayo yanaweza pia kutekelezwa na waamini katika Majimbo na Parokia zao, kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani.
Askofu mkuu Zimowski anasema, katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuiga mfano wa Msamaria mwema, aliyeona, akaguswa na taabu pamoja na mahangaiko ya yule mgonjwa, kiasi cha kumshughulikia. Yesu Kristo ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha Msamaria mwema, aliyejitwalia hali ya ubinadamu, ili kumganga mwanadamu na ile divai ya huruma ya Mungu, inayoendelezwa na Mama Kanisa kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Ni changamoto na mwaliko wa kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo na wote wanaoteseka kiroho na kimwili.
Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani iwe ni fursa ya kujenga utamaduni wa kusali kwa ajili pamoja na wagonjwa, ili wagonjwa waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu, kama anavyofafanua Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. Wafanyakazi katika sekta ya afya wanapaswa kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu; wajitahidi kukumbatia na kuenzi Injili ya Uhai na kwamba, dhamana yao kubwa ni kulinda na kutetea uhai wa binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo! Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, iwasukume kuwa ni Wasamaria wema, wanaoguswa na mateso ya wagonjwa wanaowahudumia kila siku.








All the contents on this site are copyrighted ©.