2013-02-04 12:34:08

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inaadhimisha Miaka 45 tangu ilipoanzishwa; matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican


Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia anatarajiwa tarehe 7 Februari 2013, Majira ya Jioni kuongoza Ibada ya Misa Takatifu itakayofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, kama sehemu ya maadhimisho ya Miaka 45 tangu Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ilipoanzishwa; matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ambao Mama Kanisa anaendelea kusherehekea Jubilee yake ya miaka 50, sanjari na Mwaka wa Imani, uliotangazwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.
Kuanzia tarehe 6 hadi 9 Februari 2013, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio itakuwa na Mkutano wake wa Mwaka, unaoongoza na kauli mbiu “Wakristo na Viongozi wa Kanisa kwa Siku za Usoni”. Mkutano huu unafanyika mjini Roma na kuwashirikisha Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Hii ni Jumuiya ambayo inajikita zaidi katika maisha ya: Sala na Tafakari ya Neno la Mungu; Upendo na Mshikamano na Maskini na Wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; Majadiliano ya kidini na kiekumene; ili kujenga dunia inayosimikwa katika haki, amani, upendo na maendeleo ya kweli. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio imekuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea ut una heshima ya kila binadamu, kwa kutetea utamaduni wa maisha dhidi ya utamaduni wa kifo unaoendelea kushika kasi sehemu mbali mbali za dunia.
Ni Jumuiya ambayo imesimama kidete kuanzisha Kampeni dhidi ya Adhabu ya Kifo duniani pamoja na kusaidia juhudi za mchakato wa upatanisho miongoni mwa mataifa yaliyojikuta yakielemewa na vita ya wenyewe kwa wenyewe kama ilivyotokea Msumbiji na nchi kadhaa za Kiafrika.
Mradi wa “The Dream” unaopania kutoa dawa za kurefusha maisha sanjari na kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto unaonesha mafanikio makubwa Barani Afrika. Hadi kufikia Desemba 2012, jumla ya watoto 20,000 walizaliwa bila ya kuwa na virusi vya ugonjwa wa Ukimwi. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inakuwa na kizazi ambacho hakuna virusi vya Ukimwi.
Mradi huu pia unawajengea uwezo wa kiuchumi waathirika wa Virusi vya Ukimwi, ili kujitegemea na kuzisaidia familia zao kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa. “The Dream” utaendelea kuonesha maajabu katika mapambano dhidi ya Ukimwi, ikiwa kama Serikali, Mashirika na Wafadhili binafsi, wataendelea kushikamana na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio katika kutekeleza Malengo na Mikakati yake ya Maendeleo.







All the contents on this site are copyrighted ©.