2013-02-04 10:17:36

Bado kuna wanawake wengi wanaopoteza maisha yao kutokana na ujauzito nchini Ethiopia!


Licha ya maboresho katika huduma kwa mama na mtoto sehemu mbali mbali za dunia, lakini, kuna wanawake wapatao 25,000 wanaopoteza maisha yao kutokana na matatizo ya uzazi na wengine zaidi ya 500,000 wanakabiliana na matatizo makubwa kutokana na masuala ya ujauzito nchini Ethiopia.

Hizi ni takwimu ambazo zimetolewa hivi karibuni na Mfuko wa Umoja wa Mataifa unaohudumia Idadi ya Watu, (UNFPA) baada ya kuchapisha utafiti uliofanyika nchini humo kunako mwaka 2010. Ethiopia ni kati ya nchi tano duniani zinazoongoza kutokana na idadi kubwa ya vifo vya wanawake, kabla, wakati na baada ya kujifungua.

Utafiti unaonesha kwamba, vifo vingi vinasababishwa na wanawake wa Ethiopia kushinikizwa kutoa mimba; kuharibika kwa mimba, kutokana na sababu mbali mbali pamoja na kuvuja damu kwa muda mrefu mara baada ya kujifungua pamoja na kukosa huduma ya tiba kwa karibu zaidi. Serikali ya Ethiopia inaendelea kuwekeza katika huduma ya afya kwa Mama na mwana; kwa kufanya maboresho katika vituo vya afya.

Hadi sasa takwimu zinabaianisha kwamba, ni asilimia moja tu ya wanawake nchini Ethiopia wanaojifungua kwa kupata msaada kutoka kwa Madaktari ambao kila mmoja anahudumia watu zaidi ya 2500. Hali hii ni mbaya zaidi kwa wanawake wajawazito wanaoishi Vijijini, kwani takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 50% ya wanawake wajawazito wanafariki dunia kutokana na kukosa huduma ya usafiri wa uhakika kwenda kwenye vituo vya afya.







All the contents on this site are copyrighted ©.