2013-02-05 08:57:37

Magereza yanapaswa kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu miongoni mwa wafungwa


Kardinali Jorge Urosa Savino wa Jimbo kuu la Caracas anasema, Serikali inapaswa kutambua kwamba, magereza si makaburi ya wafungwa bali ni mahali ambapo wafungwa wanapewa fursa ya kuweza kujirekebisha kwa kutumikia vifungo vyao na baada ya hapo kuweza kurudi tena katika Jamii ili kuendelea na maisha yao kama kawaida, wakiwa watu wema.

Kardinali Savino ameyasema hayo kutokana na vurugu zilizotokea hivi karibuni kati ya Wafungwa na Askari Magereza, hali iliyopelekea zaidi ya wafungwa 58 kupoteza maisha na wengine zaidi ya 90 kupata majeraha makubwa. Viongozi wa Serikali wanao wajibu wa kuhakikisha kwamba magereza yanakuwa salama si tu kwa wafungwa wanaotumikia vifungo vyao hata kwa Askari Magereza wanaotoa huduma muhimu kwa ajili ya Wafungwa hao.

Ulinzi, usalama na maisha ya watu ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa, ili kupunguza vitendo vinavyopelekea baadhi ya wananchi kujikuta wakiwa Magerezani. Bila kuimarisha misingi hii ndani ya Jamii, Serikali zitajikuta zikiwajibika kujenga na kupanua Magereza kila mwaka. Magereza yawe ni sehemu ambayo inaheshimu utu na haki msingi za binadamu, lakini ukweli wa mambo ni kinyume kabisa na kile ambacho Jumuiya ya Kimataifa inatarajia kutoka katika Magereza.

Itakumbukwa kwamba, nia za Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa mwezi Januari ziligusia kwa namna ya pekee hali ya wafungwa Magerezani, akanonesha mshikamano na watu hawa. Kardinali Jorge Urosa Savino kwa upande wake, anapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na wafungwa wa kisiasa ambao wanaendelea kusota Magerezani pasi na sababu msingi.







All the contents on this site are copyrighted ©.