Hali ya amani na usalama inaanza kurejea kidogo nchini Mali, lakini bado kuna dharura
zinazopaswa kufanyiwa kazi!
Baraza la Maaskofu Katoliki Mali linasema kwamba, hali ya usalama nchini humo inaendelea
kuwa shwari kidogo, lakini kwa sasa tatizo ni huduma kwa watu wasiokuwa na makazi,
waliolazimika kuyakimbia makazi yao ili kusalimisha maisha yao kutoka Kaskazini mwa
nchi ambako Vikosi vya ulinzi na usalama vya Ufaransa vinapambana na majeshi ya waasi
nchini Mali.
Rais Francois Hollande hivi karibuni ametembelea mji wa Timbuktu
na kupokelewa na maelfu ya wananchi wa Mali waliokuwa wanamshangilia kutokana na uamuzi
wa nchi yake kusaidia harakati za kupambana na vikosi vya waasi vilivyokuwa vinatishia
amani na usalama Kaskazini mwa Afrika, kutokana na kujihusisha pia na vitendo vya
kigaidi.
Licha ya mafanikio yaliyokwisha kupatikana, lakini bado Mali inakabiliwa
na hali ngumu ya maisha, kwani bado wananchi wengi wanahofia usalama wa maisha yao
na kwamba, gharama ya maisha imepanda sana, ikilinganishwa na hali ya maisha ya wananchi
wa Mali. Bado watu wanahitaji huduma ya afya, malazi, chakula na maji safi na salama.
Kutokana na changamoto hii, Askofu Georges Fonghoro wa Jimbo la Mopti, amewaomba
Wasamaria wema, kuchangia kwa hali na mali ili kuokoa maisha ya wananchi wanaoendelea
kuteseka kutokana na mgogoro wa kivita nchini humo. Wananchi wengi hawana makazi na
wanaoteseka zaidi ni wanawake na watoto. Bado wananchi wanaona wasi wasi wa kurudi
katika maeneo yao ili kuendelea na maisha kama kawaida!