2013-01-29 07:25:48

Mshikamano wa Baba Mtakatifu kwa ajali ya moto nchini Brazil: zaidi ya vijana 232 wamefariki dunia!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ametuma salam za rambi rambi kwa Askofu mkuu Helio Adela Ruper wa Jimbo kuu la Santa Maria kufuatia vifo vya vijana 232 walioungua moto wakati wakiwa kwenye Ukumbi wa Muziki wa Chuo Kikuu cha Santa Maria nchini Brazil.

Ujumbe huu umeandikwa kwa niaba ya Baba Mtakatifu na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican. Kuna zaidi ya vijana 130 waliopata majeraha makubwa na wengine bado wako kwenye chumba cha wagonjwa mahututi wakiendelea kupatiwa tiba.

Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea vijana wote waliopoteza maisha yao pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wanaoomboleza msiba huu mkubwa wa kitaifa. Baba Mtakatifu anawaombea faraja na matumaini ili waweze kupona haraka na kuendelea na shughuli zao za kila siku. Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil limetuma salam za rambi rambi na mshikamano wa upendo na wote walioguswa na msiba huu.

Askofu mkuu Helio Adelar Ruper anasema kwamba, watu wengi wamehuswa na msiba huu mkubwa, lakini Yesu Kristo anaendelea kuwa ni nanga ya matumaini yao katika shida na mahangaiko yao ya ndani. Ni mwaliko wa kila mtu kujiandaa kwani hakuna mtu ajuaye siku wala saa atakapokabiliana na Fumbo la Kifo. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yawe ni changamoto kwa kila mwamini kuweza kuimwilisha imani yake katika matendo yanayojikita katika fadhila ya matumaini na mapendo yanayojionesha katika huduma ya kidugu kwa Mungu na jirani.

Tukio hili limetendeka wakati ambapo Brazil inajiandaa kwa ajili ya kuwapokea mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaotarajia kwenda kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013, yatakayofanyika mjini Rio de Janeiro, Mwezi Julai, 2013.

Serikali ya Brazil imetangaza siku 30 za Maombolezo ya kitaifa, kama kielelezo cha umoja na mshikamano wa kitaifa wakati huu wa msiba mkubwa uliowagusa watu wengi zaidi. Serikali imeunda tume maalum ili kuchunguza chanzo cha moto huu.








All the contents on this site are copyrighted ©.