Juhudi za Kanisa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi katika Kipindi cha Miaka
30 iliyopita!
Miaka 30 imekwishagota, tangu wataalam walipogundua Virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi duniani,
janga ambalo limepelekea watu wengi hususan vijana ambao ni nguvu kazi ya mataifa
mengi kujikuta wakipoteza maisha wangali vijana wabichi. Katika harakati hizi, Kanisa
Katoliki limekuwa mstari wa mbele si tu kwa kutoa faraja kwa waathirika wa Ukimwi
bali pia kutoa dawa za kurefusha maisha pamoja na ushauri nasaha unaogusa maisha ya
mtu mzima: kiroho na kimwili.
Hivi karibuni, Shirika la Wayesuit linalojishughulisha
na Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa UKIMWI, AJAN kwa kushirikiana na Shirika la Mabinti
wa Mtakatifu Paulo, wamechapisha Kitabu kuhusu UKIMWI; kwa kujikita katika tafakari
za kiimani juu ya janga la Ukimwi Barani Afrika. Kitabu hiki ni jitihada za makusudi
katika mchakato wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi Barani Afrika.
Kitabu
hiki kinawahusisha wasomi, wadau na wanaharakati katika mapambano dhidi ya baa la
ugonjwa wa Ukimwi. Kinauangalia ugonjwa huu katika medani mbali mbali za maisha, daima
utu na heshima ya binadamu ikipewa kipaumbele cha kwanza. Utangulizi umeandikwa na
Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa jimbo kuu la Abuja, Nigeria, anayepongeza
juhudi na kazi kubwa iliyofanywa na waandishi wa kitabu hiki katika kuufahamu ukweli
wa ugonjwa wa Ukimwi Barani Afrika na mchango unaotolewa na Kanisa Katoliki katika
mapambano haya.
Kardinali Onaiyekan anasema, hiki ni kitabu ambacho kinagusa
mahusiano msingi ya kijamii na kiuchumi; utamaduni, haki msingi za binadamu; maadili
na utu wema. Kanisa linashiriki kikamilifu katika mapambano haya kwa kutoa nadharia
pamoja na utekelezaji wake katika uhalisia wa maisha ya watu, kwani itakumbukwa kwamba,
Kanisa Katoliki ni kati ya wadau wakubwa wanaowahudumiwa waathirika wa ugonjwa wa
Ukimwi sehemu mbali mbali Barani Afrika. Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Jumuiya
ya Kimataifa anasema Kardinali Onaiyekani ni elimu makini itakayosaidia mchakato wa
mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi.
Elimu hii inapaswa
kujikita kwa namna ya pekee katika haki msingi za binadamu, maadili na utu wema bila
kusahau kubainisha mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya kuwasaidia waathirika
wa ugonjwa wa Ukimwi. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, baada ya kifo kuna maisha ya
uzima wa milele, Kardinali John Onaiyekani, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja anasema
kwamba, mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, baado yanaendelea na kamwe watu wasibweteke,
kwani wanaweza kukiona kile kilichomnyoa kanga manyoya!