2013-02-01 11:03:46

Wahamiaji kutoka Afrika wanaoishi Australia ni Familia ya Mungu inayowajibika barabara!


Ujumbe wa Maaskofu Katoliki kutoka Sudan ya Kusini, uliokuwa chini ya Askofu msaidizi Santo Loku Pio, hivi karibuni, ulifanya hija ya mshikamano wa imani nchini Australia, ili kuwaimarisha ndugu zao katika Kristo waliohamishiwa nchini humo na sasa wanaendelea na maisha yao kama waamini wa Kanisa Katoliki na raia wa Australia.

Hija hii ni kielelezo cha mshikamano uliooneshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Australia, kwa kuwaalika viongozi wa Kanisa kutoka Sudan ya Kusini, ili kwenda kuwaimarisha ndugu zao katika imani na uwajibikaji, wakitekeleza wajibu na majukumu yao kwa weledi na majitoleo makubwa.

Askofu msaidizi Santo anasema, amefurahia kuona na kusikia kwamba, Wahamiaji hao ambao wengi wao ni kutoka Sudan ya Kusini, wanashiriki katika maisha na utume wa Kanisa nchini Australia kama Makatekista, Mashemasi wa Kudumu na kwamba, kuna baadhi ya Mapadre kutoka Barani Afrika wanaowahudumia ndugu zao katika imani. Ili kutekeleza dhamana na wajibu huu, Kanisa Katoliki nchini Australia limewekeza maradufu katika majiundo ya awali na endelevu na sasa wanachapa kazi barabara!

Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linasema kwamba, kuna Waamini wengi kutoka Barani Afrika hasa zaidi kutoka katika nchi za DRC. Uganda, Rwanda, Burundi, Kenya na Tanzania. Kwa pamoja wanaunda Familia ya Mungu inayowajibika. Changamoto kwa waamini hawa ni kuendelea kuwajibika kikamilifu, daima wakijitahidi kuwa ni raia wema, waaminifu na wachapakazi; watu ambao wanafuata sheria na kanuni za wenyeji wao.







All the contents on this site are copyrighted ©.