Mwaka wa Imani iwe ni fursa ya toba na wongofu wa ndani
Baraza la Maaskofu Katoliki Korea katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa
na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, linabainisha kwamba, Mwaka
2013 umetengwa maalum kwa ajili ya kuhamasisha shughuli za Uinjilishaji Mpya kwa ari
na kasi kubwa zaidi, kwa kujitahidi kusoma alama za nyakati na kutumia njia mbali
mbali za mawasiliano ili kuweza kufikisha ujumbe wa Injili kwa hadhira inayokusudiwa.
Waamini walei
wanaalikwa kwa namna ya pekee, kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, wakitambua
kwamba, wanayo dhamana ya kuyatakatifuza malimwengu, changamoto iliyotolewa na Mababa
wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, yapata miaka hamsini iliyopita. Familia ya Mungu
nchini Korea, itambue wajibu wake wa kumtangaza Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha
adili na matakatifu. Lengo ni kuhakikisha kwamba, kabla ya kujimwaga katika utume
wa Uinjilishaji Mpya, Kanisa lenyewe linapaswa kujiinjilisha kwanza. Familia ya
Mungu nchini Korea katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, inapaswa kujikita katika
toba na wongofu wa ndani; kuimaraisha imani, matumaini na mapeno kwa njia ya maisha
ya Kisakramenti, Tafakari ya kina ya Neno la Mungu, Tafakari ya Mafundisho ya Mababa
wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, bila kusahau kujichotea utajiri unaofumbatwa katika
Mafundisho Jamii ya Kanisa, ambayo kimsingi ni Biblia ya Waamini walei katika mchakato
wa kuyatakatifuza malimwengu. Waamini wanapaswa kuhakikisha kuwa, imani yao inajionesha
katika matendo. Maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka ishirini ya Katekisimu Mpya
ya Kanisa Katoliki, iwe ni fursa kwa waamini kufanya tafakari ya kina kwa kushirikishana
kuanzia ndani ya Familia, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo, Parokia na Jimbo katika
ujumla wake. Familia ya Mungu ijifunze kushirikishana utajiri wa Nyaraka mbali mbali
za Kanisa kwa kutumia njia za mawasiliano zilizopo, ili kweli za Kiinjili ziweze kuwafikia
na kuwagusa wengi katika maisha na vipaumbele vyao. Maaskofu wanakazia kwa namna
ya pekee mikakati inayolenga kuimarisha Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, mahali ambapo
imani katika matendo inajionesha kwa kiasi kikubwa. Hapa ni mahali waamini wanaposhirikishana
utajiri wa Neno la Mungu;Maandalizi kwa ajili ya kupokea Sakramenti mbali mbali za
Kanisa pamoja na utekelezaji wa mipango ya shughuli za kichungaji. Waamini walei,
watambue dhamana na wajibu wa kujikita katika Uinjilishaji wa Jamii, kwa njia ya utakatifu
wa maisha; Utume wa Familia pamoja na kuwahusisha vijana katika maisha na utume wa
Kanisa, kwani hawa ni tegemeo la Kanisa kwa sasa na kwa siku za usoni. Vijana wakiwa
imara na thabiti, Kanisa linauhakika wa kuendelea kutekeleza utume wake hata kwa siku
za usoni. Maaskofu wanasema kwamba, kuna mambo kadhaa ambayo Waamini katika Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani wanapaswa kuyatekeleza kwa umakini, uchaji na moyo wa ibada. Wanapaswa
kuimarisha Imani, inayokuzwa na kukomaa katika maisha ya Sala; Mafundisho Tanzu ya
Kanisa; Katika Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi
Takatifu na ile ya Upatanisho na kwamba, matendo ya huruma yawe ni matunda ya Imani
tendaji. Waamini waongozwe na kauli mbiu inayowataka kuhakikisha kuwa Familia
ya Mungu inajikita katika kutangaza Injili. Itakumbukwa kwamba, Mwaka 2012, Baraza
la Maaskofu Katoliki Korea lilikazia umuhmu wa Sala katika Familia. Kipaumbele bado
kinaendelea kutolewa kwa utume wa Familia kwani Familia katika ulimwengu mamboleo
wanasema Maaskofu inakabiliwa na changamoto hasi zinazotaka kufifisha maana, utume
na dhamana ya Familia katika Kanisa na Jamii kwa ujumla. Vijana wahusishwe kikamilifu
katika maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu wa Kanisa Katoliki Korea wanasema kwamba,
kwa njia hii, kutakuwepo na uwezekano mkubwa wa kuona matunda ya Mwaka wa Imani katika
uhalisia wa maisha ya waamini wenyewe. Mwaka wa Imani, usipite na kuwaacha waamini
wakiwa wakavu kama kigae, bali iwe ni fursa ya kuifahamu, kuishuhudia na kuitangaza
Imani ya Kanisa Katoliki inayojikita katika Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Yesu
Kristo, Mkombozi wa Dunia.