2013-02-01 08:45:04

Watawa ni mashahidi na watangazaji wa Imani


Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni kila mwaka ifikapo tarehe 2 Februari sanjari na Siku ya Watawa Duniani, iliyoanzishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, yapata miaka kumi na saba iliyopita. RealAudioMP3

Watawa ni mashahidi na watangazaji wa Imani, ndiyo kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Siku yak umi na saba ya Watawa Duniani kwa Mwaka 2013 sanjari na Mwaka wa Imani, kama ulivyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia.

Ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Kristo, Mkombozi wa Ulimwengu. Kwa njia ya Kristo Mwenyezi Mungu ameonesha upendo mkuu na kwa njia ya Ubatizo, wakawekwa wakfu ili kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani. Kwa njia ya Kristo watawa wanaendelea kupata chemchemi ya furaha ya kuwa ni wafuasi wa Kristo na mashahidi wa imani. Watawa katika miundo mbali mbali ya maisha yao wanawekwa wakfu kwa namna ya pekee kwa ajili ya kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Mama Kanisa anatambua na kuheshimu mchango wa watawa katika maisha na utume wa Kanisa.

Katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu, Mama Kanisa anawachangamotisha watoto wake na watawa kwa namna ya pekee, kujitoa kimaso maso kwa ajili ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza Imani ya Kikristo kwa ujasiri, utulivu na uthabiti wa moyo kwa wote, lakini kwa namna ya pekee kwa vijana wa kizazi kipya. Ni changamoto ya kutangaza na kutolea ushuhuda misingi mikuu ya imani, katika medani mbali mbali za maisha.

Watawa wanaweza kutekeleza wajibu huu kwa umakini na furaha ya kweli, kwa kuanzia ndani ya familia; kitovu cha utakatifu na maisha ya kuwekwa wakfu. Watawa ni mashahidi wa imani inayojionesha katika nadhiri zao yaani: utii, ufukara na usafi kamili.

Watawa wanatekeleza dhamana hii nyeti katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya: Katekesi, majiundo makini ya Kikristo; huduma katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu ya mtu mzima: kiroho na kimwili; huduma kwa familia na vijana; wakimbizi na wahamiaji bila kusahau wajibu wao wa kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani, kama kielelezo makini cha mshikamano kati ya Kanisa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Maaskofu wanabainisha kwamba, ulimwengu mamboleo una kiu ya ushuhuda makini kutoka kwa Watawa wanaoonesha uaminifu na furaha ya kweli inayobubujika katika majitoleo yao yak ila siku, ili kwa njia yao, waweze kuonja uwepo wa Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Ni changamoto ya kuwa kweli waaminifu kwa Injili ya Kristo na Kanisa lake, kwa kutambua kwamba, Uinjilishaji Mpya unaanza katika maisha ya kila mtawa, anayehamasishwa kwanza kabisa kuwa msikivu wa Neno la Mungu, akijitahidi kila wakati kutubu na kumwongokea Mungu, hija ambayo inaonesha ile furaha ya maisha ya kuwekwa wakfu.

Watawa wanapaswa kuwa waaminifu kwa Karama ya Mashirika yao kama kielelezo cha zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa, kwa kuwa mitume waaminifu pamoja na kutambua dhamana na utume waliokabidhiwa na Mama Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Watawa wajitahidi kuonja maisha ya kibinadamu, kijamii na kitamaduni, katika maeneo ambayo wanatekeleza dhamana na wajibu wao wa kila siku, ili wale wanaowahudumia waweze nao kuonja uwepo wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wao wa kinabii, hata pale inapowabidi kutoa sadaka kubwa. Ni mwaliko wa kuendelea kuwa waaminifu kwa Mapokeo na Karama za Mashirika yao ya kitawa na kazi za kitume, ili yaweze kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, linawaalika watawa kwa namna ya pekee, kuwa ni mashahidi na watangazaji wa Imani kwa njia ya ubora wa maisha yao ya kiroho, kijumuiya na huduma makini kwa jirani na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Maisha ya kiroho yanarutubishwa kwa njia ya Tafakari ya Neno la Mungu; kwa kukutana na Kristo katika Sala, kwa kuteta na Kristo katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na kuonja upendo wa Kristo kwa njia ya Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu bila kusahau kujipatanisha na Mungu na Watawa wengine katika Sakramenti ya Upatanisho, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu.

Nadhiri za kitawa ni kielelezo makini cha muungano kati yao na Kristo, kwa kujitoa kimasomaso kupokea wito wao na kuutolea ushuhuda, huku wakiendelea kutegemea neema na baraka za Mungu. Maisha ya kijumuiya yawasaidie watawa kuonesha ujasiri, unyenyekevu na uvumilivu, daima wajikitahidi kujenga na kuimarisha uhusiano wao na Mwenyezi Mungu, ili walimwengu waweze kuamini.

Ni zawadi inayopaswa kumwilishwa kila siku ya maisha na kamwe wasikatishwe tamaa na vizingiti wanavyokumbana navyo katika hija ya maisha yao kama watawa!

Ubinafsi, mahusiano tenge, upweke hasi, kinzani na migawanyiko ni kati ya matatizo na magumu wanayoweza kukabiliana nayo watawa katika ulimwengu mamboleo, lakini watambue kwamba, wanaweza kuyashinda yote haya kwa kumtegemea Mungu.

Imani yao katika huduma ya upendo na mshikamano na maskini, wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni, inawawezesha kuwaonjesha wengine ile imani iliyomo ndani mwao.

Huduma kwa binadamu ni kielelezo makini cha uaminifu kwa Mungu na kama sehemu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu duniani. Hivi ndivyo Baraza la Maaskofu Katoliki linavyohitimisha Ujumbe wake kwa watawa wanapoadhimisha Siku ya Kumi na Saba ya Watawa Duniani kwa Mwaka 2013.









All the contents on this site are copyrighted ©.