2013-01-30 08:35:36

Wakristo wajitambue vema na kuonesha ushujaa katika kuihubiri Injili ya Kristo


Kila mmoja katika kuongoka kwake, kujifahamu na kuishi kadiri ya alivyoumbwa na kuitwa ni zoezi la kiroho na hatua kubwa katika kumfuasa Kristo. Hayo yamesemwa na Askofu Mkuu Yuda Thaddei Ruwa’ichi wa Jimbo Kuu la Mwanza, Tanzania, katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya kuongoka kwa Paulo Mtume. Katika adhimisho hilo lililofanyika katika Seminari Ndogo ya Mt. Maria, Nyegezi, aliwapatia pia Majandokasisi wawili daraja ya Ushemasi ambao ni: Theophilus Kumalija wa Parokia ya Mwabagole na Bernadin Mtula wa Parokia ya Sumve.
Askofu Mkuu Ruwai’cihi alioanisha maisha ya Mtume Paulo na Wakristo katika zama hizi ili waweze kuiga mfano wa mtume huyo. Mtume Paulo kadiri ya mapokeo, alikuwa mfupi wa kimo na mwenye umbo dogo. Hakuwa mnyonge kwa sababu hizo, bali alijikubali na kujisimamia kwa ujasiri bila kumangamanga. Naye alifundwa na kubobea katika sheria, chini ya Mwalimu maarufu, Gamalieli. Paulo akawa mkereketwa wa imani yake ya Kiyahudi na hivyo akawatesa hata kufa, Wakristo waliodhaniwa kupotosha imani ya Kiyahudi.
Ukereketwa na ujasiri huo ndio, Kristo anautumia na kumuongoa Paulo, anamfanya mfuasi wake na mhubiri hodari wa Habari Njema. Pauolo alikuwa tayari kusimulia habari za maisha yake ya awali ambayo kwa mwingine angeweza kujionea aibu na kuficha: ya kwamba: alikuwa mtesi na muuaji wa Wakristo. Maneno magumu na mazito namna hii yasiposimuliwa huelemea moyo na kumfanya mhusika kuwa na huzuni.
Kumbe, ni vizuri kushirikisha juu ya maisha binafsi na kuwa tayari kubadilika. Maisha ya awali hayapaswi kuwa ni nukta katika maisha, hayapaswi kuwa mwisho bali ni hatua nyingine ya kubadilika na kusonga mbele. Kauli kuu ni kujikubali, kupokea wongofu, kuitikia wito, kuwa kiumbe kipya na kuishughulikia Habari Njema ya Wokovu.
Mtume Paulo katika kukutana na Kristo alidhihirisha sifa fulani nzuri za kujifunza toka kwake. Akitoa mifano ya baadhi ya sifa hizo, Askofu Mkuu alifafanua: kutokuwa na kigugumizi, kutokusita katika suala zima la imani na utendaji wa kila siku; kuwa na ari ya kumwamini na kumfuasa Kristo kwa ujasiri hata ikibidi kutoa sadaka kubwa, Paulo alipata shida nyingi katika safari zake kama mawimbi ya bahari, alipigwa mawe na kadhalika, lakini aliona fahari katika Msalaba wa Kristo, na hivyo kushiriki mateso kwa imani.
Askofu Mkuu alifafanua kuwa ukristo unaoogopa mateso, ukristu unaopenda mambo rahisi rahisi ni upagani mamboleo; Jambo muhimu ni kuhuburi Injili kwa uaminifu. Paulo aliliona jukumu la kuhubiri kuwa ni Jukumu Takatifu, kwani alikuwa amekabadhiwa uwakili huo na kuwa mwaminifu, na kudiriki kusema “Ole wangu nisipoihubiri Injili”; alikuwa thabiti katika ukweli, akitafuta haki kwa nidhamu na heshima. Aliwaalika waamini wote wajisomee maisha ya mtume Paulo katika kitabu cha Matendo ya Mitume na katika Nyaraka zake.
Agizo la Kristo “Enendeni ulimwenguni kote mkaihubiri Injili” bado ni agizo hai mpaka leo, alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi. Ni wito ulio hai na makali yake mpaka leo na unahitaji uwajibikaji na utekelezaji kutoka kwa kila mkristu. Kwa namna ya pekee, aliwaalika Mashemasi Theophilus Kumalija na Bernardin Mtula kuizingatia sauti hiyo ya Kristo katika wito wao, waisikie kuwa ni hai na inawadai.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alielezea pia kuwa Jimbo kuu la Mwanza limekuwa na utamaduni wa kutoa daraja ya Ushemasi katika Seminari hiyo Ndogo ya Nyegezi ili kuhamasisha, kuwatia moyo na kukuza ari ya miito kwa wasemniari wadogo. Amewapongeza wazazi wa mashemasi hao na kuwaalika waamini wote waendelee kuombea miito mitakatifu ili Kristu azidi kuita vijana wengi anaopenda wamtukie kwa namna ya pekee.
Shemasi Theophilus Kumalija alizaliwa tarehe 07 Oktoba 1978 katika Kijiji cha Mwabagole Wilayani Kwimba, Mwanza. Malezi na mafunzo ya wito Mtakatifu alipata katika Seminari kuu za Kibosho, Moshi, kwa masomo ya Falsafa na Segerea, Dar es Salaam, kwa masomo ya Taalimungu (2005-2012).
Shemasi Bernardin Mtula alizaliwa 20 Mei 1981 katika kijiji cha Sumve wilayani Kwimba, Mwanza. Mafunzo na malezi alipatia katika Seminari Kuu za Kibosho, Moshi, kwa masomo ya Falsafa na Kipalapala, Tabora, kwa Taalimungu (2005-2012).
Itakumbukwa kuwa tarehe 08 Januari 2013 Jimbo kuu la Mwanza lilipata tunda la kwanza la Ushemasi kwa mwaka huu, Peter Madata kutoka Parokia ya Kabila, Mwanza. Kwa mapenzi ya Mungu, mashemasi hawa watapadirishwa mwaka huu kama ifuatavyo: Peter Madata 08 Agosti, Bernadini Mtula 22 Agosti na Theophilus Kumalija 05 Septemba.

Na Pd. Celestine Nyanda.
Jimbo kuu la Mwanza.








All the contents on this site are copyrighted ©.