Maadhimisho ya Juma la Shule za Kanisa Katoliki Ireland
Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland, limefungua rasmi maadhimisho ya Juma la Shule
za Kanisa Katoliki nchini humo kwa kuwaalika wanafunzi, walimu, wazazi na walezi wanaounda
Jumuiya ya Shule, kuendelea kuadhimisha utambulisho wao kama taasisi za Kanisa Katoliki,
kwa njia ya maisha, masomo yanayotolewa pamoja na haki zote fungamanishi, tangu wakati
kengele ya kwanza inapogonga hadi ile ya mwisho inapoashilia kumalizika kwa siku na
hata wakati mwingine, nje ya kuta za shule.
Shule si majengo bali ni safari
inayofumbata maisha ya watu mbali mbali. Hapa ni mahali ambapo wanafunzi wanajenga
utamaduni wa urafiki wa kudumu, wanathamini elimu na maarifa waliyojipatia; ni kumbu
kumbu endelevu ya uzoefu na mang’amuzi, fadhila na tunu mbali mbali zilizorutubishwa
na kukuzwa hatua kwa hatua, ili hatimaye, ziweze kutoa mazao yanayokusudiwa.
Kanisa
Katoliki linatambua dhamana ya kutoa elimu bora na makini, itakayomwandaa mwanafunzi
katika maisha yake: kiroho na kimwili, ndiyo maana Kanisa linatoa kipaumbele cha pekee
katika mikakati ya kichungaji kuhusiana na elimu, kwani huu ni wajibu shirikishi na
utume ambao ni sehemu ya vinasaba vya Mama Kanisa, Shule zinazomilikiwa na kuendeshwa
na Kanisa Katoliki, ni Jumuiya za Imani na Yesu Kristo ndiye Kiongozi mkuu, anayewachangamotisha
kuendeleza ujenzi wa Fumbo la Mwili wake yaani Kanisa.
Juma la shule za Kanisa
Katoliki nchini Ireland kwa mwaka 2013 linaongozwa na kauli mbiu “shule ni Jumuiya
za Imani; fursa ya kushirikishana Habari Njema”. Maadhimisho haya yanayokwenda sanjari
na Mwaka wa Imani, iwe ni fursa kwa waamini kugundua ndani mwao ile furaha ya kuamini
pamoja na kuendelea kujitahidi kuwa karibu zaidi na Kristo katika Maadhimisho ya Sakramenti
za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Matendo ya huruma, yanayoonesha ushuhuda unaong’ara
ulimwenguni.