Kuna zaidi ya watu billioni moja duniani wanaokabiliana na umaskini mkubwa. Dhana
ya umaskini imekuwa ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, lakini wakati mwingine umaskini
huu unasababishwa na binadamu mwenyewe kwa kuendekeza sera na uchumi unaotoa mwanya
kwa matajiri kuendelea kutajirika zaidi na maskini, akina yakhe pangu pakavu tia
mchuzi kuendelea kuogelea katika lindi la umaskini na utupu! Huu ndio ukweli utakaoendelea
kumwandama mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani.
Ni maneno
ya Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu Misaada ya Kanisa
Katoliki Cor Unum katika mahojiano na Radio Vatican kuhusiana na baa la umaskini duniani,
kampeni ambayo inaendeshwa kwa namna ya pekee na Shirikisho la Radio na Televisheni
Barani Ulaya.
Lakini umaskini pia unaweza kuangaliwa kwa jicho chanya, kwani
ni kielelezo cha mtu kuishi kwa kiasi, wakiwa na tabasamu na furaha ya kweli, badala
ya kuwa na mali nyingi lakini daima watu wanalala macho wazi kama bundi kwa hofu na
magonjwa yanayotokana na kuwa na mali nyingi kupita kiasi. Watu maskini wana imani
kubwa katika maisha; binadamu anapaswa kupata mahitaji yake msingi yanayozingatia
utu na heshima yake kama binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Kardinali
Sarah anabainisha kwamba, hata katika Agano la Kale, utajiri ulionesha baraka na neema
kutoka kwa Mungu. Kristo katika utume wake anabainisha kwamba, amekuja kuwatangazia
maskini Habari Njema ya Wokovu na kwamba, Heri Maskini maana Ufalme wa Mungu ni wao.
Kristo Mwana wa Mungu, amejifanya kuwa maskini, kiasi hata cha kuchukua ubinadamu
na kufanana na mwanadamu katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi.
Mababa
wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanaliasa Kanisa kuonesha ile sura ya umaskini.
Huu ni mwelekeo chanya kuhusu dhana ya umaskini ndani ya Kanisa, ambao kwa maneno
mengine unafahamika kama Nadhiri ya Ufukara, yaani kuwa na matumizi sahihi ya mali
na utajiri wa ulimwengu huu, kama wanavyofanya Watawa katika Mashirika yao! Ni matajiri
wa vitu, lakini wakarimu kwa njia ya mali waliyonayo kwa ajili ya maisha na utume
wa Kanisa. Lakini Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe anasema Kardinali
Robert Sarah ili kupambana na umaskini unaodhalilisha ut una heshima ya mwanadamu.
Huu
ndiyo utume na dhamana ambayo Mama Kanisa ameendelea kuitekeleza katika hija ya maisha
yake hapa duniani kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ut una heshima ya mwanadamu,
aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kanisa limeendelea kuwekeza katika huduma ya
afya kwa kuendeleza ile kazi ya Kristo Msamaria mwema, aliyemganga mwanadamu kwa kumondolea
magonjwa yake pamoja na dhambi zilizokuwa zinamsumbua moyoni mwake. Kanisa limeanzisha
shule katika ngazi mbali mbali ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la ujinga
na kumwezesha ili kupambana fika na hatimaye, kuweza kuboresha mazingira yake, ili
dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.
Kanisa linaendelea kuunga
mkono juhudi za wakulima, ili waweze kujinasua na baa la njaa na umaskini wa kipato,
kwa njia ya kilimo bora na kilimo kinachozingatia utunzaji bora wa mazingira pamoja
na matumizi sahihi ya pembejeo na teknolojia rafiki kwa mazingira, kama sehemu ya
mwendelezo wa mchakato wa utunzaji wa kazi ya uumbaji. Kanisa kwa huduma mbali mbali
limeendelea kutoa fursa za kazi na ajira ili kuboresha maisha ya watu kwa kutambua
kwamba, kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya mwanadamu. Mama Kanisa anasema Kardinali
Robert Sarah anapenda kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili.
Kanisa linaendelea
kuonesha mshikamano wa upendo kwa watu wanaoteseka kutokana na maafa asilia, vita,
kinzani na migogoro ya kisiasa na kijamii kama inavyojionesha huko Mashariki ya Kati
na sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa limekuwa ni alama ya matumaini na kimbilio
la wengi katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi, hasa sehemu za vijijini.
Kanisa linapenda kumfariji mtu katika mahangaiko yake kimwili na kiroho, ili aweze
kutambua kwamba, anapendwa na anathamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kumbe,
kuna haja kwa kila mtu katika hali yake kuhakikisha kwamba, anatunza na kudumisha
misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano. Binadamu ajifunze kutunza mazingira;
kuzingatia kanuni maadili kuhusu uchumi na fedha kwani myumbo wa uchumi kimataifa
unaoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini wa kipato ni matokeo ya kutozingatia
kanuni maadili katika mfumo wa fedha. Mungu na mwanadamu wapewe kipaumbele cha kwanza
katika mipango na sera za maendeleo endelevu.