2013-02-07 08:19:50

Wanasiasa kamwe wasifanye mchezo mbaya na Katiba ya Nchi!


Katiba ya nchi ni sheria mama inayotokana na makubaliano ya wananchi wenyewe juu ya namna ya kuongoza na kuratibu maisha yao kama taifa. Ni chombo kinachoainisha haki na wajibu wa kila mwananchi na kwamba, ni chombo kitakatifu ambacho kama kikitumiwa vyema, kitawawezesha wananchi kuishi kwa amani na utulivu, wakiongozwa na maadili pamoja na utu wema. RealAudioMP3
Baada ya maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya uhuru wa nchi nyingi za Kiafrika, mataifa kadhaa yameanzisha mchakato wa kufanya marekebisho makubwa au kuandika upya Katiba za nchi zao kwa “kusoma alama za nyakati” na mwelekeo wa upepo kimataifa. Baadhi ya vyama vya kisiasa vilivyokuwa vinawania kupewa ridhaa ya kuongoza nchi na wananchi wamekuwa wakitumia Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba kama ajenda nyeti inayopania kudumisha utawala wa sheria, demokrasia, amani na maendeleo endelevu.
Kwa bahati mbaya katika mchakato huu, nchi kadhaa Barani Afrika zimetua nanga ya matumaini ya wananchi wake kwa kuwa na Katiba Mpya, nyingine zinaendelea na mchakato ambao bado haujakamilika. Baadhi zimekwama na cheche za upinzani zinaanza kujionesha hapa na pale!
Habari kutoka Zambia zinasema kwamba, Jukwaa la Wananchi wa Zambia, linalojumuisha: Chama cha Wanasheria wa Zambia, Umoja wa Baraza la Makanisa Zambia, Umoja wa Makanisa ya Kiprotestant Zambia pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia, kwa ufupi; Jukwaa la Oasisi limetoa tamko kuhusiana na mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Zambia ambao kwa sasa unaonekana kukwama kutokana na ukata unaotishia kutokuwepo na uwezekano wa Muswada wa Katiba Mpya ya Zambia kupigiwa kura ya maoni, kabla ya kupitishwa na kuwa Sheria mama ya Zambia.
Viongozi wakuu wa Zambia walipoingia madarakani katika hotuba zao za mwanzo waliweka bayana kwamba, Muswada wa Sheria ya Katiba ya Zambia utapaswa kupigiwa kura ya maoni, lakini mwelekeo huu unaanza kufifia ndio maana Jukwaa la Oasis linapokea habari hizi kwa mshtuko mkubwa, kwani inaonesha kwamba, Chama Tawala nchini Zambia hakina utashi wa kisiasa kuitisha kura ya maoni juu ya Muswada wa Katiba Mpya ya Zambia. Ni jambo lisilokubalika kwa Serikali kutotenga bajeti kwa ajili ya kuendeleza mchako huu mintarafu sheria za nchi na muda uliokubalika.
Jukwaa hili linaonya kwamba, ikiwa kama Chama Tawala na Serikali ya Zambia katika ujumla wake, itashindwa kuridhia matakwa ya kilio cha Katiba Mpya nchini humo, wananchi wanaweza kuonesha nguvu ya umma, jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo na ustawi wa nchi.
Hii ni changamoto kwa Serikali mbali mbali kuhakikisha kwamba, mchakato wa Katiba Mpya unakamilika kwa ajili ya mafao ya wengi na kamwe lisiwe ni jukwaa la kutaka kupata ridhaa ya kuongoza nchi na baadaye kuwatekeleza wananchi na viongozi kuingia mitini kama wanavyosema Waswahili!








All the contents on this site are copyrighted ©.