2013-02-07 08:36:23

Mafanikio ya Chuo Kikuu cha Mt. Augustino cha Tanzania, SAUT


Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania, SAUT, Mheshimiwa Padre Charles Kitima katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha baadhi ya mafanikio ya SAUT katika kipindi cha miaka 14 iliyopita. Anaelezea kwa kifupi historia ya SAUT na mchango wake katika azma ya Uinjilishaji Mpya unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. RealAudioMP3

Chuo Kikuu cha SAUT kilianzishwa kunako Mwaka 1998 kikiwa na wanafunzi 294, leo hii kina jumla ya wanafunzi 26, 500 na kina matawi 11 sehemu mbali mbali za Tanzania. Dr. Kitima anasema, Kanisa Katoliki Tanzania linawekeza katika sekta ya elimu bora na makini si tu kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika maboresho ya sekta ya elimu ya juu, bali ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina. Elimu kwa Kanisa ni chombo cha Uinjilishaji.

Padre Kitima anabainisha kwamba, kwa njia elimu ya juu: wanafunzi na wasomi wanapata fursa ya kukutana na Yesu katika hija ya majiundo yao, ili aweze kuwafunda na kuwaunda wasomi. Anapenda kuwakirimia vijana tunu za uongozi bora, ujuzi, weledi, uaminifu, maadili na utu wema, ili kuwajengea uwezo wa kujitoa bila ya kujibakiza katika kuhudumia Jamii ya Watanzania na Afrika kwa ujumla kwani hadi sasa kuna wanfunzi wengi wanaotoka sehemu mbali mbali za Bara la Afrika wanosoma SAUT.

Mafanikio yote yaliyokwisha kupatikana SAUT ni kielelezo makini cha uongozi thabiti na mshikamano kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Kwa njia ya Bodi ya Wadhamini wa SAUT inayoundwa na Maaskofu Wakuu nchini Tanzania, imeweza kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi mkubwa na kwamba, rasilimali za: watu, fedha na miundo mbinu ni kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa SAUT na Vyuo vyake vishiriki ambavyo kwa sasa vimefikia 11 na vingine viko mbioni kuanzishwa, ili kuhakikisha kwamba, elimu bora na yenye gharama nafuu inapatikana kwa watanzania wengi zaidi.







All the contents on this site are copyrighted ©.