2013-02-06 07:34:12

Mama Kanisa kutolea Rehema Kamili katika Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani 2013


Ukombozi wa mwanadamu ni matunda ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo na kwamba, mateso na magangaiko ya kila mwanadamu inaweza kuwa fursa ya kushiriki katika mateso yanayoleta ukombozi kwa kuyatimiza katika mwili wao yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake yaani Kanisa. RealAudioMP3
Ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka wa Imani mintarafu Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kutambua maana ya mateso na ushiriki wake miongoni mwa wafuasi wa Kristo. Matendo ya huruma yanayotekelezwa na Mama Kanisa kwa njia ya Watoto wake ni ushuhuda wa imani tendaji, mwaliko wa kurithisha utamaduni huu hata kwa watoto wakiwa bado katika umri mdogo, ili waweze kujifunza kugawana kile kidogo walicho nacho na jirani zao pamoja na kuwasaidia watu wenye shida zaidi.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema, Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani, ni fursa ya kufanya Katekesi makini kuhusu maana ya ukombozi katika mateso na mahangaiko ya wagonjwa, kwa wahudumu wa sekta ya afya na wadau mbali mbali wanaojitoa usiku na mchana kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa kiroho na kimwili, daima wakijitahidi kuiga mfano wa Msamaria mwema, huku wakihamasishwa, nenda nawe ukatende vivyo hivyo!
Ni mwaliko wa kuwatendea mema wagonjwa na wote wanaoteseka kwa njia ya maisha yako mwenyewe! Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani, sanjari na Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes yatakamilika kwa Ibada ya Misa Takatifu, itakayoongozwa na Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, mwakilishi wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani ambayo Mwaka huu kimataifa yanafanyika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Altotting, atatoa Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa.
Ili kuwawezesha waamini kuweza kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2013, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatoa Rehema Kamili kwa wote watakaotimiza masharti yaliyotolewa na Mama Kanisa: kwa kufanya toba na matendo ya huruma, wakisumukwa na mfano bora wa Msamaria mwema, moyo wa Imani na huruma, kwa kujitoa kuwasaidia wagonjwa; na ikiwa kama wao wenyewe ni wagonjwa; basi kuyapokea wenyewe mateso haya kwa unyenyekevu wakimtolea Mwenyezi Mungu kama kielelezo cha ushuhuda wa imani kwa njia ya Injili ya Mateso.
Waamini wanaweza kupokea Rehema Kamili ikiwa kama maisha yao ya kiroho yatakuwa safi mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kushiriki kikamilifu Sakramenti ya Upatanisho, Ekaristi Takatifu pamoja na kusali kwa nia za Baba Mtakatifu pamoja na kuombea roho za waamini Marehemu, kwa wote watakaoshiriki Maadhimisho haya kuanzia tarehe 7 hadi tarehe 11 Februari 2013, kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Altotting au katika Makanisa maalum yaliyotengwa na viongozi wa Kanisa, watashiriki kwa Ibada na uchaji mkuu Ibada ya kuomba neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Waamini hao watatakiwa pia kusali: Baba Yetu; Kanuni ya Imani pamoja na kufanya Ibada kwa Bikira Maria.
Kwa wale ambao wanawahudumia wagonjwa na kutokana na sababu mbali mbali watashindwa kuhudhuria katika Ibada, wanaweza pia kupokea Rehema Kamili ikiwa kama katika siku hizi zilizopangwa, watajitoa kikamilifu kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa kama alivyofanya Msamaria mwema. Waamini wajizuiea kutenda dhambi.
Wagonjwa na Wazee ambao hawataweza kuhudhuria Ibada kama ilivyoelekezwa, wataweza kushiriki kwa moyo na ibada pamoja na kutekeleza masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa ili kupokea Rehema Kamili, wakitolea mateso na mahangaiko yao kiroho na kimwili kwa Bikira Maria msaada wa Wagonjwa.
Waamini pia wanaweza kupata rehema ya muda kwa njia ya Kanisa, wakati wote watakapomkimbilia Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, kwa mioyo yenye toba, katika siku zilizotajwa hapo juu; watapaswa kusali kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wa mwili na roho, wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Rehema Kamili na Rehema ya Muda inatolewa tu katika kipindi hiki maalum.
Hati ya Rehema Kamili imetolewa na Kardinali Manuel Monteiro de Castro, Mhudumu mkuu wa Toba.








All the contents on this site are copyrighted ©.