Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita pamoja na Rais Giorgio Napolitano wa Italia,
kabla ya kuhudhuria Tamasha la Muziki, kama sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 84 ya Mkataba
wa Laterano, uliotenganisha shughuli za Kanisa na Serikali ya Italia, walifanya mazungumzo
ya faragha kwa takribani dakika 20.
Mazungumzo haya yamekuwa ni muhimu sana
wakati huu, Rais Napolitano anapojiandaa kung'atuka kutoka madarakani baada ya kuwaongoza
wananchi wa Italia katika kipindi cha miaka saba ya shida na changamoto kubwa kutoka
ndani na nje ya Italia yenyewe.
Viongozi hawa wawili wanaoheshimiana na kuthaminiana
katika utekelezaji wa majukumu yao, wamezungumza kwa kina na mapana kuhusu matukio
mbali mbali yanayotarajiwa kufanyika nchini Italia. Wamejadili pia masuala mbali mbali
yanayoigusa Jumuiya ya Kimataifa, lakini kwa namna ya pekee, ukosefu wa msingi ya
haki na amani huko Mashariki ya Kati na Afrika.