2013-02-02 07:32:24

Kwaresima 2013: "Kuamini katika upendo kunaamsha upendo; tumelifahamu na kuliamini pendo la Mungu lililoko ndani mwetu"


Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki Cor Unum akizungumza na waandishi wa habari anasema, ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2013 unaoongoza na kauli mbiu “Kuamini katika upendo kunaamsha upendo; tumelifahamu na kuliamini pendo la Mungu lililoko ndani mwetu”.
Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika waamini kwa namna ya pekee kufanya tafakari ya kina, ili kuona uhusiano uliopo kati ya fadhila za kimungu yaani: imani na upendo. Hii ni imani ambayo imefunuliwa kwa mwanadamu kwa njia ya yesu Kristo na upendo ni karama ya Roho Mtakatifu inayomchangamotisha mwamini kumpenda Mungu na Jirani.
Hii ni imani tendaji inayomwilishwa katika medani mbali mbali za maisha, ili kuweza kuzima kiu na njaa ya watu wanaomtafuta Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Ni imani inayomsaidia mwanadamu kutambua utu na heshima yake, kwa vile ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, imani bila matendo hiyo imekufa ndani mwake.
Imani inapaswa kumchangamotisha mwamini kuitolea ushuhuda katika matendo, ndiyo maana Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yanapaswa kuwa ni kielelezo cha mshikamano wa upendo na imani na kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Hiki ni kielelezo cha juu kabisa cha upendo wa Kristo kwa binadamu, hivyo ni jukumu na dhamana ya waamini kuhakikisha kwamba, wanaiishi imani hii katika ukamilifu wake.
Kardinali Sarah anasema kwamba, kwa njia ya Sadaka ya Kristo, kila mwamini anatambua wito na utume wake, kiasi cvha kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya mafao ya jirani yake, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kwaresima ni kipindi cha matendo ya huruma kwa jirani na mwaliko wa kugawana na wengine karama na mapaji ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake.
Kuna haja kuwa makini na aina mbali mbali za umaskini zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo kutokana na majanga asilia, athari za mabadiliko ya tabianchi, vita na migogoro na kinzani za kijamii pamoja na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Mambo yote haya yanaendelea kumtumbukiza mwanadamu katika shida na mahangaiko ya roho na mwili.
Familia nyingi zimejikuta zinaogelea katika umaskini wa hali na kipato; vijana wengi hawana fursa za ajira hata kama wanazo sifa na kiwango cha elimu kinachotakiwa. Katika shida na mahangaiko kama haya sehemu mbali mbali za dunia, kuna baadhi ya watu wanaotaka kuneemeka na matatizo ya watu, kiasi hata cha kudharirisha utu na heshima ya binadamu.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anaendelea kukazia kwamba, imani na upendo ni chanda na pete, kamwe haviwezi kutenganishwa. Imani inajionesha kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, inayoangalia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; mtu ambaye Kristo amempenda, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake, ili aweze kumkomboa kutoka katika dhambi na mauti!
Kanisa linaendelea kujenga ufalme wa Mungu kwa njia ya huduma ya upendo, ili kuzima kiu na njaa ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Kanisa halina budi kusimama kidete kutangaza Kweli za Kiinjili, kulinda na kutetea utu, heshima na maisha ya kila mtu! Liamshe dhamiri zilizokufa, ili ziuone ukweli na kuukumbatia.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika ujumbe wake kwa Kwaresima ya Mwaka 2013 anabainisha kwamba, dhamana kubwa ambayo Kanisa linatumwa kuitekeleza ni kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha matendo ya upendo. Hii ndiyo huduma ya Neno la Mungu, changamoto kwa waamini kumegeana Mkate wa Neno la Mungu pamoja na kumwezesha mwamini kujenga uhusiano wa dhati na Mwenyezi Mungu, bila kusahau mikakati ya shughuli za kichungaji, inayopania kumwendeleza mwanadamu: kiroho na kimwili.
Upendo wa Kristo unawawajibisha waamini kuwamegea jirani zao utajiri huu unaopata chimbuko lake kutoka kwa Mungu mwenyewe. Itakumbukwa kwamba, huduma ya upendo na mshikamano ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani iwe ni changamoto kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kumwilisha imani katika matendo, kama kielelezo cha waamini kujishikamanisha na Kristo. Waamini waoneshe moyo wa ukarimu na upendo kwa jirani zao na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawachangamotisha waamini katika Kipindi cha Kwaresima, kujenga Utamaduni wa Imani na Mapendo. Anawatakia wote maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima, Kanisa linapoendelea kusherehekea Mwaka wa Imani.








All the contents on this site are copyrighted ©.