Kanisa Katoliki litaendelea kuwekeza katika Katekesi na Elimu ya dini shuleni ili
kujenga taifa la watu wenye nidhamu, maadili na utu wema!
Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya, Tanzania, ametoa ufafanuzi wa tamko
la Jukwaa la Wakristo kuhusu suala la kuchoka kutukanwa na kuonewa siyo dhana ya kulipiza
kisasi bali ni kuwa watu wa sala na kitubio na ikiwezekana kukaa na kuzungumza na
wanaojenga chuki na kufanya uharibifu wa mali ya watu na serikali.
Askofu
Chengula ametoa ufafanuzi huo katika semina ya Makatekista na Walimu wa dini iliyofanyika
katika ukumbi wa vijana jijini hapa ambao walitaka kujuwa ukimya huo utadumu hadi
lini hali wanachokozwa, wanatishiwa maisha na vitu kuharibiwa.
Amesema amesema
licha ya kanisa kutukanwa,kuchokozwa na kuharibiwa na hata kufikia ya kuanza kupigwa
risasi halitajibu zaidi ya kuendelea kusali rozali takatifu,kufanya kitubio na kuendelea
kufunga ili kushinda majaribu hayo yasiyompendeza mwenyezi mungu."Kanisa Katoliki
limetukanwa sana, limefanyiwa uchokozi na uharibifu mkubwa na sasa wameanza kutupiga
na bunduki, huku vikitolewa vitisho vya kuuawa Mapadre na Maaskofu wazi wazi, lakini
tunaposema limechoka kutukanwa msibebe bunduki bali muwe watu wa sala na kuwaombea
wanaofanya hayo ili watubu na kumrudia Mwenyezi Mungu,"alisema.
Aliongeza"muwe
watu wa sala, mapatano na wakakamavu, tusali Rozali katika nyumba zetu, tufanye kitubio
na tuwe watu wa kufunga na tumshinde shetani hiyo ndiyo silaha pekee na ikibidi kutokana
na kuchoka huku tuwe tayari kuzungumza na hao wanaotuchokoza, tujimwagie majivu na
kusali." Aidha Askofu Chengula ametoa ushauri kwa Serikali na Mamlaka husika kutoruhusu
kujengwa nyumba za starehe karibu na vyuo ama shule kwani ndiyo chanzo kikubwa cha
ongezeko la vitendo vya kikatili vya utoaji wa mimba na kuuwa watoto wanaokotwa katika
madampo ya taka katika vyuo na mashule.
Amesema haiwezekani kuchanganya elimu
na starehe kwani kitendo cvha kujenga nyumba za starehe jirani na vyuo kunamjengea
mazingira magumu ya ushawishi mwanafunzi na ndiyo matokeo ya kushindwa kuendelea kimasomo
ama mwendelezo wa kuokotwa watoto katika madampo. "Pale Iringa katika chuo kikuu cha
Rouco wamefaulu kwani kuna muda walitaka kujenga majengo ya aina hiyo lakini Mungu
alisikia vilio vya watu wake na sasa pako salama na Mbeya ili vitendo vipunguwe na
kumalizika na watoto waweze kusoma kwa usalama hayo maeneo yaondolewe," amesema.
Hata
hivyo amewaagiza Mapadre, Watawa wa Kike na Kiume, Makatekista na Walimu wa dini kuongeza
jitihada za dhati kuwatembelea mara kwa mara wanafunzi na wanachuo kuwapatia ushauri
licha ya kuendeela kutoa mafundisho ya dini ili waweze kufuata maadili mema.
Katika
semina hiyo mambo mbalimbali yamezungumzwa kuhusu muhtasari wa mafundisho ya dini
kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu ambapo Katibu Mtendaji wa Idara ya Katekesi
kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania Padri Raphael Madinda alitoa mada kuhusu umuhimu
na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuridhia kuingizwa katika mtaala wa elimu
nchini. Padri Madinda alisema mmong’onyoko wa maadili na kuibuka kwa vurugu, migomo
na migogoro mbalimbali hata kusababisha maandamano mashuleni chanzo kikubwa ni ukosefu
wa mafundisho ya dini ambayo yanamjenga mwanafunzi kumuogopa Mungu na kuishi kwa kufuata:
sheria za nchi, maadili na utu wema.
Ametoa wito kwa waamini wa Kanisa Katoliki
kujitokeza kwa wingi kutoa mafundisho ya dini kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya awali,
msingi, sekondari,v yuo na vyuo vikuu ili jamii iweze kurejea katika maisha ya upendo,
amani, tulivu, upatanisho, haki na kuvumiliana; mambo ambayo yanaendelea kuporomoka
kwa kasi ya ajabu nchini Tanzania.
Katika Semina hiyo Padri Innocent Sanga
amesema changamoto kubwa wanayokabiliana ni ukata katika kuwawezesha walimu na makatekista
kufundisha katika shule mbalimbali kwani Jiografia ya maeneo ya Mkoa wa Mbeya ina
milima na mabonde na shule kujengwa umbali mrefu unaohitaji vyombo vya usafiri sanjari
na fedha za kujikimu jambo ambalo wanaendelea kulitafutia ufumbuzi wakati wakiendelea
kujitoa.
"Kwa kweli walimu na makatekista wanatoa huduma za kufundisha mashuleni
katika mazingira magumu,kuna maeneo yana umbali mrefu lakini wanajituma kutembea,tunawapongeza
sana lakini pia tunawashukuru mapadri na masista kwa kuendelea kuonyesha mfano kwa
kuendelea kufundisha,"amesema.
Hata hivyo Askofu Chengula wakati akigawa vitabu
vya muhtasari wa Mafundisho ya dini mashuleni amewapongeza Mapadri kwa kuendelea kutoa
mafundisho ya dini kwani hilo ndilo jukumu kubwa la Kanisa kufundisha Katekesimu,
Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti sanjari na huduma nyingine za kiroho na kimwili.