2013-01-30 09:12:47

St. Thomas Aquinas, Nairobi yaadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu ilipoanzishwa


Seminari kuu ya Mtakatifu Tomas wa Akwino, iliyoko Jimbo kuu la Nairobi, Kenya, iliyoanzishwa na Shirika la Wadominikani, kunako tarehe 25 Januari 1963, imeadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu ilipoanzishwa. Hadi sasa wanafunzi 1069 wamehitimu masomo katika taalimungu na kati yao zaidi ya Mapadre 1,000 wanaendelea kutoa huduma za kichungaji ndani na nje ya Kenya.

Askofu mkuu Zacchaeus Okoth, wa Jimbo kuu la Kisumu, Askofu mkuu Peter Kairu wa Jimbo kuu la Nyeri na Askofu mkuu Boniface Lele wa Jimbo kuu la Mombasa ni kati ya Maaskofu 8 waliobahatika kusoma Seminarini hapo.

Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na umati mkubwa, iliongozwa na Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, kwa kushukuru waasisi wa Seminari hii ambayo imetoa mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa nchini Kenya katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Maadhimisho ya Jubilee hii yaliongozwa na kauli mbiu "Majiundo ya Kipadre katika Karne ya 21".

Kardinali Njue amewataka wananchi wa Kenya kuendelea kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa: kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo hapo tarehe 4 Machi 2013.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Okoth amewataka wanasiasa pia kujenga utamaduni wa huduma; haki na amani; wajikitahidi kuponya madonda ya utengano ambayo yamekuwa ni kiwazo kikubwa katika kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa kutokana na misigano ya kikabila na kijamii. Ili kujipatanisha na jirani, kuna haja ya kusamehe na kusahau, kwani hii ni sehemu ya kweli za Kiinjili zinazogusa undani wa mtu!

Seminari ya Mtakatifu Tomas wa Akwino imekuwa ni kiwanda kikubwa cha majiundo ya Mapadre kwa Kanisa Katoliki nchini Kenya pamoja na nchi wanachama wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki na Kati, AMECEA. Kanisa nchini Kenya katika maadhimisho haya limewakumbuka na kuwaombea Wamissionari, Mapadre na Watawa wote waliojitoa kimaso maso kutangaza Habari Njema ya Wokovu na matunda yake yanaonekana kwa sasa.

Maadhimisho haya yamekwenda sanjari na Kumbu kumbu ya Mtakatifu Tomas wa Akwino, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 28 Januari.







All the contents on this site are copyrighted ©.