2013-02-05 14:21:41

Mwaka wa Imani nchini India: mambo makuu yanayopaswa kuzingatiwa!


Baraza la Maaskofu Katoliki India katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, linawaalika waamini kusimama kidete kutolea ushuhuda wa imani katika matendo kwa kukabiliana na changamoto mbali mbali katika hija ya maisha yao bila ya kukata tama kwa kuzingatia mambo msingi yafuatayo. Waamini wanahamasishwa kutojishikamanisha mno na malimwengu, kwani huko watatopea na kupotea gizani na badala yake, wasimame kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu.

Waamini wajibidishe kuwarithisha watoto na vijana wa kizazi kipya misingi ya imani ya Kanisa Katoliki pamoja na sadaka ambayo wadau mbali mbali wa Injili wameitoa kama njia ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu nchini humo. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, Parokia na Majimbo yachague wahamasishaji watakaotoa changamoto elekezi katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kwa kushirikiana na vyama vya kitume, wazee, watoto, vijana na familia za Kikristo.

Mwaka wa Imani uwawezeshe waamini kushikamana katika huduma kwa kuwamegea upendo maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Parokia zianzishe tume za haki na amani, zitakazokuwa na jukumu la kuhamasisha umoja na mshikamano; upatanisho na msamaha miongoni mwa Jamii ya watu. Wapange siku maalum ya kuadhimisha Siku ya Amani Kiparokia, kwa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao.

Waamini wajibidishe kutafuta haki jamii kwa wale wanaoikosa kwa kuzingatia kwanza kabisa: uhakika wa usalama wa chakula, masuala ya unyanyasaji na dhuluma za kijinsia; kutetea haki katika masuala ya mishahara bila kusahau kusimama kidete kulinda na kudumisha haki za watoto. Waamini wajenge uhusiano mwema na vyombo vya ulinzi na usalama. Mwaka wa Imani iwe ni fursa kwa waamini kujibidisha kujenga na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa uchaji na Ibada.

Waamini waguswe na mahangaiko ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, wafungwa, wagonjwa, wahamiaji na wakimbizi. Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2013 uwe ni muda uliokubalika wa kufanya toba, wongofu wa ndani na kuchuchumilia utakatifu wa maisha; kwa kujikita katika mchakato wa upatanisho na msamaha wa kweli kati ya watu binafsi, familia na Jamii katika ujumla wake.








All the contents on this site are copyrighted ©.