Mikakati ya Caritas Rwanda katika huduma za upendo na mshikamano kwa Mwaka 2013
Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Rwanda, Caritas, limehitimisha mkutano
wake wa mwaka kwa kutoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi na vitengo vyake vikuu
vinne yaani: Utawala, Afya, Maendeleo na Huduma za Kijamii. Utekelezaji huu unalihusisha
pia Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda kwa kuliomba lijihusishe zaidi na zaidi katika
huduma kwa wafungwa magerezani.
Tume ya haki, amani, familia, vijana na elimu
imeombwa pia kuwa karibu zaidi na Caritas, ili kwa pamoja waweze kutoa huduma bora
na makini zaidi kwa Familia ya Mungu nchini Rwanda. Katika Maadhimisho ya Mwaka wa
Imani, Caritas Rwanda inatarajia kuchapisha ujumbe maalum kwa ajili ya waamini, kama
sehemu ya mchakato wa kuendeleza huduma kwa wafungwa magerezani; wakimbizi na wahamiaji
ambao bado wako kwenye kambi za wakimbizi nchini humo.
Caritas katika Majimbo
mbali mbali nchini Rwanda inahamasishwa kujenga vituo maalum vitakavyosaidia kutoa
elimu ya ufundi na majiundo makini kwa watoto na vijana. Ili kuhamasisha uelewa makini
wa huduma zinazotolewa na Caritas, kuna haja ya kuanzisha Siku ya Caritas Kiparokia.
Taasisi inayoratibu huduma za afya zinazotolewa na Kanisa Katoliki nchini Rwanda,
imewapongeza wajumbe wa Caritas Rwanda kwa mchango na huduma wanayotoa kwa wananchi
wa Rwanda. Caritas Rwanda imealikwa pia kushiriki katika mkutano mkuu wa Taasisi hii
utakaofanyika tarehe 14 Machi 2013.