2013-02-02 19:25:09

Maisha ya watawa yawe ni Habari Njema inayomwilishwa na kutangazwa; maisha yanayong'ara kama Neno la Ukweli


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni inayoadhimishwa kila Mwaka ifikapo tarehe 2 Februari, sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 17 ya Watawa Duniani kwa Mwaka 2013 amepembua kwa ustadi mkubwa Simulizi la Utoto wa Yesu kadiri ya Injili ya Mtakatifu Luka. Familia Takatifu ya Yesu Maria na Yosefu ilikuwa ni maskini; watu wa kawaida kabisa lakini wachamungu na watu waliokuwa tayari kutekeleza Sheria kadiri ya Torati.

Kutolewa kwa Bwana Hekaluni anasema Baba Mtakatifu linakuwa ni tukio la pekee kabisa kwani, Mwana wa Mungu anaingia ili kulitakatifuza Hekalu na Waamini wanaolitumia. Yesu ndiye Kuhani mkuu na Mwanakondoo wa Mungu atakeyetolewa sadaka: kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, ili kuweka Agano Jipya na la Milele kati ya Mungu na binadamu. Kristo ndiye Mkombozi wa ulimwengu anayekuja kuwashirikisha wanadamu upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka.

Ni utimilifu wa unabii uliotolewa kwenye Maandiko Matakatifu, kama wanavyoshuhudia Mzee Simeoni na Anna. Ndiye mwanga unaowaangazia watu wake Israeli. Ndiyo mwanga uliokuwa umebebwa na Wakuu wa Mashirika katika Maadhimisho ya Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni.

Katika Mwaka wa Imani, Baba Mtakatifu anawaalika Watawa kutambua kwamba, ni mahujaji wanaotembea na Kanisa ili kuweza kuimarishwa katika imani, ili kujitoa kikamilifu kwa Mungu na Kanisa. Anawashukuru watawa wa mashirika na karama mbali mbali ndani ya Kanisa kwa uwepo na utume wao ndani ya Kanisa na Ulimwengu kwa ujumla.

Maisha yao yawe ni changamoto ya kuingia katika mlango wa Imani ambao daima uko wazi, ili kuweza kurutubisha wito na mapendo yao kwa Kristo. Wajifunze ukimya wakati wa kuabudu, ili kuweza kuwashirikisha wengine utii katika imani, ufukara katika mapendo na usafi kamili kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani.

Imani iwasaidie kutambua hekima inayojionesha katika udhaifu pamoja na Fumbo la Msalaba, wakitambua kwamba, katika udhaifu wao wa kimwili, wanachangamotishwa kumuiga Kristo ili waweze kufanana naye, daima wakijitahidi kuwa ni sauti ya wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii inayotafuta kwa udi na uvumba: tija na ufanisi.

Baba Mtakatifu anawaalika watawa kuuisha imani yao ili kuendeleza hija ya maisha ya baadaye inayotafuta sura ya Kristo. Hali hii ijioneshe katika kila hatua na wakati wa kufanya maamuzi mazito ya maisha. Watawa wajitahidi kujivika silaha za mwanga, wakiwa makini na kuendelea kukesha, ili kwa njia ya huruma na neema yake, waendelee kuwa ni waaminifu kwa Kristo mwenyewe.

Maisha yao kama Watawa yanawashirikisha pia lile Fumbo la Msalaba kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, ambaye moyo wake ulichomwa kwa upendo wa Mungu. Mateso na magumu wanayokumbana nayo ni mwanga katika azma ya uinjilishaji wa watu.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika mahubiri yake, anawataka watawa kuhakikisha kwamba, maisha yao yanakuwa ni Habari Njema iliyomwilishwa na kutangazwa; maisha yanayong'ara kama Neno la Ukweli.







All the contents on this site are copyrighted ©.