2013-02-02 07:54:47

Siku ya kuenzi zawadi ya uhai nchini Italia


Maadhimisho ya Siku ya Saba ya Familia Kimataifa, yaliyofanyika Jimbo kuu la Milano kuanzia tarehe Mosi hadi tarehe 3 Juni 2012, ilikuwa ni fursa ya pekee kusikiliza shuhuda mbali mbali zilizokuwa zinatolewa na Familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia, jinsi ambavyo wanavyokabiliana na changamoto mbali mbali katika utekelezaji wa dhamana na utume wao katika maisha ya Kifamilia, mintarafu Mafundisho ya Kanisa. RealAudioMP3

Familia ni kati ya taasisi nyeti zinazokabiliwa na changamoto mbali mbali katika ulimwengu huu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, familia nyingi zimetikiswa na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, kiasi hata cha kutishia maisha na ustawi wa familia kadiri ya Mafundisho ya Kanisa. Watu wengi ndani ya Familia wamekata tamaa, hawana matumaini ya kusonga mbele kutokana na vikwazo mbali mbali vilivyoko mbele yao.

Athari za myumbo wa uchumi kimataifa zimepelekea hata wanandoa kuwa na mtazamo tofauti kabisa kuhusu zawadi ya maisha, uhusiano kati yao na wakati mwingine wamejikuta wakichukua maamuzi machungu kinyume kabisa cha wito na dhamana yao katika Kanisa na Jamii kwa ujumla. Lakini, ikumbukwe kwamba, ni katika Familia inayoundwa na upendo wa dhati kati ya Bwana na Bibi, humo ndiko mahali panapochipuka na kukomaa zawadi ya maisha.

Baadhi ya nchi za Ulaya zimeendelea kukumbatia utamaduni wa kifo kiasi kwamba, hata sera na maamuzi kuhusu familia nazo zimekuwa tenge. Hali hii inajionesha kwa namna ya pekee kabisa kutokana na ongezeko kubwa la watu wenye umri mkubwa wanaohitaji kutunzwa na Jamii sanjari na idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa katika nchi za Ulaya.

Ni katika mwono huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, katika Maadhimisho ya Siku ya Maisha Kitaifa, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo hapo tarehe 3 Februari, wanaialika kwa namna ya pekee, Familia ya Mungu nchini Italia kusimama kidete kupinga sera zinazokumbatia utamaduni wa kifo kwa kisingizio cha kutaka kudhibiti athari za myumbo wa uchumi kimataifa.

Maadhimisho ya Siku ya Maisha Kitaifa kwa Mwaka 2013, yanaongozwa na kauli mbiu “endelezeni zawadi ya maisha ili kushinda athari za myumbo wa uchumi”. Ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, yanayosimikwa katika zawadi ya maisha. Wanandoa wanaalikwa kutambua, kuthamini na kuenzi zawadi ya maisha, pamoja na kudumisha uhusiano wa dhati ndani ya familia, kwa ndugu na jamaa wanaowazunguka.

Wanandoa wanapaswa kutambua kwamba, wanasukumwa na upendo wa Kristo kujenga na kuimarisha uhusiano mwema na jirani zao; kwa kujifunza kutoa sadaka hata ile ndogo kabisa katika safari ya maisha yao ya kila siku. Familia zijifunze utamaduni wa kugawana na wengine kile ambacho wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu. Familia ambazo zimekumbwa na majanga asilia, zimeonja na kumegeana ukarimu na upendo, kama kielelezo cha upendo wa Mungu unaobubujika kwa wote, ndivyo Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alivyowaambia Wanafamilia waliokuwa wanahudhuria Maadhimisho ya Siku ya Saba ya Familia Kimataifa, huko Milano.

Mambo haya yanaonesha jinsi ambavyo utu na heshima ya mwanadamu vinapaswa kuthaminiwa na kulindwa tangu pale mtoto anapotungwa tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Athari za myumbo wa uchumi kimataifa, kisiwe ni kisingizio cha kutaka kukumbatia utamaduni wa kifo, badala yake, watu waonjeshane fadhila ya upendo na ukarimu, daima wakisimama kidete kujenga utamaduni wa maisha, kwa vitendo, kwani maneno matupu, kamwe hayawezi kuvunja mfupa!

Maaskofu wanasema, maisha ni zawadi ambayo inawachangamotisha wanafamilia kwanza kabisa kuihuisha, kuipenda na kuiendeleza, kama kikolezo cha kufufua na kuenzi mchakato na sera zinazopania kufufua uchumi. Vijana wajengewe utamaduni wa kupenda na kuheshimu maisha na kwamba, kudhibiti uzazi pamoja na kukumbatia utamduni wa kifo, si suluhu ya kuondokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa.

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Italia, wanahamasihwa kupenda na kuheshimu zawadi ya uhai, mwaliko kwa wanasiasa pia kuwekeza zaidi katika maisha ya watu pamoja na kutunga sera na mikakati inayoheshimu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Maaskofu wanaamini kwamba, kwa kukumbatia zawadi ya uhai, taifa linaweza kukabiliana uso kwa uso na athari za myumbo wa uchumi kimataifa.








All the contents on this site are copyrighted ©.