2013-01-29 09:39:19

Barua ya kichungaji kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia, 2013


Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia hivi karibuni limehitimisha mkutano wake mkuu uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu "Bwana anataka nini kwako? ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako". Imekuwa ni fursa ya kuangalia hali halisi ya nchi ya Zambia kwa kumshukuru Mungu kwa mema na ukarimu wake; daima wakitembea katika njia ya upendo, haki na huruma, ukweli na upendo.

Maaskofu katika ujumbe wao wanapembua kwa kina na mapana hali ya kisiasa nchini humo tangu walipoamua kufuata mfumo wa vyama vingi vya kisiasa, kunako mwaka 1991. Wananchi wa Zambia walitamani kuwa na uhuru mpana zaidi kwa kukumbatia mfumo wa vyama vingi vya kisiasa, lakini matumaini haya bado hayajafikiwa kutokana na kinzani zinazoendelea kujitokeza miongoni mwa Vyama vya Kisiasa, hali inayoonekana kwamba, wanasiasa wengi wana uchu wa madaraka na wanaoumia ni wananchi wa kawaida.

Maaskofu wanawaomba wanasiasa nchini Zambia kuonesha ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia, utu na heshima wanapotekeleza wajibu na dhamana yao katika Jukwaa la Kisiasa; daima wakitafuta mafao ya wengi na maboresho ya maisha ya maskini.Wanatoa mwaliko kwa Tume ya Uchaguzi Zambia kuhakikisha kwamba, inapanga na kuendesha chaguzi ndogo ili wananchi waendelee kuwa na wawakilishi katika maeneo husika. Hapa kila mtu anapaswa kutekeleza wajibu wake kikamilifu. Ni matumaini ya Maaskofu Katoliki Zambia kwamba, Katiba Mpya itaweza kutoa mwongozo maalum utakaoratibu chaguzi ndogo.

Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya wanasiasa wanajitafuta wenyewe na wako katika Jukwaa la kisiasa kwa ajili ya mafao yao binafsi, ndiyo maana wako tayari kuhama kutoka chama kimoja hadi kingine, ili kutafuta masilahi. Umefika wakati kwa wanasiasa kujitathmini na kujijengea jina kwa kuwa ni wanasiasa makini, waaminifu na wa kweli katika misingi wanayopigania wakiongozwa na dhamiri nyofu kwa ajili ya mafao ya Jamii.

Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia linalipongeza Jeshi la Polisi katika utekelezaji wa majukumu yake. Lakini bado kuna malalamiko makubwa ya matumizi mabaya ya madaraka ya umma dhidi ya vyama vya upinzani na vyama vya kiraia vinapotaka kufanya shughuli zao.

Jeshi la Zambia linapaswa kuzingatia maadili, kanuni na weledi katika utekelezaji wa majukumu yake ya kulinda na kusimamia sheria na utulivu bila ubaguzi wala upendeleo kwa Chama Tawala. Wanaitaka Serikali ya Zambia kutekeleza demokrasi kabla ya nchi haijatumbukizwa katika maafa, kwa kulinda na kudumisha ulinzi na usalama.

Maaskofu pia katika barua yao ya kichungaji wanaliangalia tatizo la Barotseland, sehemu ambayo bado kuna uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu, hali ambayo kamwe haiwezi kukubaliwa na kwamba, inapaswa kusitishwa mara moja. Serikali ijenge mazingira ya kirafiki ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huu, daima wakijitahidi kujenga na kudumisha majadiliano ya kweli bila vitisho.

Katiba ya Zambia inawahakikishia wananchi wote wa Zambia haki zao msingi; haki ya kuishi, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kujiunga na vyama pamoja na makundi mbali mbali bila kusahau uhuru wa dhamiri. Ni wajibu wa Serikali kulinda na kutetea haki hizi msingi kwa raia wake, kwani kwa sasa hali inazidi kuwa mbaya zaidi siku hadi siku. Serikali imekuwa ikitumia nguvu, vitisho pamoja na kuwatia mbaroni wanasiasa na raia wanaoonekana kuipinga Serikali. Maaskofu wanasema, Serikali inapaswa kuheshimu haki msingi za binadamu.

Mahakama ni kati ya mihimili mikuu mitatu ya dola inayopaswa kutekeleza majukumu yake kwa uhuru bila ya kuingiliwa. Kadiri siku zinazovidi kuyoyoma watu wanaanza kukosa imani na Mahakama. Wananchi wa Zambia wanasubiri kwa hamu mabadiliko makubwa ya Mahakama pamoja na kutaka utata unaoendelea kujionesha katika masuala ya Mahakama kupewa ufumbuzi wa haraka.

Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia kwamba, Muswada wa Katiba Mpya ya Zambia utaendelezwa, ili hatimaye, wananchi waweze kuwa na Katiba Mpya. Ili kufikia lengo hili, Serikali haina budi kutenga bajeti kwa ajili ya jukumu hili, ili hatimaye, wananchi waweze kupigia Muswada huu kura ya maoni kama wana ukubali au wana ukataa. Serikali katika maamuzi mengi imejikuta ikiyafanya peke yake kiasi cha kukosa uongozi shirikishi ambao ni muhimu sana katika kukuza na kuimarisha demokrasia.

Serikali badala ya kujenga utamaduni wa majadiliano na wadau mbali mbali, imejikita ikitoa matamko, kama ilivyofanya katika Sekta ya Elimu: uhusiano kati ya Serikali na Kanisa. Hapa kulihitajika majadiliano ya kina, ili kuweza kufikia uamuzi mzuri zaidi. Pamoja na mambo mengine, Maaskofu Katoliki Zambia wanasema, kuna haja ya Serikali kupitia Mamlaka ya habari na Teknolojia ya Mawasiliano Zambia (ZICTA) kusajili namba zote za Simu ili kudhibiti vitendo vya uharifu vinavyozidi kuongezeka kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano.







All the contents on this site are copyrighted ©.