2013-02-01 08:49:00

Siku ya Wagonjwa Duniani 2013: changamoto ya kuwa Wasamaria wema, kielelezo cha imani tendaji


Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, kuanzia mwaka 2013 litakuwa linachapisha vitini maalum kwa lugha mbali mbali, ili kuwawezesha waamini na watu wenye mapenzi mema kuweza kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Februari, sanjari na Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes. RealAudioMP3

Vitini hivi vitatolewa kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yatakayomba ili yaweze pia kuchapisha nakala kwa ajiliya Majimbo yao mintarafu ujumbe utakaokuwa umetolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa mwaka husika. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwamba, vitini hivi vitaweza kutumika kwa Mwaka mzima wa Liturujia ya Kanisa, ili kuwawezesha waamini kukua na kukomaa katika imani, sala na tafakari ya kina kutoka ndani ya Kanisa.

Vitini hivi vimegawanywa katika sehemu kuu tatu za Mwaka wa Liturujia ya Kanisa: yaani: Kipindi cha Majilio, Noel ina Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani inayofikia kilele chake kila mwaka tarehe 11 Februari kwa Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria wa Lourdes; Kwaresima pamoja na Kipindi cha Pasaka. Kutakuwa na Njia ya Msalaba ili kuwasaidia wagonjwa na wadau mbali mbali kuweza kutafakari kuhusu Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Ni maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Padre Augusto Chendi, Katibu mwambata, Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya 21 ya Wgonjwa Duniani inayofanyika kila mwaka ifikapo tarehe 11 Februari.

Baba Mtakatifu anapenda pia kuonesha uwepo wake wa karibu katika mahangaiko na mateso ya wagonjwa ndiyo maana amemtuma Askofu mkuu Zygmunt Zimowski kumwakilisha katika maadhimisho haya katika madhabau ya Bikira Maria wa Altotting, yaliyoko nchini Ujerumani. Lengo ni kuonesha moyo wa huruma na upendo kwa wagonjwa, dhamana inayoendelezwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake.

Ili kuwawezesha waamini kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatoa pia rehema kamili na za muda kwa waamini watakaotimiza masharti yanayotolewa na Mama Kanisa, yaani kwa kupokea Sakramenti ya Kitubio, Ekaristi Takatifu na Kusali kwa nia za Baba Mtakatifu. Rehema kamili na zile za muda zinatolewa kati ya tarehe 7 hadi tarehe 11 Februari 2013.

Padre Chendi anasema, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya 21 ya Wagonjwa Duniani anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni Wasamaria wema kwa jirani zao, kama kielelezo cha imani tendaji.








All the contents on this site are copyrighted ©.