Yaliyojiri kwenye maadhimisho ya Siku ya XVII ya Watawa Duniani kwa Mwaka 2013
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Kutolewa
Bwana Hekaluni, hapo Jumamosi, tarehe 2 Februari, 2013 ameadhimisha Ibada ya Misa
Taikatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Ibada ambayo imepamba
kwa uwepo wa umati mkubwa wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume. Kwa mara ya
kwanza, Siku ya Watawa Duniani, iliadhimishwa kunako mwaka 1997, kama sehemu ya mchakato
unaopania kuhamasisha miito ya kitawa ndani ya Kanisa, kama cheche ya utakatifu wa
maisha, changamoto na mwaliko kwa kila mwamini. Siku hii inapania pamoja na mambo
mengine, kumshukuru Mungu kwa ushuhuda wa maisha na huduma inayotolewa na Watawa sehemu
mbali mbali za dunia, kwa kuishi Mashauri ya Kiinjili, yaani: Utii, Ufukara na Usafi
wa Moyo. Mara ya mwisho kwa Baba Mtakatifu kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na
Watawa wa Mashirika mbali mbali, ilikuwa ni mwaka 2006. Mara nyingine zote, Baba Mtakatifu
amekuwa akiadhimisha Siku kuu hii kwa njia ya Masifu ya Jioni. Ibada ya Misa Takatifu
kwa Mwaka 2013 imeanza kwa maandamano ya Watawa 50 kutoka Mashirika mbali mbali ya
Kitawa na Kazi za Kitume, kielelezo cha karama mbali mbali zinazojionesha ndani ya
Kanisa kama zawadi ya Roho Mtakatifu. Katika Maandamano haya, Wakuu mbali mbali
wa Mashirika wameshiriki pia, huku wakiwa wamebeba mikononi mwao mishumaa inayowaka,
kielelezo cha Kristo Mwanga wa Mataifa na changamoto kwa Watawa wenyewe kuwa kweli
ni mwanga kati ya watu wanaowahudumia. Kwa njia ya ushuhuda wao makini, watawa pia
wanaweza kuendeleza mwanga wa Kristo unaookoa walimwengu.